Tuesday, January 15, 2013

Ipo haja jeshi la polisi kupewa somo la kudhibiti vurugu......

 Tazama picha hii, wanawajaza wanafunzi bila mpangilio, huyu dada ananing'inia bila viatu na miguu imejaa vumbi ni lazima atateleza. Je hawakulifikiria hilo?

 Ni kweli, haikuhitaji utabiri wa Sheikh Yahya kujua dada huyu lazima aanguke. alianguka hatua chache tu baada ya gari kuondoka. Nayo imekuwa bahati je angeanguka sehemu mbaya ambayo ina mawe.

Tazama hakuna hata watu wa huduma ya kwanza kuweza kumsaidia mwanafunzu huyu ambae amengakuka kutoka kwenye gari inayokwenda kasi. Amezirai na wala askari hawaonyeshi kujali. Kudhibiti vurugu i kufanya ukatili.....

Jana majira ya asubuhi mpaka jioni mitaa ya Posta ilikuwa haikaliki kwa vurugu, wanafunzi wa chuo cha usimamizi wa fedha (IFM) cha jijini Dar es Salaam, walikuwa wakiandamana kuelekea ofisi za makao makuu ya jeshi la polisi kushinikiza jeshi hilo kuwapa ulinzi katika mabweni yao yaliyo eneo la Kigamboni maana wiki iliyopita walitoa taarifa hizo lakini hawakuonekana kujaliwa.

Matokeo yake walivamiwa na vibaka wakaibiwa mali zao na wanafunzi wenzao wa kiume kudhalilishwa kwa kulawitiwa, na wanafunzi wa kike kubakwa. Hilo halikuwapendeza hata kidogo.

Ninavyofahamu mimi jeshi la polisi lina kitengo cha intelijensia, ambapo kila sehemu wana watu wao hata katika vyuo hivyo yaani vyuo vikuu. Maana yake wakati masuala hayo ya kuandamana yalipokuwa yakipangwa tayari taarifa za chinichini zilishawafikia.

Ilipasa kujipanga kwa vurugu kama hizo, na hata mkuu wa polisi kanda maalum ya Dar es Salaam Suleiman Kova alipowaamuru wanafunzi hao kuandamana nao mpaka Kigamboni kuwaonyesha kituo cha polisi kilichozembea ripoti waliyotoa, kabla hawajafika Kigamboni ilichukua takriban saa mbili mpaka tatu wanafunzi hao kuvuka kwa kutumia kivuko cha MV Magogoni.

Jeshi la polisi walikuwa na muda wa kutosha kuandaa vifaa vya kuwadhibiti na kwakuwa katika kuwadhibiti wanafunzi waliohemkwa ni lazima wapo watakaoumia, walishindwa nini kuwasiliana na kituo cha msalaba mwenkundu kuandaa watu wa kushughulika na watu watakaozimia ama kuumia vibaya? Tafakari hili kabla hujaendelea na makala haya...

Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa mazoea, hawazingatii haki za raia, raia kuandamana ama kufanya vurugu ni kilele ama kielelezo cha kutoridhishwa na baadhi ya mambo yanayoendelea katika jamii. Unaweza kusema wanafunzi walikuwa na makosa lakini waswahili husema lisilo budi hutendwa.

Wanafunzi walio katika chuo kikuu wanategemewa kutanguliza busara kwanza kabla ya kuhemkwa, lakini walishafanya hivyo kwa muda mrefu, walishatoa ripoti katika mikono salama ya askari ambao kwa namna moja ama nyingine walitakiwa kuchunguza madai hayo ingawa kwao yataonekana ni ya kipuuzi.

tafakari...

Hafidh Kido
kidojembe@gmail.com
0713 593894
15/01/2013

Picha kwa hisani ya Said Powa blog

No comments:

Post a Comment