Tuesday, September 4, 2012

Mgomo wa waalimu nchini Kenya....



Serikali ya Kenya imesema kuwa haiwezi kutimiza matakwa ya walimu wa shule za misingi wanaogoma nchini humo huku mgomo wao ukiingia siku ya pili.
Waziri wa elimu Mutula Kilonzo ameelezea BBC kuwa matakwa ya walimu ya kuongezwa asilimia miatatu ya mishahara yao haiwezekani kwa sababu pesa hizo hazikujuimshwa kwenye makadirio ya bajeti ya mwaka huu.
Waziri huyo aliongeza kuwa walimu hao walichezewa shere miaka kumi na tano iliyopita wakati walikubaliana na serikali wakati huo kwamba mishahara yao ingeweza kuongezwa kwa asilimia miatatu.
Maelfu ya walimu nchini Kenya walianza mgomo wao rasmi hapo jana wakidai kuwa serikali imekuwa ikipuuza kilio chao kuongezwa mishahara kwa miaka mingi.
Walimu hao ni wa shule za misingi na zile za upili na leo wamesusia kazi wakitaka nyongeza ya mishahara huku shule nyingi nchini humo zikiathirika.
Walimu hao wamekiuka agizo la mahakama lililoharamisha mgomo huo. Shule nyingi katika miji mikubwa mfano Mombasa, Nairobi na Nakuru zilisalia kufungwa.
Walimu wa shule za upili pamoja na wahadhiri wa vyuo vikuu wamesema watajiunga na mgomo huo baadaye wiki hii ingawa tayari wameanza kususia kazi.
Mgomo huu unajiri wakati shule zikifungua kwa muhula wa tatu kitu ambacho walimu hao wanasema sio hoja kwani wamekuwa wakigoma kila muhula wa tatu unapofungua kwa zaidi ya miaka kumi iliyopita wakidai hiyo nyongeza.
Wanasema kuwa serikali haina usawa katika mishahara kwa wafanyakazi wa sekta ya umma kwani ni hivi maajuzi tu wauguzi na wafanyakazi wengine wa umma walipoongezwa mishara baada ya kugoma. Wanadai kuwa walimu wamepuuzwa.
Mgomo huu umeonekana kufanikiwa kwani shule nyingi zimesalia kuwa bila walimu wanafunzi wengi wakibaki nyumbani.
Walikuwa wamebeba mabango yenye ujumbe kwa serikali kuwa wao hawawezi kula panya kwa mishahara midogo ambayo wanapata. Na vile vile walisema kuwa wamechoka na ahadi za uongo za serikali.
Mgomo huo uliitishwa na mashirika ya wafanyakazi yanayowakilisha takriban walimu laki mbili na nusu.
Wameahidi kuendelea na mgomo hadi matakwa yao yatakapotimizwa.
Chanzo: BBC Swahili

No comments:

Post a Comment