Thursday, January 17, 2013

Hatimae Gardiola aangukia Bayern Munich


Pep Guardiola, mwenye umri wa miaka 41, awali ilidhaniwa angelijiunga na Chelsea, au Manchester City, zote za Uingereza.
Guardiola ametia saini mkataba wa miaka mitatu na Bayern Munich, hadi mwaka 2016.
Atachukua madaraka ya Jupp Heynckes, ambaye ameamua kustaafu.
Siku zake akiwa mchezaji, Guardiola, aliwahi kuvichezea vilabu vya Barcelona, Brescia, Roma, Al.-Ahli, Dorados na pia timu ya taifa ya Uhispania.
Alikabidhiwa pia tuzo nyingi akiwa mchezaji.
Katika kazi ya meneja, amewahi kuchukua ubingwa wa ligi kuu ya Uhispania, La Liga, mara tatu, ushindi wa Supercopa de Espana mara tatu, mara mbili kutwaa ubingwa wa Copa Del Rey, ubingwa mara mbili wa klabu bingwa barani Ulaya, mara mbili Kombe la Uefa na vile vile mara mbili ubingwa wa Kombe la Dunia la FIFA kwa upande wa vilabu.
Guardiola, ambaye alizaliwa tarehe 18 Januari, mwaka 1971, Santpedor, Uhispania, tangu kuondoka uwanja wa Nou Camp mwezi Mei mwaka 2012, amepumzika msimu mzima, baada ya kukiwezesha klabu kupata jumla ya vikombe 14, ikiwa ni pamoja na ushindi wa klabu bingwa barani Ulaya mara mbili.
"Tumefurahi sana tumefanikiwa kumshawishi mtaalamu wa soka Pep Guardiola kuja Bayern Munich, ambaye vilabu vingi vikuu vilimtamani na kuwasiliana naye," alieleza mkurugenzi mkuu wa Bayern, Karl-Heinz Rummenigge.
"Yeye ni kati ya makocha waliofanikiwa sana duniani, na tuna hakika kwamba sio tu ataiwezesha klabu ya Bayern kung’ara, lakini hata soka ya Ujerumani kwa jumla."
Bayern kwa hivi sasa inaongoza katika ligi kuu ya Ujerumani ya Bundesliga, na itapambana na Arsenal ya Uingereza mwezi ujao, ikiwa ni miongoni mwa timu 16 zilizosalia katika michuano ya klabu bingwa barani Ulaya.
Heynckes, mwenye umri wa miaka 67, kabla ya siku kuu ya Krismasi alikuwa ameifahamisha klabu hiyo inayocheza katika ligi kuu ya Bundesliga kwamba hana nia ya kutia saini mkataba mpya baada ya msimu huu.
Mkataba wake utakwisha tarehe 30 mwezi wa Juni, na Guardiola atachukua mahala pake siku itakayofuata.
Chanzo: BBC Swahili

No comments:

Post a Comment