Tuesday, January 29, 2013

Soma msimamo wa chadema kuhusu gesi uliowekwa wazi na Mnyika leo makao makuu...

John Mnyika Mbunge wa Ubungo na waziri kivuli Nishati na madini.


Maelezo kuhusu maamuzi ya Baraza Kuu nimeyaambatanisha. Lakini pia unaweza kunukuu kutoka majibu ya nyongeza niliyoyatoa mbele ya wanahabari leo tarehe 29 Januari 2013 wakati wa mazungumzo yangu nje ya maelezo niliyoyambatanisha kutokana na habari za leo kuwa CCM kupitia kwa Kinana na Nape imesema kwamba madai ya wananchi wa Mtwara ni ya msingi.
Kinana hana uhalali wa kuwatetea wananchi kuhusu gesi kwa kuwa yenye ni mmoja watuhumiwa wa kuwakosesha wananchi wa Mtwara manufaa ya Gesi, alikuwa alikuwa ni sehemu ya uongozi wa bodi ya wakurugenzi ya kampuni ya Artumas na alishiriki kuwakosesha wananchi wa Mtwara fursa ya umeme wa MW 300 zilizopaswa kuzalishwa Mnazi Bay toka mwaka 2009. Hatua ambayo kama ingefanyika toka wakati huo mgogoro wa gesi usingekuwa kwa kiwango cha sasa. Kinana badala ya kujifanya kuwatetea wananchi wa Mtwara awaeleze alilipwa kiasi gani na kampuni hiyo na kwanini hakutetea maslahi ya wananchi toka wakati huo.
Kinana na Nape wazingatie kuwa CCM haina uhalali wa kuwatetea wananchi wa Mtwara kwa kuwa mgogoro huo ni matokeo ya sera bomu na uongozi mbovu chini ya chama hicho ambao umeruhusu ufisadi katika sekta hiyo na kukosesha wananchi  manufaa ya gesi hiyo katika miradi ya toka mwaka 2004 hali ambayo imefanya wananchi kuandamana kutaka manufaa ya sasa. Kinana na Nape badala ya kuisukumia Serikali mzigo wa kwenda kukutana na wananchi, CCM ijieleze ni kwa nini kwa miaka mingi imetoa ahadi za uongo kuhusu uendelezaji wa miradi ya gesi kwa wananchi wa Lindi na Mtwara na pia sababu za kushindwa kuisimamia Serikali kutekeleza miradi ya gesi na umeme Mtwara ikiwemo wa MW 300 wa Mnazi Bay.
Kauli za Kinana na Nape kuhusu gesi Mtwara ni za kinafiki kwa kuwa msimamo wa Serikali na CCM ulishatolewa na Rais Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM wa kuyapinga madai hayo ya wananchi. Kikwete alizungumzia  hayo kwenye hotuba yake kwa taifa tarehe 31 Disemba 2012 na kuyapinga tena katika kauli zake mwezi Januari mwaka 2013.
Mara baada ya Kikwete kuyakataa madai ya wananchi, wananchi waliendelea kuwa na msimamo na wengine wakitaka kupata msimamo wa CCM sio wa Serikali na hatimaye mwanzoni mwa mwezi Januari 2013 Makamu Mwenyekiti wa CCM Philip Mangula alisema CCM haikubaliani na madai ya wananchi na akawaita wanaCCM wachache na wananchi wengi wenye madai hayo kuwa ni ‘waasi’.
Hivyo, Kinana na Nape ambao sio wasemaji wakuu wasitoe kauli za kinafiki za kujikosha baada ya kauli za Rais  Kikwete, Mangula na viongozi wengine wa CCM na Serikali kuchochea vurugu.
Kauli za kujikosha za Kinana na Nape haziwezi kurudisha nyuma vuguvugu la wananchi kufanya mabadiliko kwa kuiondoa CCM madarakani kupitia chaguzi za mwaka 2014 na 2015 na kuiunga mkono CHADEMA katika mwaka 2013 na kuendelea kwa kuwa imekuwa mstari wa mbele kupambana na ufisadi na kutetea rasilimali za taifa pamoja  na kuwa na sera sahihi zenye kuwezesha maendeleo endelevu ya wananchi na nchi kwa ujumla.
John Mnyika (Mb)

No comments:

Post a Comment