Thursday, November 8, 2012

Uamsho waendelea kusota rumande kwa kukosa dhamana tena.


Na Maelezo Zanzibar 08/11/2012

Kesi inayomkabili Shekh Farid Hadi Ahmed na wenzake sita wa Jumuiya ya UAMSHO na Mihadhara ya Kiislam imeakhirishwa leo hadi terehe 20 mwezi huu.

Akitoa maamuzi hayo Mrajisi wa Mahakama kuu Zanzibar iliyopo Vuga George Kazi amesema kuwa uamuzi huo umetokana na kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Kwa upande wa Wanasheria wa watuhumiwa walielezea juu ya haki ya washitakiwa wao kupatiwa dhamana lakini dhamana hiyo hawakupatiwa na kurejeshwa Rumande hadi tarehe 20 mwezi huu.

Washitakiwa hao ni Farid Had Ahmed (41) wa mkazi wa Mbuyuni, Mselem Ali Mselem(52)wa Kwamtipura, Mussa Juma Issa (37) wa Makadara, Azan Khalid Hamdan (43) wa Mfenesini, Suleiman Juma Suleiman (66) wa Makadara,Khamis Ali Suleiman (59) anayeishi Mwanakwerekwe pamoja na Hassan Bakar Suleiman (39) mkaazi wa Tomondo.

Watuhumiwa wote walishitakiwa kwa kosa la uchochezi wa kufanya fujo kinyume na kifungu cha 45 (a) (b) cha sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar.

Ilifahamishwa kuwa Agosti 17 mwaka huu majira ya saa 11:00 za jioni huko Magogoni Msumbiji Wilaya ya Magharibi Unguja, wakiwa ni Wahadhiri kutoka Jumuiya ya UAMSHO na Mihadhara ya Kiisalam, walitoa matamko ya uchochezi yanayoashiria uvunjaji wa Amani na kusababisha fujo,maafa mbalimbali na mtafaruku kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR 

No comments:

Post a Comment