Wednesday, September 5, 2012

Bei ya Mafuta yapanda Bongo..


MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli nchini ambapo bei ya petroli, dizeli na mafuta ya taa zimepanda.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Meneja Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo jana bei mpya zitaanza kutumika kuanzia leo.
"Sambamba na kupanda kwa gharama halisi za uagizaji wa mafuta kutoka kwenye Soko la Dunia, bei za jumla na rejareja kwa mafuta aina zote zimebadilika ikilinganishwa na taarifa iliyopita ya Agosti 1, 2012," ilieleza taarifa hiyo.
Kaguo katika taarifa hiyo alieleza kuwa bei za rejareja kwa Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa zimeongezeka, ambapo Petroli imepanda kwa Sh 291 kwa lita sawa na asilimia 14.50; Dizeli Sh 199 kwa lita sawa na asilimia 10.26; na Mafuta ya Taa Sh 67 kwa sawa na asilimia 3.47.
"Bei za jumla kwa kulinganisha matoleo haya mawili zimebadilika kama ifuatavyo: Petroli imeongezeka kwa Sh 291.54 kwa lita sawa na asilimia 15.07; Dizeli Sh 199.57 kwa lita sawa na asilimia 10.68 na mafuta ya taa kwa Sh 67.29 kwa lita sawa na asilimia 3.63," aliseleza katika taarifa hiyo.
Alisema kampuni za mafuta zipo huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani ilimradi bei hizo ziko chini ya bei kikomo kama ilivyokokotolewa na kanuni mpya iliyopitishwa na Ewura na kuchapwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 454 la Desemba 23, 2011.

No comments:

Post a Comment