Tuesday, March 26, 2013

Vyama vya ndondi vyamcheka Cheka




Na Hafidh Kido

VYAMA vinavyosimamia ndondi za kulipwa nchini, katika hali isiyokuwa ya kawaida, vinamcheka bondia Francis Cheka badala ya kumsikitikia kwa hujuma anazodai alifanyiwa nchini Ujerumani hivi karibuni.

Wakizungumza na kidojembe kwa nyakati tofauti, viongozi wa vyama vya PST na TPBO wameeleza ya kuwa hawashangai kusikia Cheka alihujumiwa na Promota wa Kenya, Thomas Mutua aliyekwenda naye Ujerumani  kucheza pambano la kusaka ubingwa wa Shirikisho la Ndondi la Kimataifa (IBF).

Katika pambano hilo Cheka anadai ya kuwa Promota huyo aliyekuwa kwenye kona yake kama kocha , alitupa taulo ulingoni kuashiria mwamuzi asimamishe pambano kumwokoa ilhali alikuwa yuko ‘fiti’kuendelea kupambana na Mjerumani, Uensal Arik aliyekuwa akichuana naye. Hiyo ilikuwa kwenye raundi ya saba.

“Hii si mara ya kwanza kupata malalamiko yanayomuhusu huyu ‘promota’ Thomas Mutua kutoka Kenya kuwahujumu mabondia wa Tanzania. Tulishakubaliana tusimpe kibali cha kuondoka na mabondia wetu, mimi nashangaa sana amepata wapi kibali cha kuondoka na Cheka,” alisema Emmannuel Mlundwa, muasisi wa ndondi hizo nchini anayekiongoza chama cha PST.

kidojembe ilipowasiliana na Yassin Abdallah ‘Ustadh’ Rais wa chama kingine cha ndondi za kulipwa cha TPBO naye aliungana na Mlundwa kwa kuondoka  na mtu ambaye hana baraka zozote nchini.

“Muulize Cheka aliondoka kwa kibali cha nani. Kama aliondoka kienyeji hatuhusiki. Cheka ameondoka bila kufuata kanuni za ngumi hivyo hana msaada. Katiba ya Tanzania inaruhusu mtu kusafiri popote anapotaka kama amefuata katiba ya nchi ni sawa alikuwa na haki kuenda Ujerumani lakini kwa mujibu wa kanuni za ngumi amefeli, na hili litakuwa funzo kwa mabondia wote wanaofuata mapromota kutoka Kenya,” alisema Yassin.

Cheka mwenyewe, Francis Cheka ‘SMG’ ambaye ni bingwa wa IBF Afrika uzani wa Super Middle, alikiri kutopewa ushirikiano na chama chochote cha ngumi za kulipwa Tanzania kwa ajili ya safari yake ya Ujerumani ingawa alidai kutoa taarifa kwa Rais wa kamisheni ya ngumi za kulipwa Tanzania (TPBC), Onesmo Ngowi.

“Nilizungumza na Ngowi kuhusiana na hujuma nilizofanyiwa lakini naye aliniambia hili litakuwa funzo kwangu, simuelewi kwa kweli,” alisema.

Kuhusu ni nini hasa kilichotokea, Cheka anasema kwamba aliombwa kupokea rushwa ili apoteze pambano hilo lakini akakataa.  “Ndugu yangu nilifuatwa hotelini mara tano wakitaka niuze pambano kwa Euro 6,000 nikakataa,” alisema Cheka.

“Nadhani baada ya kuona nimekuwa mbishi, walimfuata Mutua pamoja na mwamuzi, maana taulo lilirushwa na Mutua kutoka kona yangu, nilikuwa fiti na yule jamaa alishaanguka mara moja. Nashangaa kwanini mwamuzi alikubali kumaliza pambano,” aliongeza.

Cheka alisema ya kuwa mpaka sasa hajalipwa pesa zake zote. “Mkataba unasema nilipwe (Euro 11,000), lakini mpaka sasa nimelipwa Euro 4,500.

Kuhusu vyama vya ndondi za kulipwa nchini, Cheka  aliviponda. “Mimi naona kama vya kinafiki tu hasa chama cha ‘Ustadh’ (TPBO),” alisema bila kufafanua ni kwa nini hicho ndicho anachokiponda zaidi.

kidojembe ilipowasiliana na Mutua kwa njia ya simu kutoka Nairobi  alisema aliamua kutupa taulo ulingoni kumuokoa Cheka baada ya kumuona amepatwa na tatizo.

“Niliamua kurusha taulo kwa sababu niliona bondia wangu ameumia mkono wa kulia hivyo sioni kama kuna tatizo lolote kufanya hivyo kwani ni kitu cha kawaida sana kumsaidia bondia anapozidiwa,” alisema Mutua anayedai pia kwamba alipata kibali cha kumchukua nchini kutoka kwa Ngowi.

Kuhusu Cheka kufuatwa mara tano kutakiwa auze pambano, Mutua alisema hajaambiwa kitu kama hicho na bondia wake kwani ikiwa alifuatwa basi mtu wa kwanza kujua ilipasa kuwa ni yeye lakini hajui chochote na kuongeza kuwa mabondia wengi wa Tanzania wanapenda kupotosha umma wanaposhindwa.

“Kitu ambacho hatujamalizana na Cheka ni pesa zake mkataba unasema anatakiwa kulipwa Euro 11,000 lakini mpaka sasa amelipwa Euro 5,500 na sababu kubwa ni matatizo ambayo yalitokea bana yetu na promota Eva Arole ambaye aliandaa pambano lile lakini mpaka sasa tunajitahidi kuwasiliana naye kuhakikisha pesa hizo zinatumwa,” alisema Mutua.

kidojembe ilijaribu kuwasiliana na Onesmo Ngowi, ili kupata ukweli kuhusu yeye kutoa kibali kwa Mutua kumchukua Cheka  lakini simu yake ilikuwa ikiita bila kupokewa.

Mwandishi alituma ujumbe kwenye simu uliomtaka kutoa ufafanuzi juu ya chama chake kuhusika kutoa ama  kutotoa kibali kwa Cheka lakini hakujibu ujumbe huo ingawa ulionyesha kumfikia.

 kidojembe@gmail.com
Dar es Salaam, Tanzania
26 March, 2013

No comments:

Post a Comment