Thursday, May 30, 2013

BALOZI BISWARO AWAPA CHANGAMOTO STARS

                                               Afisa Habari wa TFF Boniface Wambura.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Mei 30, 2013





Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Joram Biswaro amewataka wachezaji wa Taifa Stars kuhakikisha wanaipeleka timu hiyo kwenye fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Brazil.



Ametoa changamoto hiyo wakati alipotembelea mazoezi ya timu hiyo jana (Mei 29 mwaka huu). Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imepiga kambi nchini Ethiopia na inafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Addis Ababa.



“Watanzania tunafurahi kutokana na uwezo mnaouonyesha, hasa baada ya kuifunga Morocco mabao 3-1. Kama mliwafunga nyumbani hata kwao mnaweza kuwafunga. Tunataka kuwaona Maracana (Brazil) mwakani, mimi tayari ninayo tiketi mtanikuta kule,” amesema Balozi Biswaro ambaye enzi zake aliwahi kuichezea timu ya Yanga.



Taifa Stars ambayo iko Addis Ababa tangu Jumatatu (Mei 27 mwaka huu) imeweka kambi katika hoteli ya Hilton ambapo Jumapili (Juni 2 mwaka huu) itacheza mechi ya kirafiki na Sudan (Nile Crocodile) kwenye Uwanja wa Addis Ababa.



Balozi Biswaro ameikaribisha Taifa Stars ubalozini Addis Ababa mara baada ya mechi dhidi ya Sudan ambapo itakutana na baadhi ya Watanzania wanaoishi Ethiopia kabla ya kuondoka alfajiri kwenda Marrakech, Morocco kwa kupitia Cairo, Misri.



Kocha Kim Poulsen amesema kikosi chake kinaendelea na mazoezi vizuri na kitaimarika zaidi baada ya wachezaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) kujiunga nacho Juni 3 mwaka huu jijini Marrakech kwa ajili ya mechi dhidi ya Morocco itakayochezwa Juni 8 mwaka huu.



Wachezaji walioko katika kikosi cha Stars jijini Addis Ababa ni Juma Kaseja, Aggrey Morris, Mwadini Ally, Ally Mustafa, Shomari Kapombe, Kevin Yondani, Erasto Nyoni, Haroub Nadir, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Khamis Mchana, Amri Kiemba, Salum Abubakar, Simon Msuva, John Bocco, Vicent Barnabas, Mudathiri Yahya, Athuman Idd, Haruni Chanongo na Zahoro Pazi.



Boniface Wambura

Ofisa Habari

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Addis Ababa

+251 919910240

Rais Tenga kuzindua kozi ya Makocha Jumatatu


RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodger Tenga anatarajia kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa kozi ya makocha wa ngazi ya pili (Intermediate) itakayofanyika Jumatatu (Juni 3, 2013) kwenye Ukumbi wa Hobours Club, uliopo Kurasini jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Ufundi Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Joseph Kanakamfumu, alisema Rais Tenga atakuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa kozi hiyo itakayohusisha amakocha 26.

Alisema kozi hiyo itakayomalizika Juni 28 itakuwa imewezesha kupatikana makocha watakaosaidia maendeleo ya mchezo huo katika Mkoa wa Dar es Salaam na Taifa kwa ujumla.

Aliwataja makocha wa kozi hiyo kuwa ni Shadrack Nsajigwa, Benard Mwalala, Steven Nyenge, Jemedari Said Kazumari, Zubeiri Katwila, Ibrahim Masoud ‘Maestro’, David William Ngaga, Idd Abushir Mwinchumu, Rajab Mohamed Nakuchema, Lubigisa Madata, Bakari Mahad, Greyson Swai, Chiwanga  A. Chiwanga, Sizza Mapunda na  Muhibu Kanu.

Wengine ni Omari Mbarouk, Omari Mohamed, Samuel Galafawo, Abdallah Mbogolo, Hassan Msonzo, Akida Said, Emanuel Gabriel, Barton Msengi, Edgar Method Katembo, Elly Kaiza na Renatus Benard.  



Kozi hiyo ni ya kwanza kuendeshwa na DRFA tangu kuingia kwa uongozi mpya wa chama hicho Desemba 12, chini ya Mwenyekiti Almas Kassongo.

Wengine walioingia madarakani katika uchaguzi huo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Mbezi Garden ni Meba Ramadhan (Makamu Mwenyekiti), Msanifu Kondo (Katibu), Muhsin Said (Mwakilishi wa Mkutano Mkuu wa TFF), Benny Kisaka (Mwakilishi wa Klabu), Ally Hobe (Mhazini) na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji Mohamed Shabani, Sunday Mwanahewa na Bakari Mapande.

HAFIDH KIDO
kidojembe@gmail.com

Sakata la wabunge wa Kenya kujiongezea mishahara.

Rais Wa Kenya Uhuru Kenyatta ametoa kauli kali kupinga hatua ya wabunge wa Kenya kutaka kujiongezea mishahara. Rais Kenyatta amesema kuwa taasisi zote za serikali na afisi zingine zote za umma zitafuata mapendekezo yaliyotolewa na tume ya kudhibiti mishahara bila upendeleo wowote.

Wabunge wa Kenya wamekuwa wakilumbana na tume hiyo wakidai imewanyanyasa kwa kuwapunguzia mishahara yao.
Taarifa zinazohusiana

Kenyatta emesema malumbano kati ya wabunge na tume hiyo imelemaza kazi za serikali na kwa hilo rais Kenyatta emewataka wabunge kukomesha kero zao kwa kushirikiana na tume ya kudhibiti mishahara ili kuelezea malalmiko yao kwa kufuata sheria.

Mapema Jumanne tume hiyo ya mishahara , ilitoa onyo kwa makarani wa bunge wenye jukumu la kuwalipa mishahara wabunge kuwa huenda wakapatikana na hatia ya kutumia vibaya mamlaka yao na kufuja pesa za umma ikiwa watawalipa mishahara ya juu wabunge kinyume na ile iliyowekwa na tume hiyo katika gazeti rasmi la serikali.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Sarah Serem ameonya kuwa makarani wa bunge la taifa Justin Bundi na yule wa Senate, Jeremiah Nyegenye huenda wakapatikana na hatia ya matumizi mabaya ya mamlaka ikiwa watakiuka agizo hilo.

"katiba inatupa mamlaka ya kudhibiti mishahara ya maafisa wa serikali. Na hivyo ndivyo tulivyofanya,'' alisema mwenyekiti wa tume hiyo Bi Serem.

Bi Serem alisema kuwa tume hiyo ilichapisha mishahara watakayopokea wabunge kwenye gazeti rasmi la serikali kwa ilikuwa kwa nia nzuri.

"SRC haikushurutishwa kuchapisha taarifa hiyo katika gazeti rasmi la serikali. Lakini tuliamua kufanya hivyo kwa nia njema na ili wananchi waweze kupata habari hiyo.'' aliongeza Bi Serem

Tume hiyo hata hivyo iliwapongeza Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto kwa kusisitiza kuwa serikali ipunguze matumizi ya pesa za uma.

Bi Serem alisema kuwa hatua hiyo ilichukuliwa na wawili hao ili kutenga pesa kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Onyo la tume limekuja siku moja baada ya wabunge kupiga kura kupinga tangazo la tume hiyo kwenye gazeti rasmi la serikali kuhusu kiwango cha pesa watakachopokea wabunge.

Tangazo hilo lilisema kuwa kila mbunge atapokea shilingi laki tano za Kenya ambazo ni dola elfu sita. Wabunge hao wanapigania kulipwa dola elfu kumi na kuwafanya kuwa miongoni mwa wabunge wanaopokea kiasi kikubwa sana cha mishahara duniani
BBC SWAHILI

NAMNA MIKOA YA MTWARA NA LINDI INAVYONUFAIKA NA UTAFUTAJI NA UENDELEZAJI WA GESI ASILIA

SHIRIKA LA MAENDELEO YA PETROLI TANZANIA



1.0 UTANGULIZI
Gesi asilia iligunduliwa kwa mara ya kwanza hapa nchini Mwaka 1974 kwenye Kisiwa cha Songo Songo, Mkoani Lindi. Ugunduzi mwingine umefanyiaka katika maeneo ya Mtwara Vijijini (Mnazi Bay-1982 na Ntorya-2012), Mkuranga (Pwani, 2007) na Kiliwani (Lindi, 2008). Kiasi cha gesi asilia iliyogunduliwa katika maeneo haya inakadiriwa kuwa futi za ujazo trilioni 8. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, kumekuwa na kasi kubwa ya utafutaji mafuta na gesi asilia uliojikita zaidi kwenye maji ya kina kirefu cha bahari. Kiasi cha gesi asilia iliyogunduliwa katika kina kirefu cha maji ni takribani futi za ujazo trilioni 33.7. Jumla ya gesi asilia iliyogunduliwa nchi kavu na baharini inafikia takribani futi za ujazo trilioni 41.7.
Rasilimali hii ya gesi asilia inaweza kutumika katika maeneo mbalimbali yakiwemo; kuzalisha umeme, malighali ya kuzalishia mbolea na kemikali, nishati viwandani, majumbuni na kwenye taasisi mbali mbali. Pia gesi asilia inatumika kama nishati ya kuendeshea magari.



FAIDA YA GESI ASILIA MKOA WA LINDI
1. Mradi wa gesi asilia wa Songo Songo- LINDI
(i) Kodi ya Huduma (Service Levy):
Songo Songo huzalisha gesi asilia takribani futi za ujazo milioni 102 kwa siku na kuletwa Dar es Salaam kwa ajili ya kufua umeme na kutumika viwandani. Kufuatana na kodi ya huduma (Service levy) Halmashauri ya Lindi inapata asilimia 0.3 ya mauzo ya gesi hiyo. Toka mwaka 2004 wakati mradi wa Songo Songo Songo ulipoanza kuzalisha gesi hadi kufikia mwisho wa 2012, Halmashauri imepata jumla ya Shs. 885 milioni. Wastani wa mapato kwa kila miezi mitatu ni Shillingi 110 millioni.

(ii) Umeme:
§ Wananchi wa Kisiwa cha Songo Songo hupata umeme wa uhakika na bure.
§ Mara tu Bomba la Gesi litokalo Songo Songo likifika nchi kavu sehemu ya Somanga Fungu, Serikali imefunga mitambo ya kufua umeme. Umeme unaofuliwa Somanga Fungu ni MW 7.5 unaotumika ni takribani MW 2.5. Umeme huu wa ziada unatoa fursa kwa viwanda kujengwa katika mkoa wa Lindi.

(iii) Maji Safi:
§ Mradi unatoa maji safi kwa wakazi wa Songo Songo kwa kuhudumia kisima cha Kijiji.

(iv) Huduma za jamii:
§ Kila mwaka wanafunzi kumi bora waliofaulu wanafadhiliwa na mradi kwenda shule ya Sekondari ya Makongo. Wanafunzi hawa wanaofaulu vizuri watafadhiliwa hadi vyuo vikuu.
§ PanAfrican (PAT) wamejenga Shule ya chekechea Songo Songo na watoto wanahudumiwa na kampuni hiyo.
§ PAT wamepeleka waalimu wawili wa chekechea katika mafunzo ya muda mrefu.
§ Zahanati ya Songo Songo imekarabatiwa na kuongeza baadhi ya vifaa.
§ Bweni la wasichana limejengwa na kuikarabati Shule ya Sekondari ya Songo Songo.
§ Ajira hutolewa kwa wakazi wa kijiji cha Songo Songo.
Huduma hizi za jamii zimegahrimiwa kwa kiasi cha Shilingi milioni 730 ($455,000) kwa kipindi cha 2004 hadi Desemba 2012.

2. Manufa kutokana Kampuni ya Maurel and Prom.
Katika shughuli za utafutaji mafuta Kampuni hii imejenga barabara ya kudumu ya kilometa 15 kutoka Somangafungu hadi Kinjumbi. Aidha Kampuni pia imejenga zahanati kwa ajili ya Kijiji cha Kinjumbi.

3. Manufaa kutokana na Kampuni ya Statoil
Wamepeleka wawakilishi wa wananchi wa Mkoa wa Lindi kwenye ziara ya mafunzo ya Mitambo ya Kusindika Gesi Asilia (LNG) nchini Norway.

4. Wizara ya Nishati na Madini.
Mwaka huu wa Fedha Wizara ya Nishati na Madini imefadhili wanafunzi 55 katika Chuo cha VETA Lindi kwenye fani mbali mbali za ufundi.

5. Kiwanda cha Mbolea Mkoani Lindi.
Serikali inafanya majadiliano na Kampuni kadhaa zilizoonyesha nia kutaka kujenga Kiwanda cha Mbolea Mkoani Lindi. Mazungumzo yatakamilika kabla ya mwisho wa mwaka huu.

FAIDA KWA MKOA WA MTWARA
1. Kodi ya Huduma na Umeme.
Gesi asilia iliyopo Mnazi Bay ilianza kutumika mwishoni mwa mwaka 2006 kwa kuzalisha umeme wa uhakika unaotumika mjini Mtwara. Uwezo wa mitambo iliyofungwa mjini Mtwara ni MW 18 lakini uzalishaji wake kutokana na mahitaji ni MW 12. Halmashauri ya Mtwara Vijiji hupata kodi ya Huduma (Service Levy) ya asilimia 0.3 ya mauzo gesi hiyo. Kwa wastani Halmashauri hupata Shilingi milioni 16 kwa mwaka. Kiasi hiki ni kidogo kutokana na uzalishaji na uuzaji mdogo wa gesi ingawa uwezo wa kuzalisha gesi kwenye visima vyote vinne vilivyopo Mnazi Bay kufikia futi za ujazo milioni 130 kwa siku upo. Kuanzia mwaka 2006, Mkoa wa Mtwara wanapata umeme wa uhakika unaozalishwa kutokana na gesi asilia ya Mnazi Bay.

1. Mafunzo
Mwaka 2010, Kampuni ya Petrobrass wametumia $350,000 (sawa na Shilingi 560 milioni) kufundisha na kuleta vifaa VETA Mtwara. Wanafunzi 50 (wakufunzi 2) walifundishwa kwenye fani ya umeme na makanika. Aidha, Kampuni ya BG wameendesha pia mafunzo na VETA – Mtwara mwaka 2012 kwenye fani za English language, food preparation, plumbing, welding, carpentry, motor vehicle, electrical installation and maintenance.

Katika Mwaka wa Fedha 2012/13, Wizara ya Nishati na Madini imetoa ufadhili wa wanafunzi 50 kusoma Chuo cha VETA – Mtwara.

2. Huduma za Jamii:
Kampuni ya BG imetumia jumla ya Dola za Marekani 557,028 sawa na Shilingi 891 milioni katika yafuatayo:
§ Kukarabati majengo ya shule za sekondari Mkoani Lindi
§ Madawati 600 yalisambazwa kwa shule za msingi Wilayani Mtwara Mjini.
§ Mafunzo ya Usalama Barabarani kwa shule za msingi katika Mkoa wa Mtwara – wanafunzi 14,611 wamefaidika
§ Usalama Barabarani katika Mkoa wa Mtwara – kwa wapanda Pikipiki
§ Kukarabati Maktaba ya Shule ya Sekondari ya Wasichana Mtwara
§ Hifadhi ya fukwe za bahari na (marine park) na Aga Khan Msimbati.
§ kukarabati shule za sekondari, kutoa elimu ya usalama barabarani kwa shule za msingi na mafunzo kwa madereva wa boda boda.
Kampuni ya Wentworth Resources inayofanya utafiti na uendelezaji wa Mnazi Bay nayo imetumia Dola za Marekani 551,333 sawa na Shilingi milioni 882 katika huduma zifuatazo:
§ kusambaza maji kwa shule za Mnolela na Msimbati, Mtwara Vijijini.
§ wamesambaza umeme kwenye shule ya Mnolela,
§ Wamejenga jengo la utawala, mabweni, madarasa matano, nyumba za waalimu, jiko, jengo la kulia chakula na vyoo kwenye shule ya Mnolela Kijiji cha Ruhokwe.
§ Wametoa vitanda na magodoro kwa shule hii.
§ wamejenga mabweni ya wasichana,
§ kujenga, ufadhili wa masomo na michezo na kukarabati shule mbalimbali.
§ Uchimbaji visima vya maji kwa ajili ya Kijiji cha Mnete, ukarabati barabara za vijiji, ujenzi wa darasa moja kwa ajili ya Shule ya Msingi Msimbati na uwanja wa mpira wa miguu kwa Shule ya msingi Msimbati.
§ Ajira kwa wanavijiji 10 kutoka kijiji cha Msimbati kwa ajili ya kutengeneza boti na kwa Mwaka 2013 kukarabati majengo ya shule ya Sekondari ya Msimbati.
§ Januari 2013 mchango kwa ajili Mafuriko.

Kampuni ya Dominion kwenye huduma za jamii imechangia Dola za Marekani 82,000 sawa Shilingi milioni 131 kama ifuatavyo:
§ Kuanzia 2007 hadi 2010, vijiji kumi vya Mandawa na Kisangire, vilipewa kila kimoja Shs. 5 milioni kwa ajili ya ukarabati majengo ya utawala, mabweni ya shule na kliniki. Jumla Shs. 50 milioni zilitumika.
§ Mwaka 2010 na 2011 Kampuni ilitumia shs. 10 milioni kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu hifadhi ya viumbe bahari kwa wanavijiji wa vijiji vya mwambao.
§ Mwaka 2011 na 2012 Kampuni ilitoa msaada wa $ 22,000 (sawa na Tsh. 35 milioni) kwa Chuo cha mambo ya Bahari kwa ajili ya masomo ya shahada za uzamivu kwa wanafunzi wawili kutoka Mtwara.

Kampuni ya Ophir East Africa Ventures Ltd - Tsh 34,000,000
§ Mwaka 2011 Kampuni ilisaidia Watawa wa Benedictine kwa ajili ya Dispensary/Clinic ya Shangani.
§ Mwaka 2012 Kampuni ilisaidia Shs. 16,000,000 kwa Watawa wa Benedictine kwa ajili ya Dispensary/Clinic ya Shangani.

3. Utafutaji wa Mafuta na Gesi kwenye Kina Kirefu Cha Bahari
Shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika kina kirefu cha bahari zinaendelea na zimeleta manufaa makubwa kwa wananchi wa Mikoa ya kusini. Kati ya manufaa hayo ni:
• Ajira
Uanzishwaji wa eneo la kupokelea vifaa vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia, Mtwara Supply Base kwenye Bandari ya Mtwara na uchimbaji wa gesi baharini umeajiri wafanyakazi wengi katika kada mbalimbali kama vile udereva, uboharia, waendesha mitambo na ufundi mbalimbali;
• Eneo la huduma za utafutaji wa mafuta na gesi asilia (Oil Field Supply Hub) lilianzishwa Mwaka 2010 ndani ya Bandari ya Mtwara, mahususi kwa ajili ya kuhifadhi vifaa vya utafutaji na uchorongaji wa visima vya mafuta na gesi katika kina kirefu cha bahari. Katika kutekeleza hili faida zifuatazo zimepatikana:
§ Bandari ya Mtwara imekarabatiwa;
§ Shughuli za Bandari zimeongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka kuhudumia usafirishaji wa korosho tu na kuwa kitovu cha ugunduzi wa gesi yote kwenye kina kirefu cha maji baharini;
§ Bandari ya Mtwara sasa imekuwa chimbuko kubwa la ajira kwa watu wa Mtwara;
§ Bandari ya Mtwara imekuwa yenye ufanisi wa hali ya juu, yenye gharama nafuu na ya kisasa.

3. Kiwanda cha Saruji cha Dangote.
Kiwanda kitakuwa kinazalisha saruji kwa kutumia nishati ya gesi asilia ya Mnazi Bay. Kiwanda kimekwishaanza kujengwa na kinategemewa kukamilika ndani ya miaka miwili. Kiwanda kitakuwa kikubwa kuliko chochote Kusini mwa Sahara, ambacho kitazalisha tani 3,000 kwa siku. Kiwanda kitakapokamilika kitatoa faida zifuatazo:

• Ajira rasmi kwa wananchi takribani 500 na zile zisizo rasmi takribani watu 800;
• Kitakuza uchumi wa wananchi wa Mikoa ya Kusini pamoja na Watanzania kwa ujumla; na
• Saruji itakayozalishwa itasafirishwa kwa kutumia meli na barabara, hivyo kuongeza shughuli za Bandari ya Mtwara.

4. Karakana ya Kifundi ya Schlumberger.
Kampuni ya Schlumberger ambayo hutoa huduma kwa kampuni za utafutaji mafuta na gesi imejenga karakana kubwa na ya kisasa mjini Mtwara kwa ajili ya kuhudumia utafutaji wa mafuta na gesi nchini, Msumbiji, Kenya, Uganda na Afrika kusini. Karakana hii imekamilika na inategemewa kuajiri wafanyaka takriban 100.

5. Mitambo ya kusafishia gesi asilia
Ili kuhakikisha ajira na faida nyinginezo zinabaki maeneo ambayo gesi inazalishwa, Serikali imeamua mitambo ya kusafisha gesi ijengwe maeneo yanayozalishwa gesi hiyo.

Kwa hivi sasa, Serikali kwa kupitia TPDC inajenga mitambo ya kusafisha gesi katika Kijiji cha Madimba Wilaya ya Mtwara Vijijini yenye uwezo wa wa kusafisha futi za ujazo milioni 210 kwa siku. Vilevile inajenga mitambo mingine katika kijiji cha Songo Songo mkoani Lindi yenye uwezo wa kusafisha futi za ujazo milioni 140 kwa siku. Mitambo itakapo kamilika itatoa fursa zifuatazo:

• Fursa ya ajira kwa wastani wa wafanyakazi sitini (60) kwa Mtwara na sitini (60) kwa ule wa Songo Songo (Lindi);
• Pia itatoa ajira zisizo rasmi kwa wananchi watakao toa huduma kwa wataalam kama vile chakula, afya, elimu, maji, usafiri pamoja na huduma nyingine za kijamii zitakazo hitajika;
• Kutajengwa mitambo ya kusafishia maji ambapo vijiji vilivyo maeneo ya jirani vitapatiwa maji safi. Hadi sasa tayari Mkandarasi ameshakamilisha uchimbaji wa visima vya maji eneo la Madimba vyenye uwezo wa kuzalisha mita za ujazo mia moja na hamsini (150) kwa saa (150m3/hr). Sehemu ya maji hayo yatatumika katika mtambo wa kusafishia gesi na sehemu nyingine itahudumia wana kijiji.

6. Ujenzi wa Mitambo ya Liquefied Natural Gas (LNG)

Ugunduzi wa gesi asilia katika kina kirefu cha bahari kimepelekea Serikali pamoja na Makampuni ya utafutaji kuamua kuwekeza katika uzalishaji wa LNG. Mitambo ya LNG itajengwa nchi kavu kwenye Mikoa ya Lindi na Mtwara.

