Monday, March 11, 2013

FIFA Yawasilisha Kusudio La Kuifungia Tanzania



Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA) limesema litaifungia Tanzania iwapo itabainika kuwa Serikali imekuwa ikiingilia shughuli za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

FIFA imesema kumekuwa na shutuma kupitia taarifa mbalimbali za vyombo vya habari nchini kuwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imeonesha nia ya kuingilia uendeshaji wa TFF.

Kwa mujibu wa barua ya jana (Machi 10 mwaka huu) ya FIFA kwenda kwa Rais wa TFF, Leodegar Tenga, vyombo vya habari vimemkariri Waziri (Dk. Fenella Mukangara) kuwa Serikali imeiagiza TFF kutumia Katiba ya mwaka 2006 katika uchaguzi wakati tayari imeshafanyiwa marekebisho.

“Pia imeelezwa kuwa TFF imetakiwa kufanya Mkutano Mkuu pamoja na ule wa uchaguzi kwa tarehe ambazo zimepangwa na Serikali. Vilevile imeelezwa kuwa Serikali inakusudia kuunda Kamati ya Muda iwapo TFF haitatekeleza maagizo yake,” imesema sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome Valke.

FIFA imesema iwapo yaliyoripotiwa na vyombo vya habari yatathibitika kuwa kweli, maana yake huo ni uingiliaji wa wazi wa Serikali kwa shughuli za TFF.
“Tunapenda kuwakumbusha kuwa wanachama wote wa FIFA wanatakiwa kuendesha shughuli zao kwa uhuru bila kuingiliwa na mtu mwingine kama ilivyoelezwa katika ibara za 13 na 17 za Katiba ya FIFA.

“Hivyo kama maagizo hayo yanayodaiwa kutolewa na Serikali yatatekelezwa, suala hili litapelekwa katika mamlaka za juu za FIFA kwa hatua zaidi ikiwemo kuisimamisha Tanzania kama ambavyo inakuwa pale panapokuwa na uingiliaji wa Serikali,” imesema barua hiyo.

Barua hiyo ambayo nakala yake pia imetumwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) imeelezea baadhi ya athari ambazo Tanzania itakumbana nazo endapo itasimamishwa ni timu za taifa pamoja na klabu kutoshiriki mechi za kimataifa kwa mujibu wa Ibara ya 14 ya Katiba ya FIFA.

Vilevile si TFF au wanachama wake na maofisa wengine watakaoweza kunufaika na programu za maendeleo, kozi au mafunzo yanayotolewa na FIFA na CAF.

“Madai ya uamuzi uliofanywa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ni ya kusikitisha kutokana na ukweli kuwa FIFA ilishatangaza itatuma ujumbe wake kuchunguza jinsi hali ilivyo kwa sasa na kutoa mapendekezo yake. Kutokana na hali hii, ujumbe wa FIFA uliokuwa uje kuchunguza (suala la uchaguzi) itabidi usubiri kwa vile ni muhimu kushughulikia tatizo hili kwanza.

“Katika mazingira haya tunaomba ueleze msimamo huu wa FIFA kwa mamlaka zinazohusika (Serikali) na athari ambazo mpira wa miguu wa Tanzania utakumbana nazo. Tunakushukuru na tunatarajia utatufahamisha kila hatua inayoendelea katika suala hili,” imesema barua hiyo.


Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
 11 March, 2013

No comments:

Post a Comment