Monday, March 11, 2013

Katibu mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana kufanya ziara ya siku kumi nchini China....


Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana (Kulia) akizungumza na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa dawati la maswala ya Afrika katika Idara ya Uhusiano wa Kimataifa  ya Chama Cha Kikomunisti cha China (CPC), Wang Heming (kushoto) baada ya kuwasili leo Machi 11, 2013 kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Guangzhu, kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku kumi nchini China. Katikati ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Zanzibar) Vuai Ali Vuai. 
(Picha na Bashir Nkoromo).

NA BASHIR NKOROMO, CHINA
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana amewasili leo Machi 11, 2013 nchini China kuanza ziara ya kikazi ya siku kumi, kwa mwaliko wa Chama Cha Kikomunisti cha China.
Kinana ambaye ni ziara yake ya kwanza kufanya nchi za nje tangu ateuliwe kuwa Katibu Mkuu wa C CCM, Oktoba mwaka jana, amewasili akiambatana na ujumbe wa watu 14 wakiwemo viongozi na maofisa wa Chama na kupokewa  kwenye Uwanja wa Ndege wa Guangzhu, na  Naibu Mkurugenzi Mkuu wa dawati la maswala ya Afrika katika Idara ya Uhusiano wa Kimataifa  ya Chama Cha Kikomunisti cha China (CPC), Wang Heming.

Katibu Mkuu ambaye aliwasili saa 8 mchana kwa saa za China (sawa na saa nne asubuhi) za Tanzania, ameambataba na Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Zanzibar) Vuai Ali Vuai, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Khadija Aboud, Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Dk. Asha-Rose Migiro, Katibu wa Jumuia ya Wazazi ya CCM, Khamis Suleiman Dadi, Katibu wa UWT Amina Makilangi, Katibu Mkuu wa UVCCM, Martine Shigela na Wenyeviti wa CCM wa mikoa, Jesca Msambalavangu (Iringa), Maganga Sengerema na Titus Kamani (Simiyu) na maofisa wa Chama.
Akizungumza kwenye Uwanja wa Ndege wa Guangzhu, Wang alisema, Chama Cha Kikomunisti cha China kimefarijika na kuona fahari kubwa kwa kuupokea ugeni wa Kinana, kwa sababu Katibu huyo wa CCM pamoja na kuwa ziara yake ya kwanza tangu kuteuliwa kwake kuwa Katibu Mkuu wa CCM, pia ni kiongozi wa kwanza kutembelea China tangu kupatikana kwa uongozi mpya wa China wa Rais  Xi Jimping ambaye pia ndiye Katibu Mkuu wa CPC.
Alisema, China bado inaona umuhimu mkubwa wa kushirikiana na Tanzania katika masuala mbalimbali hasa yanayohusu kuinua uchumi kwa ajili ya kuboresha maisha ya wananchi wa pande mbili za Tanzania na nchi yake.
Wang alisema, kutokana na umuhimu wa ziara hiyo, uongozi wa juu wa CPC umeandaa ratiba itakayomwezesha Kinana na ujumbe wake kushuhudia mambo mbalimbali ya kimaendeleo katika nyanja mbalimbali za Uchumi na namna China chini ya uongozi wa CPC ilivyofanya jitihada hadi kupiga mapinduzi makubwa ya kiuchumi duniani.
Kwa Upande wake Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alishukuru kwa mapokezi makubwa waliyotoa viongozi wa CPC, na kusema  kueleza matumaini yake kwamba CCM itakuwa na mengi ya kujifunza na viongozi hao kuondoka nayo kwa ajili ya kwenda kuboresha na kuinua zaidi maendeleo ya Tanzania kiuchumi.
“Tunatambua ninyi (China) mmekuwa washirika wetu wazuri na Tanzania tangu miaka mingi, kwa mfano mmehusika sana katika ujenzi wa Reli ya TAZARA ambayo inatoa mchango mkubwa katika uchumi wa taifa, na pia mmeshiriki kuanzisha viwanda nchini kwentu kikiwemo kiwanda cha Urafiki pale Ubungo na bado mnaendelea kuwa washirikia wazuri hadi sasa, kwa kweli tunafurahia sana ushirikiano huu”, alisema Kinana.


No comments:

Post a Comment