Thursday, January 10, 2013

Jengo maarufu la Bait El Ajab Zanzibar laanguka…




                                                     Tazama jengo lilivyo zuri kwa ndani...


                                  Jengo lilivyoanguka upande wa nyuma... ilipo ngome kongwe.


             Hili jahazi liliwekwa mnamo mwaka 2003 katika ukumbi wa chini.

Ukienda Zanzibar wakati unakaribia gati ya bandari Malindi, kitu cha kwanza kukiona ni jengo zuri la kizamani liitwalo Bait Al Ajab, ama kwa Kiswahili jumba la maajabu. Kwa namna nyingine jumba hilo ndiyo sura ya mji wa Unguja.

Jengo hilo sababu ya kuitwa la maajabu ni uzuri, ukubwa na samani za gharama kubwa zilizowekwa ndani yake katika miaka ambayo Afrika bado ilikuwa nyuma kimaendeleo. Vitu viwili ambavyo viliwekwa ndani ya jumba hilo ndivyo vya kwanza kutumika katika Afrika Mashariki na kati na kusini mwa jangwa la sahara.

Umeme na lift vilianza kutumika Zanzibar mwanzoni mwa karne ya 18, wakati huo nchi za ukanda wa kusini mwa jangwa la sahara, ni sehemu ya kwanza kuwekwa ni katika jumba hilo. Kwa namna moja ama nyingine hilo linaweza kuwa jengo la kujivunia kuwa urithi kwa nchi ya Tanzania na kuhitaji kulindwa ama kuhifadhiwa kwa kiwango kikubwa.

Cha kushangaza mwezi Disemba tarehe 31 mwaka jana wakati wa sala ya magharibi upande wa nyuma wa jengo lilianguka kuanzia ghorofa ya pili mpaka sakafuni. Ukumbi mzima wa nyuma ulianguka kufuatia kuvuja kwa choo kilichokuwa ghorofa ya pili hivyo udongo kunyonya maji na kushindwa kuhimili uzito wa jengo.

Jengo hilo ambalo lipo chini ya urithi wa dunia na shirika la UNESCO linatambua uwepo wake, lilijengwa mwaka 1883 na sultani wa tatu wa Zanzibar alieitwa Sultan Baraghash Bin Said Bin Sultan kwa matumizi ya starehe na sherehe za kifalme.

Kidojembe ilipata wasaa wa kuzungumza  na Ramadhan Ali Machano ambae ni mkuu wa huduma za elimu katika jengo hilo na kuweka wazi “Jengo hili lilijengwa na sultan Baraghash, na alilitumia kwa starehe tu. Kama unavyoona jumba zima halina jiko wala chumba cha kulala, kote humo ni ‘ma-hall’ (kumbi), alikuwa akitumia kufanyia sherehe kama maulidi ama sikukuu na ngoma zao za asili.”

Wakati Afrika ikiwa inaitwa bara la giza kutokana na kuwa nyuma kimaendeleo jumba la Bait Al Ajab liliwekwa umeme mwaka 1886,  kufikia mwaka 1913 Zanzibar ikiwa chini ya Waingereza wakati huo Sultan wa kumi akiitwa Sultan Khalifa Bin Haroub akiongoza ndipo jumba hilo lilipowekwa lift. Ambapo kwa mujibu wa watu wa historia kwa nchi za Afrika mashariki na kati kusini mwa jangwa la sahara Zanzibar ndiyo ilikuwa ya kwanza kutumia lift katika majumba hilo.

Hata hivyo kutokana na husda ya waingereza mnamo tarehe 27 August, 1896 vilipiganwa vita vifupi kulivyo vyote duniani ambavyo vilidumu kwa dakika 45 maarufu vita vya Alhamis. Vilisababishwa na waingereza kulazimisha kuwekwa kwa Sultan wanaemtaka ambae waliamini atawasaidia kulinda maslahi yao.

Ni baada ya kufariki kwa Sultan wa sita wa Zanzibar alieitwa Sultan Hemed Bin Thurein Bin Said. Hivyo miongoni mwa wajukuu wakawa wanagombania kurithi kiti hicho, lakini miongoni mwa wajukuu hao mmoja alionekana ana msimamo mkali hivyo waingereza hawakumtaka. Kwa kutumia ujanja mjukuu huyo alijitangazia ufalme hata kabla babu yake kuzikwa.

Akiwa katika  jumba lililojulikana kama Bait Al Hukmu ‘kwa sasa halipo’ lilikuwa jumba la tatu kutoka jumba la Bait Al Ajaib. Ndimo mjukuu huyo alipokaa na kusema hawezi kutoka mpaka waingereza watakapomtambua kuwa yeye ndie mfalme. Waingereza wakampa siku tatu kutoka na kuondoka Zanzibar, lakini kufikia siku ya tatu waingereza wakaleta meli za kivita karibu na bandari ya Zanzibar ‘ilipo bustani ya forodhani kwa sasa’ wakaanza kupiga mizinga eneo lote la forodhani mpaka kuharibu bandari yote. Ndipo waingereza wakajenga bandari mpya eneo la Malindi, ndipo ilipo bandari ya sasa.

Jumba la Bait Al Ajab lilinusurika kuvunjwa kwasababu mbele yake kulikuwa na mnara mkubwa ambao ulibomoka kiasi kutokana na makombora yaliyokuwa yakielekezwa katika jumba hilo. Lakini ni sehemu ndogo eneo la mbele lilivunjika kutokana na makombora hayo.

Kuna uvumi ambao ulivumishwa na watu kuwa katika nguzo hizo kuna vichwa vya watumwa wa kiafrika viliwekwa ikiwa ni kafara, lakini bwana Machano alipinga kwa maelezo kuwa mkandarasi wa jengo hilo alikuwa ni Mwingereza kutoka Scotland.

Mwingereza huyo ambae hakufahamika jina lake inadaiwa alikuwa mhandisi wa meli lakini alikuwa na taaluma ya usanifu majumba. Kwakuwa Waingereza walikuwa mbele katika kupinga ukatili na kukomesha biashara ya utumwa hawangeweza kuwa wa kwanza kukata vichwa vya watumwa na kuviweka katika nguzo hizo.

Kitu cha pili kuupinga uongo huo kidojembe ilishuhudia kwa macho yake upande ambao jumba hili lilianguka nguzo nne zilikuwa chini hakukuwa na mafuvu wala mifupa ya binaadam.

Aidha kitu cha kuleta matumainiSerikali imeunda tume ya watu watano ili kufuatilia gharama zitakazotumika kukarabati jengo hilo.

Kidojembe ilipata nafasi kuzungumza na muuza bidhaa za asili kwa watalii bwana Farouq Abdallah ambae alisema ana mwezi mzima tangu jengo hilo lianguke hajauza hata kifaa kimoja.

“Tangu jengo hili lifungwe rasmi mwezi uliopita sijauza hata kifaa kimoja, wazungu hawaji tena maana kwa siku kulikuwa kunajaa wazungu utadhani kuna arusi ama msiba. Lakini kwa sasa kama unavyoona hakuna mtu hata mmoja jengo limefungwa, mtihani mtupu.”

Kidojembe ilipanga kuenda kukutana na waziri mwenye dhamana ya masuala ya utamaduni lakini haikupata nafasi kwani viongozi wote wa kiserikali walikuwa katika maandalizi ya sherehe za mapinduzi. Lakini blog yako inakuahidi kulifuatilia suala hilo ili kujua mwisho wake.

HAFIDH KIDO
0713 593894
10/1/2013
Unguja, Zanzibar

No comments:

Post a Comment