Tuesday, November 6, 2012

Kufungwa mfululizo kwa simba, ati sababu ni ngono...?

Kocha wa simba akiwa na wenzake katika benchi la ufundi wakiumiza kichwa.

                                                      Beki wa Simba Shomari kapombe huyu.

                  Wachezaji wa simba wakiwa hawaamini kilichotokea juzi katika uwanja wa jamhuri.


Na Baraka Mbolembole, Aliyekuwa Morogoro

Kwa takribani miaka sita nimekuwa karibu na kambi ya Simba Sports Club, hasa inapokuwa inakabiliwa na michezo katika Manispaa ya Morogoro. Kabla sijaanza kuandika nilipenda kuwa karibu na timu hiyo kwa sababu ya kujifunza baadhi ya maisha ya wachezaji wa ligi kuu. Zaidi mimi ni mshabiki wa timu hii tangu kuzaliwa kwangu. Nikaona ni bahati kubwa kwa timu ya ndoto kuja mtaani kwetu na kuweka kambi ya muda mrefu wakati ule uwanja wa Uhuru, ulipofungwa kwa matengenezo madogo. 


Na hata wakati ule wa michuano ya ligi kuu ndogo, kwani, Simba, ilikuwa imepangwa katika kituo cha Morogoro. Mida ya asubuhi na jioni, ndiyo huwa napendelea kuichunguza timu hii, kwani huo ndiyo muda wa soka kwa mwanasoka, muda anao amka na anao lala nilipenda kutambua na kujifunza kutoka kwao. Nilikuwa na miaka 20 tu, na nilitamani kuwa mwanasoka kama wao ( wale wa Simba) pia nilipenda kuwafuatilia sababu pia ni timu niipendayo. 



Lakini kwa mara ya kwanza niliona kichefuchefu, nakumbuka kuna mwandishi mmoja ambaye alikuwa akiandika katika magazeti ya BINGWA na DIMBA, na sasa anaandika katika gazeti moja la michezo linalotoka mara mbili kwa wiki, nikamtumia sms na kumwambia, " Kaka, huyu, daah! Nimemkuta (Jina la mchezaji kapuni) katika uchochoro fulani hivi na ka- house girl, wa nyumba ya mshkaji na kesho wanacheza mechi na Ashanti United ( wakati ule wa ligi ndogo), hivi huwezi kuwaandika hawa, Kaka?" Sikuwahi kujibiwa sms hii na hadi leo kalamu ya mwandishi huyu haijawahi kuandika chochote kuhusiana na mambo kama haya. 



Nilipopata nafasi ya kushika kalamu nikasemea " Asante... Kuna siku nitaitumia kalamu yangu kuandika mambo haya kwa uwazi na ukweli, na kamwe haitamuhukumu Mwanasoka. Itamuhukumu ' hawala wa mchezo' ambaye amevamia mchezo hasioufahamu miiko ya mchezo. Kwani Mwanasoka akiwa anatakiwa kuwa mwadilifu wa kambi na ayefuata kanuni husika za klabu na miiko muhimu ya kuzingatia ili kulinda kiwango chake kwa manufaa yake na klabu yake. Lakini kwa Mwanasoka kamwe hataichukia kalamu hii zaidi ya kuipenda na kuisifia, kwani itawaondoa ' mamluki wanaowatia nuksi' katika malengo yao. Haya ndiyo madudu ya KLABU YA SIMBA SC ilipokuwa Morogoro. 



SIKU SITA ZA SIMBA MORO NA POINTI YAO MOJA: NA KOCHA MILOVAN
 
Simba ilifikia katika, Hotel ya Usambara, ambayo humilikiwa na Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Mzee Yusuph Makamba. Kuna wachezaji waliolala katika vyumba vya gharama ya 20,000, na wapo waliolala katika vile vya gharama ya 25, 000. Kocha Milovan Curkovic, yeye aliandaliwa chumba cha gharama ya 50, 000. Vikaanza vioja. Kocha akakataa kufikia Hotel isiyo na huduma ya Internet. Viongozi kwa kushirikiana na Meneja wa Hotel hiyo wakamtafutia Kompyuta yenye huduma ya Internet, lakini, Milovan, akakataa na kusema kwa kiswahili kizuri 'Nataka yenye wireless' viongozi wachache tena wa ngazi ya chini, wakashindwa na kuingia katika mtego wa Milovan, ambaye tangu awali alionesha kutotaka kukaa katika Hotel ile. Golikipa wa makipa wa timu hiyo akasema ' Hana lolote, hakuna cha Internet wala nini anataka Mwanamke tu huyo kocha hamna kitu na sasa anaongea hadi Kiswahili...' alikuwa akiongea mbele ya wachezaji wachache. 

