Thursday, November 29, 2012

Akaunti ya TFF yazuiwa...


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) lina imani kuwa mazungumzo kati yake, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yatamaliza tatizo la kushikiliwa akaunti ya TFF kutokana na malipo ya kodi ya mishahara ya makocha wa kigeni.
Rais wa TFF, Leodegar Tenga alizungumza na waandishi wa habari jana juu ya uamuzi wa TRA kushikilia akaunti ya TFF ikiielekeza Benki ya NMB kukata sh. 157,407,968 ikiwa ni malipo ya Kodi ya Mapato ya Mshahara wa Mfanyakazi (P.A.Y.E) ya makocha Marcio Maximo na wasaidizi wake.
Katika mzozo huo wa muda mrefu, TFF imejitetea kuwa haiwezi kulipa kodi hiyo kwa kuwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ndiyo mlipaji wa mishahara ya makocha hao, ikiwa ni ahadi ya Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete ya kulipia makocha wa michezo tofauti, ukiwemo mpira wa miguu.
“Hili ni suala nyeti ambalo linahitaji kumalizwa kwa mazungumzo baina ya pande zote. Ninataka kuwahakikishia kuwa suala hili linazungumzwa na tayari nimeshafanya mazungumzo na maofisa wa Wizara na tumekubaliana kukutana na pande zote wakati wowote; iwe leo jioni au kesho.
“Ni matumaini yangu kuwa suala hili litakwisha na jana nimetoka Kampala (Uganda kwenye Kombe la Chalenji) moja kwa moja na kwenda kuzungumza na viongozi wa Wizara na wamekubali kwamba tuongee pande zote kulimaliza suala hili.
“Nimezungumza na wenzetu wa Serikali kwa sababu najua unyeti wa suala hili. Fedha zilizokamatwa si zetu; ni fedha za klabu na zimetolewa na mdhamini ambaye tumekubaliana namna ya kuzitumia. Fedha hizi hazikutolewa kwa ajili ya kulipia kodi. Lakini TRA wanazishikilia kwa sababu Premier League iko chini ya TFF,” amesema Rais Tenga.
Tenga amesema TRA wanafanya kazi kwa kufuata sheria zao za ukataji kodi na hivyo wana haki ya kufuatilia kwa kuwa kwa mujibu wa sheria, mwajiri ndiye anayetakiwa kukata kodi kutoka kwenye mshahara wa mfanyakazi.
“Hivyo hatuwezi kuilaumu TRA kwa sababu ndivyo sheria inavyosema, lakini pia hatuna uwezo huo wa kulipa fedha hizo kwa sababu, kwanza hatuna na pili sio sisi tunaolipa mishahara ya hawa makocha,” amesisitiza Rais Tenga.
Akizungumzia historia ya suala hilo, Tenga aliishukuru Serikali kwa msaada ambao imekuwa ikiutoa katika mpira na kwamba ahadi ya Rais Kikwete ya kusaidia kulipa makocha wa timu za taifa imeusogeza mpira wa miguu karibu na Serikali na karibu na Rais.
“Rais Kikwete alisema wakati alipoingia madarakani (mwaka 2005) anajua kuwa kuna tatizo kwenye mpira na akatoa ahadi ya kulipa walimu wa mpira. Ahadi hiyo imefanya ukaribu uliopo sasa kati ya mpira na Serikali; kati ya mpira na Rais sasa kuwa mkubwa. Serikali imechangia kwa kiasi kikubwa kwenye mpira, yaani kulipa walimu.
“Sasa sisi ni administrators wa hawa walimu. Tunachofanya ni kuandaa mikataba ambayo ni standard duniani kote kwa mujibu wa taratibu za FIFA (Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu). Kwa kawaida makocha wa kigeni huwa wanatayarishiwa mikataba ambayo ni tax free (isiyo na kodi). Baada ya kuingia nao mikataba, huwa tunaipeleka wizarani ambao ndio wanawalipa makocha moja kwa moja kwenye akaunti zao,” amesema Rais Tenga.
Katika mkutano huo na waandishi, Rais Tenga pia aliipongeza timu ya taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars kwa kuanza vizuri mashindano ya Kombe la Chalenji, akisema ushindi huo ni ishara nzuri hasa kutokana na ukweli kuwa kikosi hicho kinaundwa na wachezaji wengi chipukizi na akataka Watanzania waendelee kuiunga mkono.
Tenga pia alisema kumekuwepo na malalamiko kuhusu makato ya mechi na kwamba suala hilo ni la muda mrefu na kwamba TFF imepiga hatua kubwa tangu ilipoanza kulishughulikia.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment