Sunday, January 6, 2013

Hatimae muafaka wapatikana Sudan zote mbili...


Marais wa Sudan na Sudan Kusini wameafikiana kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa mwaka jana.
Viongozi hao walimaliza mkutano wao wa siku mbili mjini Addis Ababa Jumamosi.
Mvutano baina ya nchi mbili hizo umekuwa tishio kubwa katika eneo lao.
Wapatanishi wa Umoja wa Afrika (AU) wataweka ratiba ya kutekeleza makubaliano yote ambayo bado hayakufwatiliwa.
Ratiba hiyo itakuwa tayari mwisho wa juma lijalo, kwa mujibu wa taarifa ambayo BBC imeiona.
Ikiwa ratiba itafuatwa, basi mpaka baina ya nchi mbili hizo rasmi utakuwa eneo la amani, na Sudan Kusini itaanza tena kuchimba mafuta na kuyasafirisha kwa kupitia Sudan.
Juba iliacha kuchimba mafuta mwaka jana kwa sababu ya ugomvi wake na Khartoum kuhusu kiasi gani inafaa kuilipa Sudan kwa kusafirisha mafuta yake kwa kutumia miundo mbinu ya Sudan.
Miezi mitatu baadae majeshi ya nchi hizo yakaanza kupigana mpakani na kutia ulimwengu wasi-wasi.
Mpatanishi wa AU, Thabo Mbeki, amesema nchi zote mbili zimekubali kuheshimu makubaliano yaliyotia saini Septemba mwaka jana.
Na suluhu kuhusu Abyei ni kwamba itawekwa serikali ya pamoja kutawala eneo hilo na maeneo mengine yenye utata.
Kwa hivo kwa ufupi marais wote wawili wameafikiana kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa awali.

Chanzo: BBC swahili

No comments:

Post a Comment