Milovan, akaamishiwa katika hotel yenye hadhi zaidi na gharama ya chumba ni zaidi ya 60, 000. Hakwenda pamoja na timu akitokea hotelini. Simba walitoka zao kivyao kutokea, Usambara, Milovan, akatokea ARC Hotel. Wakapata pointi moja mbele ya Polisi Moro. 

WACHEZAJI:
 

Walikuwa huru sana na walionekana kupitapita baadhi ya mitaa. Hawakuwa na kiongozi imara. Na hata meneja, Nico Nyagawa, hakuweza hata kuwaonya katika lugha ya mpira. Yote sababu Nyagawa naye anatambulika kama mchezaji klabuni hapo na mkataba wake unamalizika punde na kuna timu anakwenda kuichezea katika mzunguko wa pili wa ligi kuu msimu huu. Angesema nini? Angemkanya nani? Tatizo la wachezaji likaanzia kutokuwa na uongozi kambini, kocha yupo umbali kiasi na hata nahodha, Kaseja, hayupo sawa kiutulivu, kuna mambo mabaya anayaona yakifanyika lakini anatetea ajira yake. Unajua kwa nini alilia sana? 



SIKU MBILI KABLA YA KUIVAA MTIBWA

Katika hotel, ambayo wachezaji walifikia, na kuwepo hapo chini ya uongozi wa " Kishkaji na Majungu" wakaingia wapangaji wengine, walikuwa kundi kubwa la wasichana zaidi ya 300. Pakawa hapotoshi. Wasichana hawa ni wale wakaguzi wa vyuo vya juu. Nao wakapigwa na bumbuwazi, waliona kama ndoto vile kukutana na mastaa wa soka nchini. Waliwaona, Mrisho Ngassa na utitiri wa majina makubwa katika soka la nchi yetu.

Ukawa mtihani mkubwa. Mwenye mbinu bora ndiye angeufaulu. Baadhi ya wasichana wakaamua kubaki pale na kutandika vya kulalalia kwani, hotel zote za jirani zilijaa. Mtego ukaanzia hapo. Na baadhi ya wasichana walifauru vizuri, kwa sababu walikuwa na mbinu na maarifa zaidi ya baadhi ya mastaa wa Simba. Wenye uchu na tamaa walinaswa kirahisi na wakachangia asilimia 75 ya kipigo cha timu yao mbele ya Mtibwa.

 
KIGGY MAKASI NA WENZAKE NA KUNDI WA WAPENDA NGONO SIMBA
Katika miaka ya 90, timu ya Liverpool ilikuwa na kikosi bora cha mchanganyiko wa wachezaji wazoefu na wale wenye umri mdogo, na waliokuwa wakisifika kwa mchezo wa mzuri. David James, Robbie Fowler, Jammie Reddknapp, Steve McManamann, Paul Ince, walikuwa wachezaji bora katika soka la Uingereza, lakini hawakuwahi kupata mafanikio yoyote hadi pale walipotawanyika katika timu hiyo. Chini ya nyota hawa, Liverpool, ikaanza kupoteza makali uwanjani na kuwa wapambaji wa magazeti, baada ya nyota hao niliowataja kuimarisha zaidi jina lao la " Spice Boys" na kuwa maarufu na bora zaidi nje ya uwanja, wakitumia muda mwingi kujirusha na kuiporomosha timu yao.
Wakati Kiggy Makasy akiwa bado anajiuguza, alikuwa mchezaji wa kwanza wa Simba, kuwatia ' nuksi' alifanikiwa kumpata mwanachuo, mmoja ambaye alikosa chumba na kwenda kulala naye. Sijui walichofanya, macho yangu yaliishia hapo. Ghafla nikamuona Mrisho Ngassa, anashuka maeneo ya jirani ambako kuna wanachuo walifikia alichelewa sana kurejea katika chumba chake. Pia waliongiza wasichana katika vyumba vyao ni Nassoro Chollo, ambaye alifungisha bao la pili kwa kupiga ' pasi mkaa' kwa, na wengine ambao binafsi niliwaona ni, Ramadhan Chombo na mchezaji mmoja hivi simtaji kwa heshima ya ndoa yake changa. Ilikuwa ni usiku wa Jumamosi, kuamkia siku ya mchezo, Jumapili na wakachezea za kutosha tu, pale, Jamhuri. Chollo, Ngassa, Redondo, wote waliwekwa nje katika kipindi cha kwanza. Na hata, walipoingia walifanya nini? Chollo kumtoa machozi Kaseja, kwani hakuwa fiti kabisa na kama angekuwa fiti angesogea na mpira mbele lakini alilala na msichana akawa na uchovu, taabu ya nini? Akachoma, lango lake. 


