Wednesday, April 24, 2013

Bara la Afrika limefukarishwa na usaliti wa viongozi wake

Na Goodluck Eliona, MWANANCHI



Suala la Afrika kujitawala na kujitegemea katika nyanja zote limekuwa mjadala wa muda mrefu kutoka kwa Waafrika wenyewe.
Kwa muda mrefu Bara la Afrika limeonekana kuwa nyuma katika maendeleo ya uchumi, jamii na siasa.
Baadhi ya wapelelezi wa wakoloni katika karne ya 18 walilitaja bara hilo kama la giza kutokana na hali ya kudorora kimaendeleo kulinganisha Ulaya walikotoka.
Licha ya kuja kutawala kwa takriban karne moja, wakoloni kutoka Ulaya wameendelea kuzitawala nchi za Afrika kwa ukoloni mambo leo.
Suala la Afrika kujitawala na kujitegemea katika nyanja zote limekuwa mjadala wa muda mrefu kutoka kwa Waafrika wenyewe.
Mjadala huo umeibuka pia katika tamasha la tano la Kigoda cha Mwalimu Nyerere, ililofanyika hivi karibuni katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam likiwa limebeba ujumbe wa “Maendeleo ni mapambano ya Ukombozi,” suala la Afrika kujitawala limetawala.
Akitathmini falsafa ya maendeleo ya Mwalimu Julius Nyerere, Profesa Manuh Takyiwaa kutoka chuo Kikuu cha Ghana, Legon anasema pamoja na Afrika kuwa na maliasili nyingi, bado wapo viongozi ambao wanazigombania kwa lengo la kujinufaisha wao binafsi huku wakiwaacha wananchi mikono mitupu.
Anahoji falsala ya kujitegemea na kama rasilimali yaani watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora zinatumika ipasavyo.
“Waafrika bado wanagombania maliasili zao, nyingine zikichukuliwa na kusafirishwa nje kwenda kuyanufaisha mataifa ya mbali. Hata kitendo cha kuikumbatia China kinaonyesha kuwa hatuja jifunza chochote,” anasema Takyiwaa.
Naye Profesa Penina Mlama kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anatoa mfano wa utegemezi wa Watanzania kiasi cha kuwataka hata wahisani wachangie ujenzi wa vyoo vya shule.
“Shule nyingi vijijini hazina vyoo… Nimekutana wa wakuu wa shule wanaosema tunasubiri wahisani watusaidie. Nini kinachotufanya tuwasifu na kuwatetemekea baadhi ya viongozi ambao tunajua kabisa wanalimaliza taifa letu?”
Profesa Mlama kwa upande mwingine anasema hali imekuwa mbaya zaidi hata kwa baadhi ya wasomi, ambao wamekuwa wakifundisha njia sahihi ya kufuatwa huku wakiwanyooshea vidole wengine, lakini hivi sasa wameanza kwenda kando na kuanza kuyatenda yale waliyokuwa wakiyapinga.
“Tunapozungumzia mustakabali ukombozi wa kimaendekeo ni lazima tupate suluhisho la hii nguvu inayoleta haya yote. Watu wapo, lakini ni wa aina gani?”
Kwa upande wake Profesa Monica Lima e Souza kutoka Chuo Kikuu cha Federal cha Rio Dejaneiro, anatoa uzoefu wa Brazil ambayo imepiga hatua katika kujikomboa kwa kuanzisha mtalaa wa masomo katika vyuo vikuu unaolenga kujikomboa kimaendeleo kupitia fikra za Kiafrika.
“Tusiwe na mwelekeo mmoja katika kufikia malengo yetu. Tunazungumzia bara nzima, turuhusu mawazo tofauti kutoka kila kona ili tuwe na nguvu ya kufika kule twendako,” anasema Souza.
Brazil ambayo nusu ya watu wake wana asili ya Afrika, pamoja na kuwa katika orodha ya nchi zinazoibuikia katika uchumi, bado inakabiliwa na matatizo lukuki.
