Monday, April 22, 2013

Shyrose Banji akubali matokeo CHANETA.




ALIYEKUWA mgombea nafasi ya uenyekiti katika uchaguzi mkuu wa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA), Shyrose Bhanji, amempongeza Anna Kibira kwa ushindi katika nafasi hiyo nyeti katika kupigania mafanikio ya mchezo huo.
Pongezi hizo zilitolewa juzi usiku ikiwa ni saa chache baada ya kwisha kwa uchaguzi huo, ambapo kwa nafasi ya uenyekiti, Kibira aliyewahi kuwa katibu mkuu wa chama hicho katika uongozi uliomaliza muda wake, alishinda kwa kura 61 dhidi ya 21 za Shyrose.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Kigali, Rwanda, anakoshiriki kikao cha Bunge la Afrika Mashariki, Shyrose alisema amefarijika chama hicho kufanya uchaguzi na anautakia heri na mafanikio uongozi mpya.
“Nampongeza dada Kibira (Anna) kwa ushindi na ninamtakia mafanikio yeye na uongozi wake katika kupigania mafanikio ya mchezo wa netiboli, naamini ushindi wake ni ushindi wa mchezo huo,” alisema.

Alisema kutokana na upenzi wake katika michezo, pamoja na kutoshinda kwa nafasi hiyo, atakuwa tayari kushirikiana na uongozi mpya katika kuendeleza harakati za kupigania mafanikio ya mchezo huo kwa maslahi ya vijana na taifa.
“Kwa upande wangu naahidi jambo moja kwamba niko tayari kusaidiana na uongozi mpya kama utahitaji kwa maslahi ya mchezo wa netiboli, nikiamini michezo sasa si burudani na afya tu, pia ni ajira kwa vijana wenye vipaji,” alisema Shyrose aliyekuwa makamu mwenyekiti katika uongozi uliopita chini ya Anna Bayi.
Wengine waliochaguliwa juzi ni Zainab Mbiro Makamu Mwenyekiti, Agness Hatib Mweka Hazina huku wajumbe wa Kamati ya Utendaji ni Yasinta Silvester, Fortunata Kabeja, Asha Sapi, Penina Igwe, Hilda Mwakatobe na Judith Ilunda.
 MJENGWA BLOG

No comments:

Post a Comment