Wednesday, March 27, 2013

UJUMBE WA FIFA KUSIKILIZA WAGOMBEA TFF APRILI 16




SHIRIKISHO la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ambalo lilisimamisha mchakato wa uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutokana na baadhi ya wagombea kulalamika kuenguliwa sasa litatuma ujumbe wake nchini katikati ya mwezi ujao.

Ujumbe huo ambao moja ya shughuli zake kuwasikiliza wote walioenguliwa na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF na hawakuridhika na uamuzi huo, utakuwepo nchini Aprili 16 na 17 mwaka huu.

Kwa mujibu wa barua ya Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome Valcke kwenda kwa Rais wa TFF, Leodegar Tenga, kazi ya ujumbe huo ni kubaini tatizo lililopo na kutoa ripoti kwa mamlaka zinazohusika ndani ya FIFA kwa ajili ya kutoa mwongozo.

Ujumbe huo utakutana na pande mbalimbali zinazohusika wakiwemo wagombea, kamati za uchaguzi za TFF. Lakini pia ujumbe huo unatarajia kumtembelea Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara pamoja na watendaji wake wizarani.

Uchaguzi wa viongozi wa TFF ulikuwa ufanyike Februari 24 mwaka huu, lakini ukasimamishwa na FIFA baada ya baadhi ya wagombea walioenguliwa kulalamika kuwa hawakutendewa haki na wangependa shirikisho hilo liingilie kati.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment