Tuesday, January 1, 2013

our population is 44,929002 Tanzanians....


                                               Rais Jakaya Mrisho Khalfan Kikwete...

RAIS Jakaya Kikwete jana alizindua matokeo ya awali ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, yanayoonyesha kuwa Tanzania sasa ina watu 44,929,002, kati yao 43,625,434 wakiwa wa Tanzania Bara na 1,303,568 Zanzibar.
Akitangaza matokeo ya Sensa katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jana, Rais Kikwete alisema takwimu hizo zinaonyesha kuwa Tanzania ina kasi kubwa ya ongezeko la watu.
“Kwa kasi hii, hadi kufikia mwaka 2016 tutakuwa jumla ya watu 51 milioni. Idadi hiyo yaweza kuonekana kuwa haina tatizo kwa nchi kama Tanzania, lakini huo ni mzigo kwa taifa, jamii na kwa uchumi,” alisema.
Alisema kuwa kwa kasi hiyo ya ongezeko la watu hapana budi kuwa na mikakati madhubuti na mipango mipya ya maendeleo kuanzia sasa.
“Kuna umuhimu wa kupanga uzazi, vinginevyo hali ya maisha itazidi kushuka na ushindani katika rasilimali hizi chache tulizonazo utazidi kuwa mkubwa,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Lazima tulipe uzito stahiki suala hili la kupanga uzazi. Lazima ujue utazaa kipindi gani na watoto wangapi ili uweze kuwahudumia.”
Alisema takwimu za matokeo hayo zina maana kwamba Serikali ianze kujipanga kwa ongezeko hilo la watu na jamii kwa upande wake, ianze kujipanga kukabiliana nalo.
“Tukizingatia haya tutaweza kupiga hatua. Sisi serikalini tutaanza kupanga mipango yetu kwa kuzingatia matokeo haya. Nanyi wenzangu anzeni kujipanga kuchukua hatua,” alisema Rais Kikwete.
Alisema matokeo mengine yatatolewa Februari ambayo ndiyo yataonyesha mchanganuo wa jinsia, umri kiwilaya, kikata na kishehia.
Rais Kikwete alisema Sensa ya mwaka 2012, ni ya tano kwa Tanzania, ya kwanza ilifanyika mwaka 1967 na kulikuwa na watu 12,313,054; Tanzania Bara watu 11,958,654 na Zanzibar 354,400.
Sensa ya mwaka 2002 ilionyesha kuwa Tanzania ina zaidi ya watu 34 milioni. Alisema tangu Sensa ya kwanza ilipofanyika hadi ya sasa, kuna ongezeko la watu zaidi ya 33 milioni.
Alisema hatua ya mwisho ya matokeo ya Sensa ya 2012 yanatarajiwa kutolewa Juni, 2013 ikiwa na mchanganuo wa taarifa zote muhimu zikiwamo za kiuchumi kwa kaya.
Rais Kikwete alisema Sensa hutoa taarifa muhimu zinazotumiwa na Serikali kupanga mipango ya maendeleo ya watu wake.
“Tulitenga siku 14 kwa ajili ya zoezi hili la Sensa, wengine hizi ndizo walifanya siku za mikutano na maandamano. Mwaka una siku nyingi, lakini sijui kwa nini walitaka wafanye mikutano na maandamano hayo katika siku hizi 14 tu?” alisema Rais Kikwete.
Aliwashukuru viongozi wa vyama vya siasa, dini na vyama vya kiraia pamoja na wamiliki wa vyombo vya habari ambao waliwahamasisha watu wao kushiriki katika sensa hiyo akiwataka kuendelea kuhamasisha matumizi ya taarifa za matokeo ya Sensa hiyo.
Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Sensa hiyo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema Serikali kutokana na kutambua umuhimu wa Sensa, imekuwa ikiongeza bajeti kwa ajili ya shughuli hizo.
Alisema katika Sensa ya mwaka huu, imetoa asilimia 90 ya gharama zote, kulinganisha na asilimia 75 katika Sensa ya mwaka 2002.
Alisema pia katika kutekeleza jukumu hilo kulikuwa na changamoto mbalimbali ikiwamo ya watendaji wanne kupoteza maisha. Hata hivyo, hakufafanua zaidi walipoteza maisha katika mazingira yapi.
Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa alisema Sensa ya mwaka 2012, itachangia kuboresha maisha kwa kutumia takwimu sahihi za wakati ili kuwezesha kutunga sera na kupanga maendeleo.
Alisema matokeo ya Sensa ya 2012 yametoka mapema kuliko miaka mingine kutokana na maendeleo ya kiteknolojia na utayari wa Serikali katika kuhakikisha kuwa yanapatikana haraka.Kamishna wa Sensa, Hajat Amina Mrisho Saidi alisema utoaji wa matokeo ya Sensa kwa mwaka huu ni jambo la kujivunia, akisema hata nchi zilizoendelea matokeo hayo huwa yanachukua muda.
Tanzania tumeweza kutoa matokeo haya ya awali ndani ya muda wa takriban miezi mitatu tu, kutokana na dhamira ya kweli ya Serikali kufanya Sensa na uzalendo wa wataalamu na wananchi,” alisema.
Alisema ofisi yake itahakikisha kuwa machapisho ya taarifa zote za Sensa, yanatolewa kwa Kiswahili na kusambazwa kwa wananchi ifikapo Juni, mwaka huu.
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mipango ya Watu, Mary Khan aliipongeza Tanzania kwa kuendesha Sensa na kutoa matokeo ndani ya muda mfupi.
Alisema matokeo ya Sensa hiyo yatawasaidia watunga sera na viongozi ikiwa ni pamoja kufanikisha mipango ya maendeleo na malengo ya kitaifa na kimataifa.
Chanzo: mwananchi.com

No comments:

Post a Comment