“Wanasema Brazil ipo katika kundi la nchi zinazokuwa kiuchumi. Sawa, lakini watu wengi wana hali mbaya kiuchumi,” anasema Souza.
Naye Profesa Thandika Mkandawire kutoka Shule ya Uchumi ya Uingereza, aliyekuwa mgeni rasmi wa tamasha hilo anasema baadhi ya viongozi wanadhoofisha kwa makusudi jitihada za kuiletea maendeleo Afrika.
Anaongeza kuwa japo wazo la kuiunganisha Afrika lilikuwa na nia ya kulipa nguvu ya kiuchumi bara hilo, lakini kinachofanyika hivi sasa ni kinyume na dhana nzima ya waasisi wake.
“Katika mashirikisho mbalimbali ya nchi hivi sasa, ajenda zao ni tofauti kabisa na zile za kulikomboa bara la Afrika,” anasema Mkandawire.
Anaongeza kuwa Bara la Afrika linauwezo, nguvu na maarifa ya kujitawala lenyewe na siyo watu kutoka nje kuja kuchuma maliasili na kuondoka na utajiri mkubwa huku watu wake wakigeuka vibaraka wanaowanaoshuhudia tu kinachoendelea.
“Hatuhitaji watu wapya kutoka nje, bali tunahitaji watu wapya kutoka hapa hapa,” anasema Mkandawire.
Licha ya kuhimiza mapambano ya Afrika kwa vijana, Mkandawire ameonyesha wasiwasi kwa vijana wa sasa.
“Ni kweli kuwa vijana wanahitajika sana, lakini je, wapo hao wenye uwezo?” anahoji Mkandawire.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Rwekaza Mukandara  anamtaja Rais wa Misri, Mohamed Morsi kuwa ni mfano wa viongozi wa Afrika wasio na maono na bara hilo.
Anasema wakati Morsi anaapishwa alitoa hotuba yake ya dakika 15, lakini hakutaja jambo lolote kuhusu bara la Afrika.
Kwa upande wake Profesa Mshumbusi Kiboyonga wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasisitiza kuwa Afrika siyo bara maskini bali wakoloni ndiyo cha umaskini huo.
“Afrika siyo maskini. Matatizo yetu yamefanywa mtaji na mataifa mengine. Kama wana nia ya dhati, kwanini wameleta mpango wa kupunguza umaskini na si kuondoa umasiki” anahoji.
Akizungumzia elimu inayotolewa Afrika na mfumo mzima wa mitaala anasema nacho ni chanzo kingine cha Waafrika kushindwa kujikomboa kiuchumi kwani imejaa kifra za kigeni.
“Hatuna chuo chochote Afrika kinachofundisha Uafrika, kufikiri na kuendelea Kiafrika.
 Tanzania ni nchi tajiri kuliko nchi yoyote Ulaya. Utajiri wa Afrika ni watu na mali zao.Tukiwaweka pamoja, bara hili tutafika tunakotaka kwenda,” anasema Kiboyonga.
Naye Diana Kamara wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere licha ya kutambua kuwa ukombozi wa  maendeleo ni mapambano yanayoanza ndani ya mtu, baadhi ya viongozi wa Afrika walijaribu kuvaa ngozi ya kondoo ili kutaka kuihadaa jamii wanayoitawala kuwa wao ni Waafrika asili kwa mavazi wanayovaa.
“Wapo wanaovaa vitenge au kofia kama Mobutu aliyekuwa anavaa kofia ya ngozi ya chui, lakini hakuwa na nia ya dhati ya kulikomboa bara hili. Lazima tuwe Waafrika kutoka moyoni,” anasema Kamara.
Naye Profesa Mathew Luhanga akichangia mjadala huo anasema ili kuhakikisha kuwa taifa linatimiza malengo yake ya kujikomboa ni lazima kuwe na uhusiano mzuri kati ya watunga sheria na wasomi.
“Kuna pengo kubwa kati ya watunga sheria na wasomi, hiki nacho ni kikwazo kwa maendeleo,” anasema Profesa Luhanga.

No comments:

Post a Comment