JUMA KASEJA
Kwa kipindi chote tangu naanza kumfahamu miaka kumi, iliyopita, nimegundua, tabia nyingi za ajabu kuhusu, nahodha huyu wa Simba na Taifa Stars. Ni msiri sana, mcheshi, mwenye kupenda ushirikiano, anayejituma, mwenye hitaji la ushindi katika moyo wake. Lakini, kama mwanadamu mwingine, Kaseja, naye ana wivu. Wivu wa kufanikiwa na kuendelea kuwa juu. Nadhani vitu hivi ndivyo vilivyomsaidia sana kuwa miongoni mwa makipa bora kuwahi kutokea nchini. Atakumbukwa kwa mengi sana mazuri, ambayo ameyafanya katika wakati wake na hadi sasa bado namtambulisha kama ' Hasiyegusika wala kufananishwa" Nani kama yeye? Nani anayekuja kuvaa ' glovu' zake? Hakuna, hilo ndiyo jibu sahihi. Kwa muda wote wa uwepo wa timu pale hotelin, Kaseja aliweka akili yake katika michezo miwili ya timu yake dhidi ya Polisi Moro na Mtibwa, alikuwa muda mwingi mwenye kuswali.
 


SHOMARI KAPOMBE: 
" Masikini, Kapombe, amegombana na Kaburu, hadharani vile... Sijui maisha yake yatakuwaje, Simba?" Ni maneno ya mwanachama mwandamizi wa Simba, akizungumzia kitendo cha mlinzi kinda wa timu hiyoa Kapombe, kurushiana maneno makali na Makamu Mwenyekiti wa klabu yake, Geofrey Nyange Kaburu, ambaye alikuwa akimshutumu Kapombe kama sehemu ya kufungwa kwa timu yao na Mtibwa Sugar. Awali wakati mchezo ukienda mapumziko, Kapombe alionekana kuanza kumrushia maneno makali ya kumshutuma Felix Sunzu. Kabla ya Sunzu, kuanza kumjibu, lakini haraka, Kaseja, akawatuliza.
Wakati wakiwa, hotelin, mlinzi wa kimataifa kutoka Kenya, Paschal Ochieng, alikuwa akiwaambia, Amir Maftah na Kapombe, kuwa wawe makini, kwani ndiyo waliochangia, Polisi Moro, kupata, bao wakati wa mchezo baina yao. Akawa anawaelekeza maeneo ambayo walitakiwa kuwepo, alimwambia, Maftah, kuwa alipitika kirahisi na kuruhusu, krosi ambayo ilizaa bao pekee la Polisi, na akamwambia, Kapombe, kuwa hakuwa katika eneo sahihi kama mlinzi wa kati. Kapombe, akamjibu ' hata wewe hukuwa katika eneo lako'. Dogo, huyu hivi ameota ' majipu kwenye kwapa zake' naye ' hagusiki' kwa mpira gani? Ule wa kukimbizwa na ' Babu, Kisiga?' chunguza vizuri sababu ya mabao waliyofungwa Simba na Polisi kisha Mtibwa Sugar, utagundua kuwa Kapombe hagusiki Simba. 


MSIKILIZE OBADIA MUNGUSA ANAVYOMZUNGUMZIA KABURU 
" Unajua hivi sasa sipo na timu, kuna mambo hayapo sawa kati yangu na Bosi, Kaburu. Unajua yeye ndiye aliyenisainisha mkataba wakati nasajiliwa na Simba, hivyo kila kitu ananisimamia yeye" anasema mlinzi huyo ambaye hayupo kikosini hivi sasa. ' Unajua wakati wananisajili kuna makubaliano ambayo kimsingi pande zote zilitakiwa kuyatekeleza, lakini haikuwa hivyo. Ndipo nikajaribu kuulizia mbona makubaliano wanayakiuka na wala hayakuwa kama hali ilivyokuwa, Ikawa, kosa, kwanza alinionesha dhaharu kubwa sana, pia aliniambia wazi naweza kuondoka, kwani sina nafasi ya kucheza. Akaniambia wewe tafuta tu timu, Simba huna nafasi. Sikuwa na jinsi nikatafuta timu nyingine, lakini kuna wachezaji wanaonekana wana thamani zaidi ya wengine kikosini, labda hiyo ndiyo sababu ya wachezaji wengine kudharaulika. Ukitazama aliwaleta wachezaji kama Kanu Mbiyavanga, Linno Musombo na Mussa Mudde baada ya kuwapatia pesa nyingi, lakini walifanya nini walipokuja? Kwa nini pesa kama ile tusipewe wazawa? Kwani hao wageni hawana jipya lolote" 

