Monday, March 18, 2013

Papa Francis I amtembelea Papa aliestaafu...



Vatican City. Papa Francis ameadhimisha misa yake ya kwanza tangu alipochaguliwa kuwa kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki duniani, huku akitoa hotuba ya dakika tano mbele ya waumini wa Parokia ya Mtakatifu Anna.
Jana, katika mahubiri yake mafupi, Papa Francis alishangaza wengi kwa kueleza kuwa binadamu hawana budi kusameheana, kama ambavyo Mungu amekuwa mwenye huruma kwa wanadamu.
Awali, Papa alijitokeza hadharani katika lango kuu la kuingilia kanisa hilo la parokia akiwa amevaa kanzu nyeupe, viatu vyeusi, kuwapungia mkono watu wote, kisha kupeana nao mikono.
Kisha, alibusu, kuwashika mabegani watoto na kueleza kuwa jukumu la binadamu ni kupendana.
“Ningependa sisi sote tuwe na ujasiri wa kutembea katika uwepo wa Mungu,” alisema Papa Francis kwa Kilatini.
Mapema, Papa alifanya maombi binafsi katika Kanisa Kuu la Santa Maria Maggiore na baadaye alikutana na watoto na wasafiri waliokwenda kumsalimia.
Papa, pia ameanza kazi ya uteuzi wa maofisa wa juu wa Vatican, ingawa orodha hiyo haijakamilika wala kuwekwa wazi.
Jumatano usiku muda mfupi baada ya kuchaguliwa kwake, aliusalimia umati wa watu waliofurika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro akitoa wito wa unyenyekevu na kuwaomba waumini wamwombee baraka kabla yeye hajawabariki.
Alhamisi, Papa Francis alirudi kwenye makazi ya watumishi yaliyopo mjini Rome alipokuwa akiishi mbele ya jengo la mikutano ulimofanyika uchaguzi uliomweka madarakani.
“Alifungasha mizigo yake na kwenda kulipia chumba alichofikia ili kuwa mfano bora.
“Pia, alivunja utamaduni wa kwenda kuwasubiri makardinali waliokwenda kumpa pongezi, badala ya kukaa kwenye kiti cha enzi,” alisema msemaji wa Vatican, Padri Federico Lombardi.
Ijumaa alikutana na makardinali 106 wakiwamo wale ambao hawakuingia kwenye mkutano wa uchaguzi.
Jumamosi, Papa alikutana na mamia ya waandishi wa habari wa kimataifa na kuweka msimamo wa kanisa lake.
Siku ya Ijumaa, anatarajiwa kumtembelea mtangulizi wake , Papa Benedict XVI, eneo la Castel Gandolfo, nje kidogo ya Mji wa Rome.
Kumtembelea mtangulizi wake kunaelezwa kuwa ni muhimu kwa kuwa kuwepo kwake kunaweza kuleta upinzani katika madaraka yake.
Papa Francis anatarajia kusimikwa rasmi Jumanne katika misa ya uzinduzi ambayo itahusisha maelfu ya waumini.
Ingawa alitajwa kushika nafasi ya pili katika uchaguzi wa mwaka 2005 uliomweka madarakani Papa Benedict XVI, baadhi ya watu walitabiri kuwa papa atakayefuatia atatoka nje ya Ulaya.
Akiwa mzaliwa wa Amerika ya Kusini, anaonekana kuwa mtu aliyeshika mno mafundisho na mwenye misimamo.
Hali hiyo inamfanya kuonekana kama mtu wa mabadiliko katika utendaji wa Vatican akisaidiwa na makardinali waliomzunguka.
Hata hivyo, wachunguzi wa mambo wanasema Papa Francis anakabiliwa na changamoto nyingi katika uongozi wake hasa kwa kuwa kanisa hilo linakabiliwa na kashfa za unajisi zilizowakumba makasisi wake na tuhuma za rushwa.
Changamoto nyingine inayomkabili ni pamoja na suala la wanawake kupewa upadri, kuibuka kwa madhehebu na kupukutika kwa waumini kunakoendelea katika sehemu mbalimbali duniani, ikiwamo Ulaya na Marekani.
Papa Francis au Kardinali Jorge Mario Bergoglio, alizaliwa Desemba 17, 1936 mjini Buenos Aires, Argentina. Ni mfuasi wa Shirika la Wajesuiti tangu mwaka 1969 na alisomea Argentina na Ujerumani. Alipewa ukardinali mwaka 1998.
*Elias Msuya kwa msaada wa mashirika ya habari ya kimataifa.     
Chanzo: Mwananchi.

No comments:

Post a Comment