Monday, March 11, 2013

Willy Mutunga jaji mkuu wa Kenya afungua njia kwa Odinga na chama chake cha CORD kuenda mahakamani.



Jaji mkuu wa Kenya Willy Mutunga amesema kuwa mahakama ya juu zaidi itasikiliza na kuamua bila mapendelo kesi iliyowasilishwa katika mahakama ya juu zaidi kuhusu utata wa kura za urais.
Kesi hii imewasilishwa na muungano wa Raila odinga wa CORD wakipinga ushindi wa Uhuru Kenyatta.
Bwana Mutunga aliyepokea stakabadhi zenye matokeo ya uchaguzi mkuu wa urais kutoka kwa tume ya uchaguzi Kenya, pia alisema majaji wa mahakama hiyo ndio watasikiliza kesi hiyo.
Alisema kuwa uchaguzi ulikuwa wenye amani na pia aliwashukuru wakenya kwa kuwa na imani na idara ya mahakama.
Jaji Mutunga alivitaka vyombo vya habari kupeperusha moja kwa moja kesi hiyo wakati itakapokuwa ikisikilizwa ka sababu ya kuhakikisha uwazi.
Mgombea wa urais aliyeshindwa, Raila Odinga , Jumapili aliunda kikosi cha mawakili watakaowasilisha kesi dhidi ya ushindi wa Uhuru Kenyatta kama rais wa nne wa Jamuhuri ya Kenya, kama alivyotangazwa na tume ya uchaguzi na mipaka Kenya.
Odinga anataka mahakama iamuru kuhesabiwa tena kwa kura na kuchunguza visa vya kupungua maradufu kwa kura za urais kutoka maeneo bunge fulani baada ya sajili la wapiga kura kufungwa.
Pia wanahoji uwezekano wa wapiga kura milioni moja kumpigia kura rais peke yake bila kumchangua mtu mwingine akisema kuwa huenda wakawasilisha kesi hiyo Jumatano.
Kenyatta alimshinda Odinga kwa kura laki nane na kupata zaidi ya asilimia hamsini na moja ya kura zilizopigwa.
Chanzo: BBC Swahili.

No comments:

Post a Comment