" Unajua nimerudishwa sana nyuma kwa kipindi ambacho nimekuwa, Simba, lakini nimejifunza mambo mengi sana kama mchezaji wa soka. Lakini nitabaki namshangaa, Kaburu kuanzia namna anavyoyachukulia matatizo ya wanadamu wenzake hadi katika uongozi wake wa soka. Unajua usajili anafanya yeye, si mbaya lakini amekuwa akikurupuka sana kwani akiambiwa mahali fulani kuna mchezaji anakwenda na kumsajili, na ndiye aliyewaleta kina, Ochieng baada ya kina Musombo kuonekana si wachezaji wazuri, pia amekuwa akiingilia hadi mambo ya utawala wa benchi la ufundi, sasa unabaki unajiuliza huyu ni kiongozi wa soka kweli?"
 

Je, kama mambo yatawekwa sawa na kupewa anachodai, Mungusa anaweza kurejea katika timu hiyo?
 
" Nina uchungu sana na kilichonitokea katika klabu hiyo ( Simba) kwanza mtu unakuwa na majeraha ya mara kwa mara tena yasiyoeleweka, halafu unakuta tena kwenye malipo wanakuzingua, mimi nina majukumu yangu pia. Kuna viongozi wamekuwa wakinipigia simu na kuniambia nirejee kikosini na nijishushe kwa Kaburu, kwa madai kuwa ndiyo tabia yake. Lakini sidhani mana nina hasira nao sana"
" Kwa mfano mechi ya juzi hadi yule mtoto kacheza! Simba ndiyo imekuwa hivyo sasa?" anahoji mlinzi huyo mwenye miaka 24. " Kama ipo ipo tu, nasubiri dirisha dogo kujua nini kitatokea"


OKWI NAYE NI TATIZO KUBWA SIMBA SC 

Ni mchezaji mzuri sana na anajitolea kwa timu yake, lakini ni kama kila mtu ndani ya timu hiyo ameekeza nguvu zake kwa Mganda huyu kitu ambacho ni hatari. Kuna tetesi za chinichini kuwa baadhi ya wachezaji wazawa wamekuwa wakichukia kuona Okwi anavyotazamwa zaidi ndani ya timu hiyo kuliko wachezaji wengine. Ni lazima timu itazame upya namna ya kucheza michezo mfumu bila Okwi kwani tayari wapinzani wengi wamekuwa wakimuandalia mikakati ya kumzima na sasa wameanza kupata dawa yake. Amewaambia wapenzi na mashabiki wa timu hiyo kuhama na kutafuta timu nyingine ya kushangilia kama wanaumizwa zaidi kuliko wao na matokeo ya timu hiyo hivi sasa. Hi ni kauli ya mwisho inayoweza kuthibitisa kuwa hivi sasa yeye ndiye staa zaidi kikosini. Ameingia katika mzozo mkubwa na wachezaji wazawa kwa sababu ya dharau zake.



MENEJA/ MISHAHARA YA MAPROO
 
Simba inatakiwa kuwa na meneja imara na mwenye kuripoti taarifa za siri kwa uongozi kuhusiana na wachezaji ambao hukiuka miiko ya kambi na kuchangia matokeo mabaya uwanjani. Nyagawa hawezi jukumu hili. Mishahara ya wachezaji wengi wa kigeni ndani ya timu hiyo kwa miaka ya karibuni imekuwa ghali sana, na hilo limepelekea sononeko lisilokwisha kutoka kwa wachezaji wengi wazawa, ambao hulipwa mishahara kiduchu, wale wazawa wanaoona wenzao wanapendelewa mno wakati hawatoi matunda mazuri uwanjani. Nalo hili litazamwe.

Picha zote pamoja na habari ni kwa hisani ya blogu ya Shaffih dauda mwanamichezo mashuhuri na mtangaziji wa radio na TV Clouds ya jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment