Thursday, January 17, 2013

Charles Taylor alia na bunge la nchi yao....


Aliyekuwa rais wa Liberia Charles Taylor ambaye amezuiliwa kwa makosa ya jinai, amewaandikia barua wabunge wa nchi hiyo na kuwataka wamlipe malipo yake ya uzeeni dola 25,000.
Katibu wa baraza la senate, Nanborloh Singbeh amesema kuwa barua hiyo itaweza kujadiliwa na wabunge katika kikao cha wiki ijayo.
Barua hiyo inayosemekana kutoka kwa Taylor inasema kuwa kubana malipo yake ya uzeeni ni dhulma kubwa kwake.
Mwezi Mei mwaka jana, mahakama iliyokuwa inasikiliza kesi za ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Sierra Leone, ilimhukumu Taylor miaka 50 gerezani kwa makosa 11 ya ukiukwaji wa haki za binadamu.
Taylor ndiye rais wa kwanza wa zamani kufungwa jela na mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita tangu kesi zilizowahusu waliokuwa watawala wa Nazi baada ya vita vya pili vya dunia.
Hata hivyo Taylor, amekata rufaa dhidi ya hukumu hiyo iliyotolewa na mahakama maalum ya Sierra Leone iliyoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.
Iliamua kuwa Taylor, aliunga mkono waasi waliofanya uasi nchini Sierra Leone wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka 1991-2002.
Mwandishi wa BBC Jonathan Paye-Layleh mjini Monrovia anasema kuwa saini iliyo kwenye barua hiyo inafanana sana na ile ya bwana Taylor.
Hata hivyo, imebainika kuwa barua hiyo ina makosa kadhaa ya kisarufi,
Kilio cha Taylor kimesababisha maswali kuhusu ikiwa Taylor ndiye aliandika barua hiyo.
Hata hivyo, shemeji yake Taylor Arthur Saye aliambia waandishi wa habari kuwa rais huyo wa zamani ndiye aliandika barua hiyo.
Chanzo: BBC Swahili

No comments:

Post a Comment