Friday, November 23, 2012

Madiwani wa chadema kuwalipa chadema gharama za kesi waliyoshindwa...


Na:Na Mussa Juma

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, imewaamuru madiwani watano waliotimuliwa Chadema kulipa gharama za kesi waliyokuwa wamefungua kupinga kufukuzwa uanachama, vinginevyo watapelekwa magereza.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Charles Magesa alitoa hukumu hiyo jana baada ya Chadema kushinda kesi hiyo.Hakimu Magesa alisema madiwani hao wanapaswa kulipa Sh15 milioni ndani ya miezi miwili, wakishindwa watapelekwa gerezani.

Madiwani hao ni Estomih Mallah (aliyekuwa Naibu Meya ya Manispaa ya Arusha kipindi hicho), John Bayo aliyekuwa Diwani wa Elerai, Reuben Ngowi (Themi), Charles Mpanda (Kaloleni) na Rehema Mohamed aliyekuwa Diwani wa Viti Maalumu.

Pia, katika kesi hiyo ya madai Chadema walikuwa wakiwakilishwa na Wakili Method Kimomogoro, wakati wadaiwa hao walikuwa wakijitetea wenyewe baada ya aliyekuwa wakili wao kujitoa.Akisoma uamuzi huo, Hakimu Magesa alisema baada ya mahakama kupitia hoja za pande zote, imeona wadaiwa hao wanapaswa kulipa zaidi ya Sh15.1 milioni, kila mmoja anatakiwa kulipa zaidi ya Sh3.2 milioni katika kipindi kisichozidi miezi miwili.

Awali, kulikuwa na mvutano kati ya wadaiwa hao jambo lililosababisha kesi hiyo kusikilizwa kwa kipindi kirefu ambapo walitakiwa kueleza mahakama hiyo sababu ya kutokupelekwa gerezani, huku kila mmoja akitamka kiwango cha fedha ambacho angeweza kulipa kwa mwezi.

Kwa upande wake, Ngowi alisema ana uwezo wa kulipa Sh25,000 kwa mwezi, Mpanda Sh20,000, Mallah Sh20,000, Rehema Sh15,000 na Bayo Sh15,000 kwa mwezi bila kuonyesha mchanganuo wa kipato chao, jambo lililopingwa vikali na Wakili Kimomogoro kwamba kiwango hicho ni kidogo.

Hakimu Magesa alisema kisheria mtu akishinda kesi ana uwezo wa kuchagua hukumu ya kulipwa kwa kuchukua mali za mdaiwa au mlalamikiwa kupelekwa kifungoni.

“Kimsingi mtu anaposhinda kesi lazima alipwe gharama aliyotumia na iwapo mahakama itaridhia alipwe kwa kiwango hicho, itachukua muda mrefu kati ya miaka 10 na 16 kumaliza deni hilo, jambo litakalosababisha aliyeshinda kushindwa kuona matunda ya ushindi wake,” alisema Magesa.

Alisema fedha hizo wanapaswa kuzilipa mara mbili,  awamu ya kwanza inatakiwa kila mmoja kulipa zaidi ya Sh1.5 milioni na  wawe wamemaliza kwa miezi miwili na kwamba, iwapo watashindwa mdai anaweza kupeleka mchanganuo wa gharama za kumtunza mfungwa na mahakama kuupitia na baadaye kutoa amri wapelekwe gerezani

No comments:

Post a Comment