Monday, March 4, 2013

Malawi watilia shaka Tanzania itavunja makubaliano juu ya mgogoro wa ziwa Nyasa.


SERIKALI ya Malawi imesema ina wasiwasi kuhusu hatma ya mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa na kwamba hali hiyo inatokana na Tanzania kuvunja sehemu ya makubaliano ya usuluhishi.
Kauli hiyo inakuja wakati jopo lo viongozi wastaafu kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika(Sadc), likijiandaa kuwasilisha ripoti yake baadaye mwezi huu.
Jopo hilo linaloongozwa na Rais Mstaafu wa Msumbiji, Joachim Chissano, litakabidhi ripoti hiyo kwa viongozi wakuu wa nchi zote mbili.
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Malawi, Ephraim Chiume, ameituhumu Tanzania kwamba imeanza kuzungumzia utatuzi wa mgogoro huo wakati ikijua kuwa mzozo huo uko katika hatua ya upatanishi maalumu.
Waziri Chiume aliikosoa kauli iliyotolewa hivi karibuni na Waziri wa Mambo ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, kuwa ufumbuzi wa mgogoro wa mpaka baina ya mataifa hayo mawili, unakaribia kupatikana.
Alisema  kitendo cha  Membe kuzungumzia maendeleo ya mgogoro huo kinapingana na makubaliano ya pamoja yaliyowasilishwa kwa  Chissano na kwamba hatua hiyo inavunja moyo.
Waziri Chiume aliliambia gazeti la Nyasa Times kuwa pande zote mbili zilipokutana Nombemba 17 mwaka jana jijini Dar es Salaam, zilikubaliana kuzungumzia mgogoro huo ili kuepuka kuingilia juhudi za upatanishi.
Alisema hata hivyo, hivi karibuni ya Serikali ya Tanzania imekiuka sehemu ya makubaliano hayo.
 “Tanzania wamevunja makubaliano, na sisi tunasisitiza kuwa Ziwa Nyasa ni la Malawi,” alisema waziri.
Baadhi ya wachambuzi wa mambo, wamesema kauli huyo inaashiria kuwa huenda pande hizo mbili zikashindwa kukubaliana na mapandekezo yatakayowasilishwa na mpatanishi wa mzozo huo.
Mpatanishi huyo mwezi huu anatazamiwa kukutana na Rais Jakaya Kikwete na yule wa Malawi, Joyce Banda.
Hata hivyo, alivyotafutwa ili kuzungumzia malalamiko hayo, waziri Membe  kupatikana, lakini Naibu wake Mahadhi Maalimu, alisema: “Ninachosema mimi kwanza hizo taarifa sijazipata na kama zipo basi Serikali itawasiliana kupitia mikondo sahihi. Serikali haiwezi kujibizana kupitia magazeti”
Hivi karibuni Serikali ya Tanzania na Malawi zilipeleka barua ya pamoja kwenye Jukwaa la Marais wa Wastaafu wa Nchi za Kusini mwa Afrika linaloongozwa Chissano, zikiomba zipatanishwe katika mzozo huo.
Hatua hiyo ilikuja  baada ya majadiliano ya pande zote mbili kushindwa kuzaa matunda.
Kama sehemu ya kuepusha mgongano wa kimaslahi, jopo hilo la wasuluhishi halikuwahusisha viongozi wastaafu wa Tanzania Alhaji  Ali Hassani Mwinyi na  Benjamin Mkapa.
Hali kadhalika Bakiri Muluzi wa Malawi.
Hata hivyo, duru za kidiplomasia mjini Lilongwe zinasema  Serikali ya Malawi imejiandaa kwenda katika  Mahakama ya Haki ya Kimataifa(ICJ) kama upatanishi huo utashindwa kuzaa matunda.
Gazeti la Daily Times limewanukuu maofisa wa Serikali wakisema kuwa karata ya mwisho kwa Malawi itakuwa ni kwenda katika mahakama hiyo.

No comments:

Post a Comment