Wednesday, April 3, 2013

Ajinyonga baada ya Mahakama kukubali matokeo ya Uhuru kuwa Rais kenya.


Nairobi. Raia mmoja nchini Kenya amejinyonga baada ya Mahakama ya Juu kuidhinisha ushindi wa  Uhuru Kenyatta kuwa Rais wa Kenya.
Mkuu wa polisi wa eneo hilo Richard Bitonga alisema mwanamume huyo alijitia kitanzi nje ya nyumba yake katika kituo cha kibiashara cha Lwanda, eneo bunge la Nyatike.
“Alianza kwa kuvaa nguo ya chama cha ODM iliyokuwa na picha ya Waziri Mkuu kabla ya kujitia kitanzi,” Alisema  Bitonga. Ingawa hakuacha ujumbe wowote, alikuwa amewaeleza marafiki wake kwamba alikasirishwa na uamuzi wa mahakama.
Baadhi ya wakazi walisema marehemu alikuwa ametisha kujitoa uhai ikiwa Odinga hangeshinda kesi ya kupinga uchaguzi wa urais. “Alisema hakuona sababu ya kuendelea kuishi katika ulimwengu huu ikiwa Odinga hatakuwa Rais wa nchi hii,” alisema mkazi  Samuel Otieno, ambaye ni mchimba dhahabu.
Mbunge wa eneo hilo,  Eric Anyanga  alisema “Uamuzi wa mahakama ulishtua wafuasi wengi wa Cord kote nchini waliotarajia awamu ya pili ya uchaguzi wa urais baada ya dosari tele kugunduliwa katika uchaguzi wa Machi 4,” alisema Mbunge huyo
Wakati huohuo, Waziri Mkuu Raila Odinga na Makamu wa Rais Kalonzo Musyoka wanapanga kukutana na maseneta na Wabunge wa Muungano wa CORD wiki ijayo kujadili hatima yao ya kisiasa baada ya uchaguzi mkuu kukamilika.
Odinga na  Musyoka walikutana na baadhi ya wabunge na maseneta wa Cord katika ofisi ya waziri mkuu katika barabara ya Harambee Avenue, Nairobi.
Chanzo: Mwananchi.

No comments:

Post a Comment