Friday, October 12, 2012

un YASHEREHEKEA SIKU YA MTOTO WA KIKE KWA MARA YA KWANZA DUNIANI...


Na: Mwandishi Maalum

 Kwa mara ya kwanza, jana Alhamisi, Umoja wa Mataifa umeadhimisha siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike kwa kutoa wito wa kukomesha ndoa za utotoni. Na kuhimiza elimu kama mkakati wa kuwalinda watoto wa kike dhidi ya mila hii potofu ya kuwaoza wakingali bado wadogo. Katika salamu zake katika maadhimisho hayo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon amesmea “ elimu kwa watoto wa kike ni moja ya mkakati wa kuwalinda dhidi ya ndoa za utotoni.

 Watoto wakike wakipata na fursa ya kukaa shuleni na kuepuka kuolewa mapema, wanajijengea uwezo na misingi ya kuwa na maisha bora kwao wenyewe na familia zao”. Akaongeza kwa kusema “ Hebu na tutimize wajibu wetu wa kuwaacha watoto wa kike wawe watoto wakike na sio wachumba”. Huku akizihimiza serikali, jamii, viongozi wa dini, vyama vya kijamii, sekta binafsi ,familia na hususani wanaume na wavulana kutetea haki za watoto wa kike.

 Mwezi wa Desemba mwaka 2011, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha Azimio linaloitangaza Octoba 11 ya kila mwaka kuwa siku ya kimataifa ya mtoto wa kike, dhumuni likiwa katika kutambua changamoto za msingi zinazomkabili mtoto wa kike duniani kote. Maudhui ya mwaka huu ya siku hii ya kimataifa ya mtoto wa kike ni “Utokomezaji wa ndoa za utotoni” Kwa mujibu wa taarifa za Umoja wa Mataifa, inakadiriwa kwamba leo hii kuna wanawake vijana zaidi ya milioni 70 walioolewa wakiwa chini ya miaka 18.

 Kielelezo kinachodhihirisha kwamba ndoa za utotoni zinamnyima na kumkatisha mtoto wa kike haki yake ya kupata elimu, na kupunguza fursa mbalimbali na kuongeza hatari ya kuwa mhanga wa vitendo vya kikatili na uharibifu wa afya yake. Katika maadhimisho hayo, ilielezwa bayana kwamba mtoto wa kike mwenye elimu duni anayonafasi kubwa ya kuolewa mapema na ndoa za utotoni zimedhihiria kuwa mwisho wa fursa ya elimu kwa mtoto wa kike.

 Aidha takwimu za Umoja wa Mataifa zimedhihirisha pia kwamba kwa wasichana ambao wamepata fursa ya kufikia elimu ya sekondari hawamo katika hatari ya kuolewa wakiwa na umri mdogo na hivyo kuthibitisha kwamba elimu ndio silaha sahihi ya kupambana na ndoa za umri mdogo.

Maadhimisho hayo hapa Umoja wa Mataifa yamefanyika sambamba na majadiliano yaliyohusisha viongozi mbalimbali akiwamo Askofu Mkuu Desmond Tutu na wawakilishi katoka Mashirika ya Umoja wa mataifa ya UNFPA, UNICEF, UN Women pamoja na maonesho ya picha zilizokuwa na maudhui “ bado ni mdogo mno kuolewa”.

 Aidha maadhimisho hayo ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike, yamefanyika ikiwa ni takribani kama siku mbili hivi kupita tangu kuuawa kwa Malala Yousufzai, msichana wa miaka 14 huko Pakistani kosa lake likiwa ni kupigania haki ya mtoto wa kike kwenda shule, msichana huyo aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wanaodaiwa ni wa kundi la Talban wakati akitoka shule.

 Kifo cha msichana huyo kimemfanya Katibu Mkuu Ban Ki Moon kuonyesha mshangao wake mkubwa dhidi ya kiwango cha matumzi ya nguvu, vurugu, ubaguzi na unyanyasaji ambao bado unaendelea katika karne ya leo dhidi ya mtoto wa kike.

 Akasema Ban Ki Moon, “ Kumshambulia mtoto huyo mtetezi wa haki ya wasichana kupata elimu ni kitendo siyo tu cha udhalimu bali ni uoga wakijinga ulioonyeshwa na magaidi dhidi ya nguvu ya elimu kwa mtoto wa kike.

Haiingi akilini mahali popote duniani ambako kitendo cha mtoto wa kike kupigania fursa na haki yake ya kupata elimu kikatafsiriwa kama kitendo cha ushajaa na kusababisha kukatisha uhai wake ”.


No comments:

Post a Comment