Monday, March 11, 2013

FBI waacha mchoro wa aliemuua Padri Zanzibar...


Polisi Zanzibar imesambaza picha ya mchoro ya mtu anayedaiwa kumuua kwa kumpiga risasi, Padri Evaristus Mushi wa Kanisa Katoliki mwezi uliopita.
Mchoro huo uliosambazwa kwa vyombo vya habari jana na Ofisi ya Kamishna wa Polisi Zanzibar, unamwonyesha mtu aliyevaa kofia ya baraghashia.

Katika taarifa hiyo, Polisi ilisema kwamba mtu atakayesaidia kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo atazawadiwa Sh10 milioni... “Mwananchi yeyote ambaye anamjua mtu aliyefanana na mchoro huo atoe taarifa katika kituo chochote cha polisi na iwapo atakuwa ndiye mhusika atapewa zawadi hiyo.”

Kamishna wa Polisi Zanzibar Mussa Ali Mussa hakupatikana jana kutoa maelezo zaidi juu ya hatua hiyo, lakini Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Haji Abdallah Hanna alithibitisha kuwa taarifa hiyo imetoka Polisi.

Hata hivyo, Kamanda Hanna hakuwa tayari kutoa ufafanuzi zaidi kwa maelezo kwamba upelelezi wa suala hilo unafanywa na Makao Makuu ya Polisi Zanzibar.

Kuuawa kwa Padri Mushi lilikuwa tukio la tatu kubwa la kushambuliwa kwa viongozi wa dini baada ya kumwagiwa tindikali kwa Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Fadhil Soraga na kupigwa risasi Padri Ambrose Mkenda wa Kanisa Katoliki.

Kitendo cha kutoa picha hiyo ni hatua kubwa katika upelelezi wa kifo cha Padri Mushi, ambacho kilitikisa visiwani Zanzibar.
Pia hatua hiyo imekuja siku chache baada ya kutua kwa maofisa wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI), ambao wanasaidiana na Polisi wa Tanzania kuchunguza tukio hilo.

FBI wana kawaida ya kutumia picha na michoro pale wanapochunguza matukio makubwa ya uhalifu au ugaidi.

Mathalan, pale wanapotaka kupeleleza kwa kutumia michoro ya sura za wahalifu wasiowafahamu, hufanya mahojiano na watu waliokuwapo kwenye tukio na wakati wakipata maelezo hayo, huwa na wataalamu wao wa uchoraji karibu ili kujaribu kutengeneza sura za watu wanaotafutwa.

FBI walikuja nchini baada ya kualikwa na Serikali ya Tanzania ambayo inataka kujua chanzo cha vitendo vinavyotishia maisha ya viongozi wa dini huko Zanzibar.

Hii ni mara ya pili kwa FBI kufanya kazi Tanzania baada ya mwaka 1998 walipokuja kuchunguza kulipuliwa kwa bomu kwa ubalozi wa Marekani.
Chanzo: Gazeti Mwananchi

No comments:

Post a Comment