7. Ujenzi wa Kiwanda cha Mbolea (Urea)

Kwa kuzingatia sera ya kilimo kwanza, Serikali inatarajia kujenga kiwanda cha Mbolea kwa kutumia gesi asilia katika Ukanda wa Mikoa ya Kusini. Hadi sasa Serikali inafanya mazungumzo na Makampuni mbalimbali ambayo yameonesha nia ya kuwekeza katika mradi huu. Kampuni nyingi zimeonesha nia ya kujenga kiwanda cha mbolea Mtwara kwa kutumia gesi asilia ya Mnazi Bay. Kiasi cha mtaji unaohitajika kwa ujenzi wa mtambo wenye uwezo wa kuzalisha tani 3,800 za mbolea (Urea) ni takribani Dola za Marekani bilioni 1.7. Kiwanda hiki kitatumia kiasi cha gesi ipatayo futi za ujazo milioni 60 kwa siku.
Eneo la Mnazi Bay lina kiasi kikubwa cha gesi asilia ya kutumika katika viwanda mbali mbali vikiwemo vya mbolea. Kiwanda cha Mbolea kitakapokamilika kitatoa faida zifuatazo:

• Ajira kwa wananchi. Kwa kiwanda kitachotumia chenye uwezo wa kuzalisha tani 3200 kwa siku kitaajiri wastani ya watu 400 kwa ajira rasmi na ajira 1,600 zisizo rasmi;
• Kitakuza uchumi wa wananchi wa mikoa ya kusini pamoja na Watanzania kwa ujumla;
• Kutokana na mbolea kuzalishwa hapa nchini, ni wazi kuwa pembejeo hii itapatikana kwa bei nafuu na hivyo kuongeza kipato kitokanacho na kilimo; na
• Mbolea itakayozalishwa itasafirishwa kwa kutumia meli na barabara, hivyo kuongeza shughuli za bandari ya Mtwara.

8. Ujenzi wa Kiwanda cha Amonia

Wawekezajiwengi wameonesha nia ya kujenga kiwanda cha kuzalisha Amonia kwa kutumia gesi asilia ya Mnazi Bay. Kiwanda kinakadiriwa kuwa na uwezo wa kuzalisha tani 3,000 za Amonia kwa siku na kitagharimu takribani Bilioni 1.6 dola za marekani na kitatumia gesi asilia kiasi cha fut iza ujazo milioni 160 kwa siku.Kiwanda hiki kitakapo jengwa kitatoa ajira kwa watu wapatao 400 kwa ajira rasmi na zaidi ya watu 1,500 kwa ajira zisizo rasmi.

9. Mitambo ya kuzalisha umeme

Mradi wa kuzalisha umeme upatao Megawati 400 utatekelezwa kama sehemu ya upanuzi wa mitambo iliyopo sasa huko Mtwara. Katika kutekeleza wa mradi huu, Serikali kwa kupitia Tanesco, imeingia ubia na Kampuni ya Symbion kuweka mitambo ya kuzalisha umeme mjini Mtwara kutokana na gesi asilia ya Mnazi Bay.

Pamoja na Mikoa ya Mtwara na Lindi umeme utakaozalishwa unatazamiwa kuunganishwa kwenye gridi ya Taifa na pia utasambazwa katika Wilaya za Newala, Namtumbo, Mbinga, Songea pamoja na sehemu nyinginezo.

10. Ujenzi wa Kiwanda cha Methanol

Wawekezaji mbali mbali wa viwanda vya Kemikali wanataka kujenga Kdiwanda cha kuzalisha Methanol kwa kutumia gesi asilia. Kiwanda hiki kinatarajiwa kiwe na uwezo wa kuzalisha tani 5,000 za methanol kwa siku na kitagharimu Bilioni 1.7 Dola za Marekani na kitatumia gesi asilia kiasi cha futi za ujazo milioni 180 kwa siku. Kiwanda kitakapo jengwa kitatoa ajira kwa watu wapatao 400 kwa ajira rasmi na zaidi ya watu 1,500 kwa ajira zisizo rasmi.

11. Uanzishwaji wa Ukanda huru wa Bandari (Free Port Zone)

Ili kuhakikisha sekta ya uchimbaji wa mafuta inafanikiwa ni muhimu kwa serikali kuandaa mazingira yatakayovutia makampuni yanayotoa huduma na yanayouza malighafi na vitendea kazi kwenye sekta hiyo. Aidha, ili kutengeneza hayo mazingira kuwa mazuri kwa makampuni ya huduma, malighafi na vitendea kazi, serikali imetenga eneo maalum ndani ya Bandari ya Mtwara ambalo litawekewa miundombinu ya msingi na kutoa vivutio mbali mbali kwa makampuni hayo. Eneo hilo litapewa hadhi ya Ukanda Huru wa Bandari (Freeport Zone). Huduma za shughuli za utafutaji na uzalishaji wa gesi na mafuta nchini zitapatikana Mtwara badala ya kwenda nje ya nchi kutafuta huduma hizo. Hii itaongeza ajira kwa wakazi wa maeneo ya Kusini na kukuza uchumi.

Faida za Ukanda Huru wa Bandari (Freeport Zone) ni kama zifuatazo:
• Kuvutia uwekezaji wa kigeni;
• Kukuza makusanyo ya mapato ya serikali kupitia kodi ya mapato (Corporate Tax), ushuru wa forodha na VAT pale ambapo bidhaa zitaingizwa ndani ya nchi, PAYE na tozo za bandarini (Port Charges);
• Kukuza makusanyo ya mapato ya fedha za kigeni kupitia bidhaa zitakazouzwa nje ya nchi kwa kuwa eneo hili litakuwa kama kiunganishi (hub) cha Afrika Mashariki na Kati;
• Kukuza ajira;
• Kukuza biashara za kimataifa;
• Kukuza uchumi wa nchi; na
• Kukuza na Kuboresha uwezo wa kiteknolojia.

Kwa taarifa zaidi na ufafanuzi wasiliana na:
Mkurugenzi Mtendaji
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania
S.L.P 2774
Simu: 2200103/4 & 2200112
Fax: 2200113
Dar es Salaam
Email: tpdcmd@tpdc-tz.com
Website: http://www.tpdc-tz.com

Sababu za kifo cha msanii wa Tanzania nchini afrika Kusini, ni hizi.

Mangwea (katikati) akiwa katika moja ya harakati zake za muziki enzi za uhai wake.
Wadau mbalimbali wa sanaa ya muziki Tanzania wakiwa katika viwanja vya Leaders Club jana kujadili na kuunda kamati itakayoshughulikia kuusafirisha mwili wa msanii huyo. Mpaka jana taarifa zilizopatikana na kuwa mwili unahitaji Sh mil 30, ili kuweza kuusafirisha kutoka Afrika Kusini. 
Mtangazaji wa kituo cha Clouds FM, Millard Ayo akifanya mahojiano na mmoja wa watu walio Afrika Kusini kuhusiana na msiba huo wakati aliposafiri mpaka Hospitali aliyofariki Mangwea.



Dar es Salaam. Wakati mazishi ya mwanamuziki marehemu Albert Mangwea(28) maarufu kama `Ngwair’ yakitarajiwa kufanyika mjini Morogoro, maeneo ya Kihonda baada ya mwili kuwasili nchini, hospitali iliyomfanyia vipimo imethibitisha kuwa pombe na dawa za kulevya kupita kiasi ndivyo vilivyomuua.

Mwili wa mwanamuziki huyo, ambaye alitamba kwenye miaka ya 2000 na wimbo wa `Mikasi’, unatazamiwa kuletwa kesho nchini na kuagwa Jumamosi kabla ya kusafirishwa kwenda kwao Kihonda, Morogoro kwa mazishi.

Kwa mujibu wa taarifa Mangwea alifariki dunia juzi kwenye Hospitali ya St Hellen, iliyopo Johannesburg, Afrika Kusini alikokuwa amekwenda kwa shughuli za muziki.

Kifo chake

Ripoti iliyochapwa na mitandao mbalimbali ya ndani na nje ya nchi inasema marehemu alifikwa na umauti baada ya kulewa kupindukia, kibaya zaidi alikuwa hajala.

Siku ya kifo chake, Mangwea alianguka nyumbani kwa rafiki zake akiwa katika hali hiyo ya kulewa sana.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, baada ya kufikishwa hospitalini, Mangwea aligundulika kulewa mara tano ya kipimo cha kilevi kilichopitishwa na serikali ya Afrika ya Kusini, ambacho ni 416mg za pombe kwenye kila milimita 100(kwa mlevi anayeendesha chombo cha moto).

Pia marehemu alikutwa na upungufu wa hewa ya oksijeni kwenye seli na tishu za mwili wake.

Ripoti hiyo ilibainisha kuwa Mangwea, maarufu Ngwair, alikuwa na tatizo la kutokula chakula vizuri kabla ya kifo chake na pia kukosa muda wa kupumzika.

Sampuli zilizopatikana mwilini mwake zinaonyesha mkusanyiko wa dawa za kulevya mbalimbali zikiwemo heroine, cocaine chafu na bangi ya gramu 0.08 ambavyo vilikutwa kwenye damu yake.

Kifo chake kilitokana na mshtuko wa moyo na kushindwa kupumua, hali iliyosababisha mapigo ya moyo wake kusimama kwa sekunde chache, na kusababisha kifo chake.

Mwili wa Ngwair ulionekana kana kwamba alitokwa na damu nyingi puani baada ya kuonyeshwa kwa Watanzania wengi jana jioni Johannesburg, Afrika Kusini.

Taarifa za awali zilizotolewa na rafiki wa karibu aliyepo nchini Afrika Kusini, aliyejitambulisha kwa jina moja tu la Jonathan zilidai kuwa marehemu hakuamka tangu alipopumzika usiku wa kuamkia juzi.



M2 The P naye mahututi

Rafiki wa Ngwair aliyekuwa naye siku ya tukio, ambaye pia ni msanii, Mgaza Pembe maarufu kwa jina la `M2 To The P’ naye alifikishwa katika Hospitali ya St Hellen baada ya kukutwa amepoteza fahamu akiwa na Ngwair. Msanii huyo, ambaye makazi yake yako Kibaha mkoani Pwani, aliwahi kutamba na wimbo wa ‘M2 To the P’ na ule wa hivi karibuni wa `Nyumbani’.

Historia ya Ngwair

Ngwair alizaliwa Novemba 16, 1982 jijini Mbeya, ni mtoto wa mwisho kuzaliwa kwa baba akiwa mtoto wa 10 na kwa mama akiwa mtoto wa sita. Ngwair asili yake ni Ruvuma kabila la Wangoni. Akiwa na miaka mitano walihamia Morogoro akasoma Shule ya Msingi Bungo alipofika darasa la tano, baba yake akapata uhamisho kwenda Dodoma. Baadaye alisoma Shule ya Sekondari ya Mazengo kabla ya kujiunga na Chuo cha Ufundi Mazengo.

Aliondoka lini?

Ngwair aliondoka nchini mwaka huu mwezi Machi, tarehe 26 kwa mwaliko wa kisanii ambapo tangu kipindi hicho, amekuwa akifanya onyesho moja kila mwezi na mara ya mwisho, onyesho lake lilikuwa wiki mbili zilizopita.

P Funk: Ngwair Ana nyimbo 50 ambazo hazijatoka!

Paul Mathyesse, a.k.a P Funk ambaye ni mtayarishaji aliyefanya idadi kubwa ya muziki wa Ngwair, ameiambia Mwananchi kuwa hadi sasa haelewi nini kimetokea lakini anachofahamu kuwa Albert Mangwea ni zaidi ya msanii kwake na ni kati ya wasanii aliofanya nao kazi nyingi.

Alisema kila ambacho amekuwa akimfundisha na kumwelekeza ndicho alichokifanya kwa kuwa alikuwa na uwezo wa kuimba aina zote za muziki Hip Hop, Free style na ragga.

“Nilikuwa na Ngwair kwa zaidi ya miaka 13, ninamfahamu vizuri na ninaujua uwezo wake, alikuwa ni zaidi ya rafiki yaani sina neno zuri la kusema kumhusu zaidi ya kumtakia safari njema,”alisema.

P- Funk pia ni Mkurugenzi wa Bongo Records ambayo marehemu alikuwa akifanyia kazi zake hadi anafikwa na umauti.

P –Funk anafafanua kuwa hata albamu zote mbili za Ngwair yeye ndio amefanya ukiachilia mbali nyimbo ambazo alikuwa akifanya moja, moja ambazo hadi sasa wanazo nyimbo 50 ambazo hawajazitumia.

Anasema alikutana na Ngwair mwaka 2000 ambapo alikwenda studio na rafiki yake ambaye hamkumbuki jina ilipofika wakati wa kuimba ndio alipokigundua kipaji chake na kumsainisha mkataba na wimbo wao kwanza ulikuwa ni ‘Gheto langu’.

Anaendelea kusema kuwa hata kumtambulisha kwa mashabiki mikoani kwa mara ya kwanza walifanya wao ambapo aliunganishwa kwenye ziara ya ‘wimbo wa nini cH chanzo’ wa Juma Nature,mwaka 2001.

Maneno ya mwisho aliyoandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Ilikuwa ni Mei 26 Ngwair aliweka ujumbe huu kwenye ukurasa wake wa Twitter,”Namuhitaji Mungu kwa kila dakika kila saa,” akitumia lugha ya Kiingereza.



Maneno ya mwisho kuzungumza na mama yake

Ilikuwa ni wiki mbili zilizopita Ngwair aliwasiliana na mama yake na kumtaka aendelee kumwombea au waombeane na kumwahidi angerudi Ijumaa iliyopita na hakuwasiliana naye tena hadi anafikwa na umauti.



Baadhi ya watu aliowahi kufanya nao kazi wazungumzia kifo chake

Mchezaji Adam Nditi aliandika kupitia ukurasa wake wa Twitter R.I.P Albert Ngwair You will be missed by many Tanzanians.

Mtangazaji wa Clouds Loveness aliandika kwenye ukurasa wake kuwa “Yani siamini Ngwair amefariki dunia nini ilichomkuta #RIP # Ngwair r #akaCowobama

Jamani Ngwair , am in tears now ….. Jamani!. I can’t believe this. I can’t tweet The RIP….

Whyyyyy?

Mr II a.k.a Sugu

R.I.P ALBERT MANGWEA a.k.a NGWAIR...U R GONE TOO SOON MY NIGGA...



Lady Jay Dee

Ngwair ndio aliniandikia verse ya Rap, kwenye wimbo wa Jaffarai. Unaoitwa “Sio Kweli”

ASALAAM ALAYKUM, TANZANIA. IT’S JIDE ONCE AGAIN HEAR ME LOUD N CLEAR.........na maneno mengine yote yalioendelea.

I Wish i could turn back the hands of time.

Profesa Jay

PUMZIKA KWA AMANI KAMANDA Wangu Wanadamu tulikupenda sana ila MOLA amekupenda zaidi, Jina lake LIHIMIDIWE.. Tutakukumbuka daima #COWIIZZ”.

Diamond

DAH! bado nashindwa kuamini nnachokiskia na kukiona kwenye Media.

 Wasanii na watu mbalimbali wamekuwa wakiandika kwenye kurasa za kijamii kuhusiana na kifo hicho cha ghafla cha msanii huyo.

 Imeandaliwa na Harrieth Makwetta, Kalunde Jamal na Vicky Kimaro
MWANANCHI

Ndiyo mana hujisikia faraja kuiita Tanzania MAMA.


Wednesday, May 29, 2013

Zitto Kabwe amwandikia barua waziri mkuu wa Uingereza.

Dar/Dodoma. Waziri Kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia Chadema, amemwandikia barua Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron akimwomba kufuta sheria ya nchi yake inayowalinda watoroshaji wa fedha za umma wa nchi mbalimbali.

Zitto pia amemwomba Cameron kuzishawishi nchi nyingine tajiri kuwa na sheria za aina hiyo ili kudhibiti mafisadi wa nchi zinazoendelea.

Hatua hiyo ya Zitto, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema upande wa Tanzania Bara, ni mwendelezo wa juhudi zake za kupambana na mafisadi ndani ya Serikali wanaodaiwa kuweka katika benki za nje kiasi cha dola za Marekani milioni 196 (sawa na Sh323 bilioni).

Zitto amechukua hatua hiyo kwa kuzingatia kuwa Waziri Mkuu Cameron atakuwa mwenyeji wa Kundi la Nchi Tajiri Duniani linalojulikana kama G-8 ambalo litakutana Lough Erne, Uingereza kuanzia Juni 17–18. Cameron ndiye atakuwa Mwenyekiti wa mkutano huo.

Novemba mwaka jana, Mbunge huyo alipeleka hoja binafsi bungeni akitaka iundwe timu maalumu kwa ajili ya kufuatilia kiasi cha Sh 323 bilioni ambazo zimethibitika kufichwa Uswisi.

Zitto aliikabidhi barua hiyo Jumatatu ya wiki hii kwa Balozi wa Uingereza nchini Dianna Melrose, akimwomba aiwasilishe kwa Waziri Mkuu Cameron, kuelezea kilio cha Watanzania kuhusiana na fedha hizo.

Alisema sheria hiyo ina athari kubwa kwa maisha ya Watanzania wengi maskini na Afrika kwa ujumla, ambapo alisema anaamini sheria inayotaka uwazi itapitishwa kwenye mkutano wa mataifa manane tajiri yenye viwanda duniani, maarufu G-8, utakaofanyika mwezi ujao.

Akizungumzia suala hilo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema alisema kuwa ana taarifa kuhusu barua hiyo iliyoandikwa na Zitto kwenda kwa Cameron kuhusu shinikizo la Serikali kufanya mchakato wa kurudisha fedha zilizofichwa nje ya nchi.

“Tunafanya kazi na siyo kuzungumza ovyo kila mahali au kila hatua tuliyofikia, ila tunafanya kazi masaa yote, Watanzania wasubiri tu hatua tutakayofikia na tukiona tumejiridhisha tutawaambia nini kimefanyika,” aliongeza Werema.
MWANANCHI

TAIFA STARS YAANZA KUJINOA ADDIS ABABA

Mei 28, 2013
Taifa Stars imetua jijini Addis Ababa, Ethiopia leo (Mei 28 mwaka huu) alfajiri kwa ndege ya EgyptAir ambapo itaweka kambi ya wiki moja kujiandaa kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Morocco (Lions of the Atlas) itakayochezwa Juni 8 mwaka huu jijini Marrakech.

Stars iliyotua na kikosi cha wachezaji 21 imefikia hoteli ya Hilton, na imeanza mazoezi leo (Mei 28 mwaka huu) saa 12 jioni kwenye Uwanja wa Addis.

Kwa mujibu wa Kocha Kim Poulsen, Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itakuwa na vipindi (sessions) vinne vya mazoezi kabla ya kucheza mechi ya kirafiki na Sudan (Nile Crocodile). Mechi dhidi yan Sudan itachezwa Jumapili kuanzia saa 11 jioni kwenye Uwanja wa Addis.

Sudan ambayo pia imeweka kambi yake Addis Ababa kujiandaa kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia ilicheza mechi yake ya kwanza jana (Mei 27 mwaka huu) dhidi ya wenyeji Ethiopia na kulala mabao 2-0.

Wachezaji wanaounda Stars ni nahodha Juma Kaseja, nahodha msaidizi Aggrey Morris, Mwadini Ally, Ally Mustafa, Shomari Kapombe, Kevin Yondani, Erasto Nyoni, Haroub Nadir, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Khamis Mchana, Amri Kiemba, Salum Abubakar, Simon Msuva, John Bocco, Vicent Barnabas, Mudathiri Yahya, Athuman Idd, Haruni Chanongo na Zahoro Pazi.

Kikosi hicho kinatarajiwa kuondoka Addis Ababa kwenda Marrakech alfajiri ya Juni 3 mwaka huu kwa ndege ya EgyptAir. Stars itatua siku hiyo hiyo Casabalanca na kuunganisha moja kwa moja kwenda Marrakech.

 Boniface Wambura

Ofisa Habari

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Addis Ababa

+251 919910240

Muziki bila madawa inawezekana.

Taifa la muziki wa kizazi kipya nchini Tanzania limeondokewa na msanii mahiri wa bongofleva hasa katika upande wa mitindo huru 'free style' Albert Mangwea.

Nimeanza kumfahamu Mangwea akiwa amejipambanua katika sanaa kwa majina mengi ambayo alijipa kutokana na kipaji chake cha uimbaji. Binafsi nimeanza kumfahamu kwa kina baada ya kuimba wimbo wa 'Ghetto langu'. Naamini hata wengine walianza kumjua kwa kina kutokana na wimbo huo.

Ingawa alianza kuimba akiwa Dodoma na kundi lake la Chamber Squad mskani ya East Zuu, akiwa na kina Dark Master na Mez B, lakini kujulikana kwake kulianza baada ya wimbo huo.

Mpaka sasa watu wakiwa na vyumba vizuri utawasikia wakijisifia 'Ghetto langu zuri kama la Mangwea', hakuna shaka katika hilo kuwa wimbo ule ulimtoa vilivyo.

Baadaye aliimba vibao vingi ambavyo mpaka sasa vikipigwa kwenye radio lazima utikise kichwa, hasa 'Mikasi' alioshirikisha wasanii wakongwe chini ya mtayarishaji mahiri P Funk wa Bongo Record.

Mara baada ya kusikia kifo chake cha ghafla kilichotokea nchini Afrika Kusini jana, sikusumbuka sana yalikuja mawazo mengi lakini kubwa lililosumbua kichwa changu ni dawa za kulevya. Ingawa hakuna taarifa rasmi za daktari juu ya kifo chake lakini watu wa karibu wa marehemu wanaeleza alitumia dawa za kulevya kwa kiwango kikubwa kabla mauti hayajamfika.

Ingawa mauti yalimkuta usingizini lakini hilo la dawa za kulevya haliepukiki kwa maana tayari alishaingia katika kundi hilo baya, lakini mara kwa mara alikuwa akipinga taarifa hizo lakini waswahili husema 'mtu atakunyima chakula lakini hawezi kukunyima maneno' rafiki wa karibu wa Mangwea walikuwa wakisema wazi kukerwa na tabia ya ndugu yao kutumia dawa za kulevya.

Naandika haya si kwa kumdhalilisha marehemu, lakini ni kuonyesha wazi kuuungana na kampeni ya wasanii wa bongofleva iliyoanzishwa mwishoni mwa mwaka jana kuhusu matumizi ya dawa za kulevya. Yaani 'muziki bila madawa inawezekana'.

Nimefurahi kusikia baadhi ya wanamuziki kusogeza mbele matamasha yao ambayo mengi yalitakiwa kufanyika siku za hivi karibuni, lengo ni kuungana na ndugu pamoja na wanafamilia ya muziki nchini kuomboleza kifo cha ndugu yao.

Ipo haja kuchukua mifano hai ya matatizo ya dawa za kulevya, tayari msanii mwingine wa bongo fleva Rehema Chalamila 'Ray C' alisaidiwa matibabu na Rais Jakaya Kikwete, kuhusiana na dawa za kulevya.

Wapo baadhi ambao wanatajwa kuendelea na madawa miongoni mwao wakiwa ni TID, Loyd Eyez, Daz Baba na wengine ambao bado hawajajibainisha, lakini mficha maradhi kifo humuumbua.

Kwa pamoja tupige vita matumizi na uuzaji wa dawa za kulevya, kwa maana hakuna haja ya kusifia utajiri wa vijana wanaouza dawa za kulevya wakati vijana wengine wanaharibikiwa na kupoteza uhai wakati taifa bado linawahitaji.

MUZIKI BILA MADAWA INAWEZEKANA

HAFIDH KIDO
kidojembe@gmail.com
DAR ES SALAAM, TANZANIA
29, May 2013

Monday, May 27, 2013

Ziara ya mkuu wa magereza kutoka nchini Namibia.

 Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini Namibia, Kamishna Jenerali Evaristus Shikongo akiijaribu moja ya silaha inayotumika kwa ajili ya kutuliza ghasia wakati wowote inapotokea ndani na nje ya gereza.

 Askari wa Kikosi Maalum cha Kutuliza Ghasia Magerezani, wakimuonesha mbinu za kupambana na adui pasipo kutumia silaha Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini Namibia.

Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, Kamishna Jenerali John Minja (kushoto) na Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini Namibia, Kamishna Jenerali Evaristus Shikongo wakionyesha taarifa ya makubaliano waliyosaini.

Mkutano wa kujadili amani Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na wanahabari baada ya kuhudhuria Mkutano wa Kanda wa Usimamizi wa Amani, Usalama na Ushirikiano katika DRC na nchi za Maziwa Makuu katika makao makuu ya Umoja wa Afrika
Ibada ya kuwaombea waliotangulia kabla ya kuanza kikao.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akizingumza na Marais Wastaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Mzee Benjamin Mkapa na Waziri Mkuu Mstaafu na Katibu Mkuu wa Umoja wa Afrika Mstaafu Dkt Salim Ahmed Salim kuhusiana na sherehe za miaka 50 ya AU alipokutana nao jijini Addis Ababa, Ethiopia,
 Ndani ya jengo la Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa nchini Ethiopia, hii ndiyo taswira nzuri ya jengo hilo.


Wanafunzi kidato cha nne kupata mteremko....

Dar es Salaam. Idadi ya watahiniwa waliofaulu mtihani wa kidato cha nne mwaka jana imeongezeka kwa kati ya asilimia 20 na 23 baada ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), kufanya marekebisho alama za viwango vya ufaulu, Mwananchi limebaini.

Habari ambazo gazeti hili imezipata zinasema matokeo hayo ambayo yamewezesha kiwango cha ufaulu kupanda na kufikia asilimia kati ya 54 na 57, huenda yakatangazwa wiki hii pamoja na yale ya kidato cha sita ambayo pia yamechelewa kutangazwa.

Chanzo cha habari kutoka Necta kimesema matokeo hayo mapya yanaonyesha kuwa, ufaulu wa kuanzia daraja la kwanza hadi la nne umeongezeka kutoka asilimia 34.5 kwa matokeo yaliyotangazwa awali na huenda yakafikia asilimia 57. Hii inamaanisha kwamba watahiniwa wapatao 82,000 ambao awali walikuwa wamepata sifuri katika matokeo ya awali sasa wamepanda na kupata madaraja ya ufaulu katika matokeo mapya.

Kwa matokeo hayo, watahiniwa wa mwaka 2012 watakuwa wamefanya vizuri kuliko wa mwaka 2011, ambao watahiniwa 225,126 sawa na asilimia 53.37 ya 349,390 waliofanya mtihani huo walifaulu.

Msemaji wa Necta, John Nchimbi alisema upangaji wa matokeo hayo ulikuwa bado unaendelea. “Ninachojua kwa sasa ni kuwa mchakato unaendelea na matokeo yatatangazwa mapema tu ili watoto waweze kujiunga na shule mapema,” alisema Nchimbi.

Pia alisema usahihishaji wa mitihani ya kidato cha sita umekamilika.

Matokeo ya awali

Matokeo ya awali yaliyotangazwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa yalionyesha kuwa kati ya watahiniwa 367,756 waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana, waliokuwa wamefaulu kwa daraja la kwanza mpaka la tatu walikuwa 126,847 sawa na asilimia 6.4. Waliopata daraja la nne walikuwa ni 103,327 sawa na asilimia 28.1.

Katika matokeo hayo, watahiniwa 240,909 sawa na asilimia 65.5 walipata sifuri, hesabu ambayo imebadilika katika matokeo mapya ambayo yanaonyesha kuwa sasa waliopata daraja hilo ni 158,100 ambayo ni asilimia 43.

Hata hivyo, habari kutoka Necta zinasema kuwa licha ya kuwezesha kuongezeka kwa waliofaulu, matumizi ya kanuni mpya ya kukokotoa matokeo hayo yalisababisha zaidi ya wanafunzi 2,500 kushuka ufaulu ikilinganishwa na awali.

Maofisa mbalimbali wa Necta pamoja na wale wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na taasisi zake, walikutana mwishoni mwa wiki iliyopita kukubaliana masuala mbalimbali juu ya matokeo hayo pamoja na suala la matokeo ya wanafunzi hao 2,500 kabla ya kutangazwa wiki hii.

“Baada ya wajumbe kujadili suala lile, busara ilibidi itumike kwa hiyo hakuna mwanafunzi ambaye alama yake itashuka, kwa kawaida isingewezekana mtoto ambaye matokeo yalitoka akiwa amefaulu leo umwambie ameshuka,” kilieleza chanzo chetu.

Matokeo ya awali ndiyo chimbuko la kupitiwa upya baada ya wadau kuyalalamikia na kumlazimisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuunda tume ya kuyachunguza Februari 23, mwaka huu.

Kabla ya tume hiyo kuhitimisha shughuli zake, ilitoa taarifa ya awali ambayo ilipendekeza kufutwa kwa matokeo hayo kwa maelezo kwamba Necta ilitumia kanuni mpya ya kukokotoa matokeo bila kushauriana na wadau.

Serikali ilitoa taarifa bungeni kwamba imeamua kufuta matokeo ya 2012 na kuamuru yapangwe upya kwa kufuata madaraja yaliyotumika mwaka 2011.

Ratiba ya Bunge

Wakati hayo yakiendelea, ratiba ya vikao vya Bunge la bajeti imefanyiwa marekebisho na kusogeza mbele zamu ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambayo awali, ilikuwa imepangwa kusoma hotuba yake ya makadirio ya matumizi leo, badala yake nafasi hiyo imepewa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Wizara ya Elimu sasa imepangiwa kuwasilisha hotuba yake Juni 4 mwaka huu, hatua ambayo inatajwa kwamba lengo ni kusubiri kutangazwa kwa matokeo hayo ya kidato cha nne na kidato cha sita.

Wakati Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete alipokutana na wabunge wa chama chake Mei 19, mwaka huu mjini Dodoma, walisema hawako tayari kujadili hotuba ya wizara hiyo hadi matokeo ya kidato cha nne na sita yatakapotangazwa.

Katika mabadiliko hayo, hotuba ya Wizara ya Elimu imeondolewa kama ilivyotarajiwa na sasa italetwa bungeni Juni 3.

Taarifa zinaeleza kuwa, kusogezwa kwa hotuba hiyo kunatokana na mipango ya Serikali ambayo inatafuta namna na kukamilisha mchakato wa matokeo ya kidato cha nne ili kuipa mteremko hotuba ya Waziri wa Elimu, Shukuru Kawambwa bungeni.

Tofauti na mapumziko ya siku mbili za kawaida kwa wabunge, safari hii walipumzika siku moja baada ya Jumamosi kutumiwa kwa ajili ya kuhitimisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini ambayo iliahirishwa Alhamisi iliyopita kutokana na vurugu za Mtwara.

Ratiba ya awali inaonyesha kuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilikuwa isome hotuba yake ikifuatiwa na Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kabla ya kuhitimisha wiki kwa kusoma Makadirio ya Wizara ya Mambo ya Nje.

Wizara ya Elimu ilikuwa katika ‘mtihani’ kwenye Kikao cha 10 cha Bunge mapema Februari,  hasa baada ya Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia kuwasilisha hoja binafsi kuhusu udhaifu uliopo katika sekta ya elimu na zaidi ni kukosekana kwa mitalaa ya elimu.

Hatua hiyo ililazimisha Waziri wa Elimu, Shukuru Kawambwa kupewa muda kuwasilisha mtalaa huo na alifanya hivyo Februari 6, ukihusisha elimu ya chekechea, elimu ya msingi na sekondari kabla ya kupitishwa na Bunge.

Kamati ndogo iliundwa chini ya Magreth Sitta akiwemo Mbatia na wabunge wengine waliobobea katika masuala ya elimu kuangalia uhalali wake.

Hata hivyo, katika kile kinachoelezwa kuwa ni wasiwasi kwa Serikali kuhusu hofu ya vivuli vya wabunge wa upinzani, ratiba ilibadilishwa na kuisogeza mbele hotuba ya Wizara ya Elimu.

Ratiba mpya ya Bunge sasa inaonyesha kuwa, leo Bunge litapokea hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambayo itajadiliwa kwa siku mbili.

Hotuba hiyo pia haitegemei kuwa na mteremko kwani wabunge watakuwa na shauku ya kujadili kuhusu migogoro ya mipaka pamoja na masuala ya upimaji wa ardhi ili kuondoa kero za wakulima na wafugaji yakiwemo mashamba yanayomilikiwa bila kuendelezwa.

Baada ya hotuba hiyo yatafuata Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Wizara ya Kazi na Ajira na kufuatiwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Nchi kabla ya kuhitimishwa kwa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ambazo zote zitakuwa zikisomwa na kujadiliwa kwa siku moja.

MWANANCHI

Thursday, May 23, 2013

Hali bado tete vurugu za gesi Mtwara.


Waziri wa Nishati na Madini Prof Sospeter Muhojngo akijadiliana na baadhi ya Mawaziri na Wabunge mara baada ya kikao cha Bunge kuahirishwa jana ili kufuatilia vurugu za Mtwara.




Mtwara. Wakati mtu mwingine akiripotiwa kufa, hali bado ni tete katika Mji wa Mtwara kutokana na mabomu ya machozi na risasi za moto kuendelea kurindima kwenye mitaa kadhaa wakati polisi wakipambana na makundi ya vijana wanaopinga mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kwenda Dar es Salaam.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula, Mohamedi Kodi alithibitisha kupokea mwili wa mjamzito ukiwa na tundu tumboni, linaloaminika kuwa linatokana na risasi.

“Ni kweli kwa leo tumepokea maiti moja ya mwanamke ambaye ni mjamzito wa miezi saba akiwa amepigwa risasi tumboni,” alisema Dk Kodi. Inadaiwa kwamba mjamzito huyo ambaye jina lake halikufahamika, ameuawa akiwa nyumbani kwake. Kifo hicho ni cha pili baada ya Karim Shaibu (22), mkazi wa Chikongola kuuawa juzi.

Aidha, kuna taarifa ambazo hazijathibitishwa kuwa mtu mwingine ambaye jinsia yake haikujulikana aliuawa kwa bomu la machozi na mwili wake kutawanyika barabarani.

Kuhusu majeruhi, Dk Kodi alisema wamefikia watu 18... “Majeruhi wa mwisho tuliyempokea ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Chuno. Alikuwa amevunjwa miguu yote kwa risasi.”

Waomba hifadhi hospitalini

Umati wa watu wengi wao wakiwa kinamama na watoto umemiminika kwenye Hospitali ya Ligula kukimbia msako wa nyumba kwa nyumba unaofanywa na polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti, wakazi hao wamelalamikia kitendo cha polisi kuingia katika makazi yao, kuwapiga na kuwapora mali zao.

“Magomeni A hatuna amani, askari wanaingia nyumbani kwetu, wanatupiga na kutunyang’anya simu, yaani huku Magomeni hatuna amani kabisa, tumepotezana na watoto na hatujui hata waume zetu wako wapi,” alisema Paulina Idd.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa alisema hali ni shwari na kuwataka wananchi kuendelea na shughuli zao kama kawaida.

Hadi sasa huduma za kijamii zimesimama, hakuna maduka yaliyofunguliwa, hakuna usafiri wa daladala wala pikipiki, mji upo kimya huku sauti za milio ya mabomu na bunduki ikitawala, wanajeshi waliovalia sare wametapakaa sehemu mbalimbali za mji wakiwa katika magari na pikipiki.

Nchimbi atua Mtwara, jeshi lamwaga vifaa

Dk Nchimbi aliwasili jana jioni kwa helikopta na kukutana na viongozi wa Mkoa wa Mtwara walioongozwa na Mkuu wa Mkoa, Kanali Joseph Simbakalia kujadili suala hilo.

Pia ndege kubwa ya jeshi nayo ilitua huko na wanajeshi walikuwa wakipakua vitu mbalimbali vilivyoaminika kuwa vifaa.

Jeshi hilo limeombwa kuongeza kukabiliana na vurugu hizo ambazo zimesambaa sehemu mbalimbali za Mtwara.

Imeandikwa na Haika Kimaro, Mary Sanyiwa na Elias Msuya.
MWANANCHI

Mpenzi wa Dk Slaa ashinda kesi ya Talaka, yupo huru kuolewa sasa.

Dar es Salaam. Mpenzi wa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbroad Slaa, Josephine Mshumbusi ameshinda rufaa ya kupinga talaka yake, iliyofunguliwa na aliyekuwa mumewe wa ndoa, Aminiel Mahimbo.

Josephine kwa sasa amekuwa akiishi na Dk Slaa na tayari wamefanikiwa kupata mtoto mmoja, lakini harakati zao za kufunga ndoa zimekwama baada ya kupingwa na Mbunge wa Viti Maalumu wa Chadema, Rose Kamili akidai kuwa ana ndoa halali na Dk Slaa.

Mahimbo alikata rufaa hiyo katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, akipinga hukumu ya Mahakama ya Mwanzo Sinza iliyotoa talaka kwa Josephine dhidi yake, mwaka 2012.

Pamoja na mambo mengine, Mahimbo katika rufaa yake hiyo namba 32/2012, alikuwa akidai kuwa hapakuwa na ushahidi wa kutosha kiasi cha kuifanya Mahakama ya Mwanzo Sinza kutoa talaka hiyo.

Hata hivyo jana, Hakimu Aniseth Wambura aliyesikiliza rufaa hiyo, aliitupilia mbali ombi hilo akisema kuwa ameridhika na hukumu ya Mahakama ya Mwanzo Sinza kwamba kulikuwa na ushahidi wa kutosha kutoa talaka kwa Josephine.

Hakimu Wambura alisema katika hukumu hiyo,baada ya kupitia hoja za mrufani na za mjibu rufaa pamoja na mwenendo wa kesi ya msingi,amekubaliana na hukumu ya Mahakama ya Mwanzo Sinza kuwa ni sahihi.

Katika kesi ya msingi Josephine, alidai talaka kutoka kwa Mahimbo, pamoja na kudai kuwa Mahimbo hakuwa mwaminifu kwa kuwa alikuwa akitoka nje ya ndoa na kwamba alikuwa amemtelekeza bila kumpatia mahitaji na huduma za msingi, huku akimtesa.

Hakimu Wambura katika hukumu yake jana kwenye rufaa hiyo alisema, kutokana na sababu zilizotolewa na Josephine katika kesi ya msingi ni dhahiri kuwa hapakuwa na ndoa na kwamba mahakama haiwezi kuwalazimisha watu ambao hawapatani kuishi pamoja.

“Baada ya kusikiliza hoja za mrufani na mjibu rufaa ,mahakama hii imekubaliana hoja za mjibu rufaa (Josephine), kuwa kwa tabia ile mbaya na ukosefu wa uaminifu katika ndoa yake hapakuwapo na ndoa baina yao.”, alisema Hakimu Wambura.

“Hivyo mahakama hii inatangaza kuwa hukumu ya Mahakama ya Mwanzo Sinza ambayo iliivunja ndoa hiyo ilikuwa sahihi,” alisema kwa msisitizo Hakimu Wambura.

Wakili wa Josephine, Philemon Mutakyamilwa alisema kuwa amefurahishwa na hukumu hiyo akidai kuwa mahakama hiyo imetenda haki kwa mteja wake.

Licha ya kupangua kikwazo hicho, Josephine bado anakabiliwa na kikwazo kingine kilichomweka njia panda katika mipango yake ya kufunga ndoa na Dk Slaa.
Josephine na Dk Slaa walitarajia kufunga ndoa Julai 21, 2012, lakini imekwama baada ya Rose Kamili kufungua kesi Mahakama Kuu akiipinga kwa madai kuwa ana ndoa halali na Dk Slaa.

Pamoja na pingamizi hilo, Rose anamtaka Dk Slaa amlipe Sh50 milioni kama fidia ya kujihudumia pasipo matunzo ya mumewe huyo, huku pia akimtaka Josephine amlipe Sh500 milioni kama fidia ya maumivu aliyoyapata kutokana na kitendo chake cha kuingilia ndoa yake.

Kesi hiyo namba 4 ya mwaka 2012, inasikilizwa na Jaji Lawrance Kaduri, na itatajwa tena mahakamani hapo Julai 17, mwaka huu.
MWANANCHI

RIO FERDINAND AONGEZA MKATABA MAN U.


Mchezaji mkongwe wa Manchester United Rio Ferdinand ametia saini mkataba wa mwaka mmoja hivyo kusalia katika klabu hiyo kwa mwaka mmoja zaidi.
Shughuli hiyo iliyoidhinishwa na Meneja mpya David Moyes - imehitimisha wasiwasi ulikokuwepo kuhusu uwezekano wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 34 kutundika viatu vyake. 
Hivi majuzi Ferdinand alitangaza kustaafu kutoka timu ya taifa akidai alikuwa anataka kutumia muda wake mwingi kushughulikia timu yake ,Manchester United.
Ferdinand amesema: "nimefurahi. Imekuwa ni safari ya kufurahisha sana na natumai itaendelea kuwa hivyo."
Wakati akitangaza kuondoka kwake kama meneja wa Manchester United,Sir Alex Ferguson alisema Ferdinand amekuwa na wakati mzuri sana katika klabu hiyo na ataongezewa kandarasi.
Katika msimu uliomalizika mchezaji huo wa safu ya nyuma ameichezea Mashetani wekundu mara 34 kati ya mwaka 2012-13, hii ikijumuisha mechi 28 katika mechi za Ligi kuu ya Uingereza.
Ferdinand amesema : "nani hataki kukichezea klabu hiki tena mbele ya mashabiki 76,000 kila wiki?
"sasa naweza kujikita zaidi katika klabu yangu ambayo imeniweka vyema sana katika ile miaka ambayo nimekichezea.
Mchango wa Ferdinand katika timu ya Manchester United kulimfanya wakati mmoja kuchaguliwa na wenzake kuwa mchezaji bora zaid.
Mchezaji huyo wa zamani wa West Ham United na Leeds United ameichezea timu ya taifa ya Uingereza mara ,81 na alijiunga na Manchester United Julai 2002 kwa karibu £30m hivyo kuwa mchezaji wa ulinzi anayelipwa pesa nyingi zaidi duniani.
Kijumla Rio Ferdinand ameichezea Manchester United mara 432 na kushinda kombe la klabu bingwa bara ulaya mara moja na taji sita za ligi kuu ya Uingereza.
BBC SWAHILI

Wednesday, May 22, 2013

Ripoti ya kamati ya kuchunguza tuhuma za Rais wa Kenya yatoka..



Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na naibu wake wametajwa katika ripoti inayowahusisha na ghasia za baada ya uchaguzi katika ripoti iliyosubiriwa kwa muda mrefu kuhusu ukiukwaji wa haki za bindamau nchini humo.

Ripoti hiyo hata hivyo haikutoa mapendekezo ya hatua inazotaka kuchukuliwa dhidi ya Rais Kenyatta na naibu wake William Ruto.

Mwenyekiti wa tume hiyo, aliambia BBC kuwa ni kwa sababu wawili hao wanakabiliwa na kesi ya uhalifu dhidi ya binadamu katika mahakama ya kimataifa ya ICC.

Rais Kenyatta na bwana Ruto wanakana tuhuma hizo.

Tume ya maridhiano na haki ilikabidhiwa jukumu la kuchunguza visa vya ukiukwaji wa haki za binadamu vilivyofanywa tangu mwaka 1963 nchi hiyo ilipojipatia uhuru wake.

Iliundwa baada ya ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007/08 uliozua ghasia miaka mitano iliyopita kama njia ya kuleta maridhiano miongoni mwa wakenya.

Baada ya uchaguzi huo, watu 1,500 waliuawa na wengine zaidi ya 600,000 kulazimika kutoroka makwao.

Kenyatta na Ruto, waliokuwa mahasimu katika uchaguzi wa mwaka 2007, walishinda uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Machi baada ua kuungana chini ya muungano wa Jubilee.

Licha ya kuwa hakuna mapendekezo yaliyotolewa na tume hiyo dhidi ya Rais na naibu wake, inapendekeza uchunguzi zaidi dhidi ya maafisa wakuu waliotajwa kuhusika na ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 2007 na hata kufunguliwa mashtaka

Baadhi ya waliotajwa ni pamoja na waziri mpya wa madini Najib Balala na maseneta wawili.

Hata hivyo yume hiyo ilimtaka rais Kenyatta kuwaomba radhi wakenya kwa makosa waliyotendewa chini ya seri9kali zilizopita katika kipindi cha miezi sita tangu kukabidhiwa ripoti hiyo hapo jana.

Rais mstaafu Daniel Moi pia alitajwa katika ripoti hiyo akihusishwa na mauaji ya waliokuwa wanasiasa mashuhuri wakati wa utawala wake
BBC SWAHILI

Maoni na Mapendekezo ya CHADEMA juu ya Rasimu Muongozo uliotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuhusu Mabaraza ya Katiba ya Asasi, Taasisi na Makundi yenye mlengo yanayofanana

Wednesday, May 22, 2013


1.0. UTANGULIZI

Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83 (kifungu cha 18 (3)) imetoa wajibu kwa tume wa kuunda Mabaraza ya Katiba kwa ajili ya kupitia na kutoa maoni juu ya Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume.

Kifungu cha 17 (8) kinaeleza kuwa, isipokuwa kama mazingira yatahitaji vinginevyo, Tume itabuni utaratibu unaofanana ambao utatumika kila upande wa Muungano.

Kifungu cha 18 (6) kinaeleza aina nyingine ya Mabaraza ya Katiba kwa kueleza kuwa Tume inaweza kuruhusu Asasi, Taasisi au Makundi ya Watu kuwasilisha maoni yao kuhusu Rasimu ya Katiba.

Ikumbukwe kwamba Kamati Maalum ya CHADEMA ilikutana na Tume ya Mabadiliko ya Katiba tarehe 7 Januari 2013 kuwasilisha maoni ya CHADEMA kuhusu katiba mpya kama ilivyoalikwa lakini pia kutumia fursa hiyo kuwasilisha mapendekezo ya CHADEMA kuhusu marekebisho na maboresho yanayohitajika kuhusu mchakato wa mabadiliko ya katiba ili kupata katiba bora.

Tarehe 31 Januari 2013 Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilitoa taarifa kwamba imeamua kuwa Mabaraza ya Katiba yatakuwa katika makundi mawili yafuatayo: Mabaraza ambayo Tume itayasimamia na kukusanya Maoni (Mabaraza ya Katiba ya Wilaya – Ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa) na Mabaraza ambayo Tume haitayasimamia. Mabaraza hayo yatajisimamia yenyewe na kukusanya maoni yatakayowasilishwa kwenye Tume kwa mujibu wa maelekezo. (Mabaraza ya Katiba ya Asasi, Taasisi na Makundi ya Watu).

CHADEMA baada ya kupitia muongozo huo na kwa kuzingatia kuwa tayari tume ilishafanya uamuzi kuwa mabaraza ya katiba yatakuwa ya wilaya, tarehe 14 Februari 2013 kiliwasilisha maoni na mapendekezo yake kuhusu uteuzi wa wajumbe ambayo kwa sehemu kubwa hayakuzingatiwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na hivyo kusababisha matatizo makubwa katika mchakato mzima wa uteuzi wa mabaraza ya katiba ya wilaya.

Kufuatia hali hiyo katika Maoni ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu, tulitangaza kwamba CHADEMA itajitoa ushiriki wake katika mchakato wa Katiba Mpya endapo mambo yafuatayo hayatapatiwa ufumbuzi hadi kufikia tarehe 30 Aprili, 2013:

“Mosi; Kufutwa kwa uchaguzi wa wajumbe wa mabaraza ya wilaya ya Katiba uliofanywa na Kamati za Maendeleo za Kata, na badala yake wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya wachaguliwe moja kwa

moja na wananchi wa Kata husika bila kuchujwa na WDC;

Pili: Serikali ilete mbele ya Bunge hili tukufu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba yatayofanyia maeneo yafuatayo marekebisho.”

2.0 MAONI NA MAPENDEKEZO KUHUSU MWONGOZO WA MABARAZA YA ASASI, TAASISI NA MAKUNDI YENYE MALENGO YANAYOFANANA:

Bila kujali upungufu uliokuwepo katika uteuzi wa mabaraza ya katiba ya wilaya, Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetoa rasimu ya Mwongozo kuhusu Mabaraza ya Katiba ya Asasi, Taasisi na Makundi yenye malengo yanayofanana; hivyo, CHADEMA kinatoa maoni kuhusu rasimu hiyo kama ifuatavyo:

1. Uendeshaji (2.2) ; makundi yaliyotajwa ni yale yanayoanzia chini mpaka taifa na taifa: wakati ambapo kuna makundi ya ngazi ya chini pekee mathalani taasisi za jumuiya (CBOs), au taasisi iliyosajiliwa kwenye ngazi ya wilaya au hata mitandao ambayo haijasajiliwa, hivyo wigo upanuliwe kuruhusu makundi yote.

2. Utaratibu wa kutambua makundi (3.0); kipengele cha kutaka kuwasilishwe ‘taarifa ya kusudio’ kiondolewe, kinaongeza urasimu hasa kwa kuzingatia kwamba taarifa hizo zinawasilishwa tume makao makuu. Tume ikishatoa muongozo maana yake ni kwamba tayari imefungua mlango kwa makundi kujadili rasimu, hivyo ngazi pekee itayobaki iwe ni 4.0 ya kuwasilisha maoni. Hatua hii itachelewesha makundi ya kijamii kutumia haki na uhuru wako wa kikatiba wa kujumuika na kuwasilisha maoni.

3. Utaratibu wa kuwasilisha (4.0), maneno “Tarehe zitazoelekezwa na tume ya mabadiliko ya katiba” katika sentensi ya kwanza, kwa sababu inaweza kuleta tafsiri ya kwamba tume itayapangia tarehe za kukutana mabaraza hayo ya makundi ya kijamii ambayo kimsingi ni kuyaingilia. Tume ipange tu tarehe ya mwanzo wa kupokea maoni na mwisho wa kupokea maoni kwa awamu ya mabaraza. Tarehe ya kuanza uendeshaji imeshatajwa kwenye 2.2 “wakati wowote kuanzia tarehe itayotangazwa na tume”, tarehe ya mwisho wa kuwasilisha maoni imewekewa utaratibu kwenye 4.0 “ maoni yatawasilishwa kwa tarehe zitazoelekezwa na Tume”; hivyo sentensi hiyo ya kwanza haina haja ya kuwepo.

4. Uzito wa maoni (6.0), maelezo ya kwamba ‘maoni yatakuwa na uzito ulio sawa’, yanapaswa kufafanuliwa; kwa mantiki ya sentensi hii ni kwamba makundi yenye malengo yanayofanana hata yawe mengi kiasi gani yatakuwa na uzito sawa na mabaraza yatayosimamiwa na tume ambayo tayari yameshalalamikiwa kwamba yana hodhi ya chama kimoja na hayana uwakilishi wa moja kwa moja wa wananchi. Hivyo, tafsiri itolewe ambayo itahakikisha kwamba maoni ya wengi na matakwa ya umma yatatamalaki.



5. Tume kualikwa kusikiliza; Pamoja na kwa mujibu wa kipengele 2.2 mabaraza ya makundi yenye malengo yanayofanana ‘yatajisimamia na kujiendesha yenyewe’, pawepo na kipengele kwamba iwapo asasi, taasisi au kundi husika linaweza kuomba tume itume maafisa wake kuangalia/kusikiliza moja kwa moja ziada/zaidi ya utaratibu uliotajwa kwenye 4.0

3.0 MAONI NA MAPENDEKEZO JUU YA MASUALA MENGINE KUHUSU UENDESHAJI WA MABARAZA NA UTOAJI MAONI JUU YA RASIMU:



Aidha, pamoja na maoni kuhusu muongozo; CHADEMA kinatoa maoni ya ziada kwa Tume kuzingatia yafuatayo:

· Muongozo wa kwanza uliotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ulihusu “Muundo, utaratibu wa kuwapata wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya (Mamlaka za Serikali za Mitaa) na uendeshaji wake”.

Hata hivyo, muongozo uliotolewa ulijikita katika muundo wa mabaraza na mchakato wa uteuzi wa wajumbe wa mabaraza hayo, lakini haujatoa maelezo na maelekezo ya kutosha kuhusu namna mikutano ya mabaraza ya katiba ya wilaya itavyoendeshwa na utaratibu mzima utakaotumika kujadili rasimu ya katiba mpya katika mabaraza hayo.

Aidha, CHADEMA kinapendekeza kwa mara nyingine kwamba tume itoe muongozo mwingine mahususi kuhusu uendeshaji wa mabaraza ya katiba ikiwemo utaratibu utakaotumika wakati wa kujadili rasimu katika mabaraza; aidha kabla ya muongozo huo kuanza kutumika wananchi wapewe nafasi ya kutoa maoni na mapendekezo kama ilivyokuwa kwa muongozo huu kuhusu uteuzi wa wajumbe.

· Kwa kuwa mpaka awamu ya nne ya ukusanyaji maoni ya wananchi binafsi ilipokamilika wananchi waliotoa maoni kwa njia ya simu walikuwa 16,261 tu kati ya idadi ya wateja wa makampuni ya simu za mkononi ambao watajwa kuwa zaidi ya milioni 20 (mobile phone subscribers); Tume ya Mabadiliko ya Katiba iweke mfumo wa wananchi binafsi kuweza kutoa maoni kuhusu rasimu ya katiba kupitia simu za mkononi.

CHADEMA kinarudia kutoa mwito kwa tume kushirikiana na makampuni ya simu kuwezesha ujumbe wa simu ya mkononi kutumwa kwenye kila mtanzania mwenye simu kumpa dondoo juu ya rasimu ya katiba na kumpa namba anazoweza kutuma maoni kwa njia ya simu na pia maelekezo ya namna ya kutuma ujumbe wa bure wa maoni yake.

Hii itafanya wananchi wengi kuweza kushiriki kutoa maoni. Aidha, pawepo na uwazi katika mfumo mzima wa maoni yanayokusanywa kwa njia ya simu na mitandao mingine ili kusiwe na uwezekano wa "kuchakachua".

4.0 HITIMISHO:

Pamoja na kuwasilisha maoni na mapendekezo haya izingatiwe kuwa madai ya Kambi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA kuhusu kufutwa kwa chaguzi za mabaraza na kuwasilishwa bungeni kwa muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba katika mkutano wa kumi na moja wa Bunge unaoendelea hayajatimizwa.

Waziri Mkuu aliahidi (wakati wa kuhitimisha hoja ya Ofisi ya Waziri ) kwamba Serikali italeta Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kabla ya mwisho wa Mkutano huu wa Bajeti.

CHADEMA kinasubiri ahadi hiyo kutekelezwa katika kipindi hiki ambacho kitaenda sambamba na Tume kutoa Rasimu ya Kwanza ya Katiba Mpya kwa ajili ya kuanza kujadiliwa na Watanzania.

Endapo hadi kufikia mwisho wa kipindi hicho Serikali itakuwa haijaleta Muswada wa marekebisho yanayotakiwa; au endapo Muswada utakaoletwa hautakidhi matakwa ya kuboresha mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya; basi CHADEMA itawaalika wanachama, wafuasi na mashabiki wake Tanzania nzima, pamoja na taasisi za kiraia na za kidini, vyama vya siasa na Watanzania wote wenye nia njema na taifa hili kuhamasisha umma kuikataa Rasimu ya Katiba Mpya kwenye kura ya maoni itakayofanyika kwa ajili ya kuihalalisha Katiba hiyo mbovu.

Naomba kuwasilisha,

John Mnyika (Mb)

Kny. Katibu Mkuu

JK atoa tamko vurugu za Mtwara....


Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete amewaonya watu wanaosababisha uvunjifu wa amani nchini humo kuwa watakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Taarifa zinazohusiana

Onyo hilo linafuatia ghasia ambapo ofisi kadha, maduka na nyumba zimechomwa katika mkoa wa Mtwara ulioko kusini mashariki mwa Tanzania leo.

Akihutubia kupitia televisheni ya taifa, TBC1, Rais Kikwete amesema wale waliokamatwa na polisi wakati wa ghasia hizo watashitakiwa.

Ghasia hizo zilianza muda mfupi baada ya Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo kuwasilisha bajeti ya wizara yake bungeni. Akizungumzia madai ya waandamanaji hao, Rais Kikwete amesisitiza kuwa raslimali za nchi ni mali ya taifa zima.

Amesema mkoa wa Mtwara haujatelekezwa na kusema kwamba kuna mipango ya kutumia gesi hiyo kujenga viwanda vya mbolea na kutumia gesi hiyo asilia kuzalisha nishati ya umeme kwa mikoa ya Mtwara, Lindi, na Ruvuma ili kuunganishwa katika gridi ya taifa.
Ofisi zachomwa

Kwa mujibu wa mkuu wa polisi wa mkoa wa Mtwara kamanda Linus Sinzumwa, vurugu hizo zimetokea asubuhi ya leo mara baada ya Wizara ya Madini na Nishati kusoma bajeti yake ya makadirio ya mapato na matumizi huko Bungeni mjini Dodoma na kusababisha uharibifu wa mali.

Ametaja uharibifu huo kuwa ni pamoja na kuchomwa kwa majengo ya serikali kama mahakama, nyumba za watendaji wa serikali, baadhi ya majengo ya chama tawala na nyumba za watu binafsi.

Polisi wawasaka waandamanaji Mtwara

Hata hivyo, kamanda huyo, amekanusha taarifa za kuuawa kwa mtu mmoja katika eneo hilo na kubomolewa kwa daraja linalounganisha mji wa Mtwara na maeneo mengine.

Kamanda Sinzumwa amesema watu wapatao tisini na mmoja wanashikiliwa na jeshi na polisi kuhusiana na matukio mbalimbali ya ghasia hizo.

Ghasia hizo, zinahusishwa na madai ya muda mrefu sasa ya wananchi wa mkoa huo kupinga ujenzi wa bomba la gesi iliyogunduliwa mkoani humo kusafirishwa hadi Dar es Salaam, kaskazini mwa Mkoa wa Mtwara, kwa ajili ya kuzalisha nishati ya umeme.

Hii ni mara ya pili mkoani Mtwara kutokea kwa ghasia zinazohusisha maafa kwa binadamu na uharibifu wa mali kama ilivyotokea mapema mwaka huu.
KIDOJEMBE

Tukio la kigaidi London.


Mtu mmoja ameuwawa katika shambulio la mapanga na washukiwa wawili wamepigwa risasi na polisi katika mtaa wa Woolwich, kusini mashariki ya London.

Waziri Mkuu David Cameron amesema kuna ishara nzito kua ni tukio la kigaidi na Uingereza haitaterereka wakati inakabiliwa na mashambulio kama hayo.

Picha za video zimejitokeza zikimuonyesha mtu akipunga panga la kuchinja nyama na kutoa matamshi ya kisiasa.

Akisema " Lazima tupigane nao kama wanavyopigana nasi. Jicho kwa jicho,jino kwa jino".

Taarifa zizisothibitishwa zaeleza mtu aliyeuwawa alikuwa mwanajeshi katika kambi ya kijeshi ya Woolwich.

Makao ya waziri mkuu yamesema Bwana Cameron ambae alipanga kulala mjini Paris baada ya kukutana na Rais wa Ufaransa anarejea Uingereza.

Waziri wa mambo ya ndani Theresa May aliita mkutano wa kamati ya dharura ya usalama , Cobra.

Watu wote wawili waliopigwa risasi na polisi walipelekwa hospitali na mmoja anasemekana kua katika hali mbaya.

Mtu mmoja aliyeshuhudia tukio hilo alisema watu hao wawili walimshambulia mtu mmoja mwenye umri wa miaka 20 ambae alikua amevalia fulana iliyokua na maandishi ya wakfu wa kuwasaidia wanajeshi uitwao Help for Heroes.Msaada kwa mashujaa.
BBC SWAHILI

VURUGU MTWARA BAADA YA SERIKALI TAMKO LA SERIKALI KUHUSU GESI




Huko MIKINDANI ofisi zote za serikali zavamiwa na kuchomwa na mpaka daraja la Mikindani nalo limevunjwa kwa maana hauwezi kutoka wala kuingia MTWARA

Kuna madai kwamba silaha zimeibiwa (Haijathibitishwa)

Maaskari wanafanya msako wa nyumba hadi nyumba maeneo ya Magomeni na Mangowela

Askari achomwa mshale. Haijulikani hali yake

Ni mapambano baina ya vijana na maaskari. Vijana hawaogopi tena risasi wala mabomu .

Kundi limeelekea Shangani kwenye nyumba za vigogo.

 Nyumba ya kupumzikia wageni inayoitwa Shengena Lodge imechomwa moto kwa kile kinachoelezwa kwamba iliwapokea askari Polisi.

Ofisi ya CCM saba saba imechomwa moto, na baadhi ya waandishi wamezingirwa maeneo ya Sokoni, sasa ni milio ya risasi na mabomu.

Matairi  kila  kona  ya mji  yamechomwa  barabarani  polisi  na  zimamoto   wanafanya kazi ya kuzima na kufukuza wananchi. Kauli mbiu "Gesi haitoki hata kwa bomba la peni"

Kambi ya Upinzani yaukataa mpango wa serikali wa ujenzi wa bomba la gesi

Nyumba kadhaa  za watumishi  wa Serikali  zimechomwa  maeneo ya Shangani.(habari haijathibitishwa rasmi)

Ni magari ya FFU tu ndio yapo barabarani nayo hupata wakati mgumu kupita kwasababu ya mawe na magogo yaliyowekwa na vijana,baadhi ya watu kadhaa wamechukuliwa na askari eti kwakuwa walipita jirani na gari yao,askari wengi waliokuja si wa hapa Mtwara wengi wametoka Masasi na Lindi. Ving'ora vinalia ovyo ovyo.

watoto wamefungiwa mashuleni walimu wamekimbia

Vituo vya Redio vya Mtwara havizungumzii hali hii ya hatari. Vinapiga Muziki pengine vinakusanya matukio na habari ya majanga haya. Ili Wananchi wayapate .

 Mabomu yanapigwa mfululizo maeneo ya Magomeni-Mtwara . Takriban mabomu 20 na ushee mpaka sasa. Na wanaendelea kupiga mabomu.

Sasa hali si shwari kila eneo, wakionekana watu watatu wanaongea maongezi maaskari wanapiga mabomu. Mabavu yamechukua mkondo wake. Wananchi wamejifungia majumbani mwao. Chuki dhidi ya Polisi yaimarika. Polisi wanapiga mabomu bila mwelekeo.

Magomeni na sokoni kimenuka, mabomu yanarushwa na wananchi wanakimbia ovyo.

Kituo  kimoja  cha habari  kinachorusha habari za bunge chazuia mawimbi yake kwa Mkoa wa Mtwara hivyo hakisikiki(Redio na TV). Na kimewanyima haki wananchi wa Mtwara ya kupata taarifa.(Hatimaye wamerejesha matangazo yao)

Waziri wa Nishati amesoma hotuba yake kwa hisia kali na mbwembwe. Mwishoni amesema bomba la gesi linajengwa kutoka Mtwara kwenda Dar.


Maduka yote yamefungwa, baa zimefungwa, hakuna huduma za usafiri, ofisi za serikali zimepwaya kimsingi hakuna lolote linalofanyika

Boda boda zinazoonekana maeneo ya Nkanaledi na abiria zinapigwa mawe.

Makachero nao wanajifanya madereva wa boda boda na Bajaji, Tax wengine wanatembea na magari ya Serikali.
Chanzo: WANABIDII.

MWAMUZI WA AFRIKA KUSINI KUICHEZESHA STARS MOROCCO


                                                         Ofisa Habari TFF Boniface Wambura.

Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limemteua mwamuzi kutoka Afrika Kusini kuchezesha mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika kati ya Tanzania (Taifa Stars) na wenyeji Morocco (Lions of the Atlas).



Mechi hiyo ya kundi C itachezwa Juni 8 mwaka huu jijini Marrakech, Morocco kwenye Uwanja wa Grand kuanzia saa 3 kamili usiku kwa saa za Morocco. Mwamuzi atakayechezesha mechi hiyo ni Fraser Daniel Bennett.



Bennett atasaidiwa na Thusi Zakhele Siwela pia wa Afrika Kusini, wakati mwamuzi msaidizi namba mbili atakuwa ni Marwa Range kutoka Kenya. Mwamuzi wa akiba (fourth official) ni Lwandile Mfiki wa Afrika Kusini.



Kamishna wa mechi hiyo ni Robert Mangollo-M’voulou wa Gabon wakati mtathimini wa waamuzi (referee assessor) ni Charles Masembe kutoka Uganda.



Taifa Stars ambayo iko chini ya Kocha Kim Poulsen, na ikidhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager tayari iko kambini katika hoteli ya Tansoma ikiendelea kujinoa kwa ajili ya mechi hiyo ambapo kabla itajipima na Sudan (Nile Crocodiles) Juni 2 mwaka huu jijini Addis Ababa, Ethiopia.



Ratiba ya mazoezi kwa timu hiyo ni kama ifuatavyo;



Mei 22                 Saa 10 jioni                             Uwanja wa Karume

Mei 23                 Saa 1 asubuhi na Saa 10 jioni   Uwanja wa Karume

Mei 23                 Saa 10 jioni                             Uwanja wa Karume





Mei 25                 Saa 1 asubuhi na Saa 10 jioni     Uwanja wa Karume

Mei 26                 Saa 3 asubuhi                            Uwanja wa Karume

 Boniface Wambura

Ofisa Habari

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Tuesday, May 21, 2013

Mourinho njia nyeupe kurudi Chelsea.

Klabu ya Real Madrid imethibitisha kuwa kocha wa timu hiyo Jose Mourinho ataondoka kwenye kibarua cha kuifundisha timu hiyo mwishoni mwa msimu.

Rais wa klabu ya Real Madrid,Florentino Perez amewaambia waandishi wa habari jumatatu jioni kuwa Mourinho hatofukuzwa bali wamekubaliana kumaliza mkataba wao na kocha huyo raia wa Ureno.

Aidha Madrid, imeongeza kuwa haijaanza mazungumzo na kocha yeyote kwaajili ya kuchukua nafasi ya Mourinho lakini vyanzo mbalimbali vya habari za michezo zinamtaja kocha wa PSG ya Ufaransa, Carlo Ancelloti kuchukua jukumu la kuifundisha Madrid msimu ujao.

Duru za kimichezo zinasema, Jose Mourinho huenda akarejea nchini Uingereza kuifundisha klabu yake ya zamani ya Chelsea baada ya kuwepo makubaliano baina yake na uongozi wa klabu hiyo.

Wakati Real Madrid ikitangaza kuwa inamtaka Kocha Carlo Ancelotti timu yake ya Paris St-Germain ya Ufaransa imesema haiwezekani yeye kuhama.

Wiki iliyopita maombi ya klabu hicho cha Uhispania yalikataliwa na mabingwa hao wapya wa Ufaransa.
Taarifa zinazohusiana.
                                                                         Carlo Ancelotti

Sasa Ancelotti mwenyewe ametangaza kuwa anataka kuondoa Ufaransa na kuijunga na Real Madrid

"nimewaomba kuondoka na hadi sasa bado nasubiri jubu lao," Ancelotti, wenye umri wa miaka 53 amesema.

Lakini Rais wa PSG Nasser al-Khelaifi mwenye makao yake Qatari amesema: " ameomba kuondoka na kujiunga na Real Madrid , hii haiwezekani kwa sababu kwa muujibu wakandarasi yake bado amesalia na mwaka mmoja, kwa hiyo huo ndio uamuzi wetu".

Akizungumza na kituo kimoja cha Televisheni cha Qatari rais huyo amesema : " hiyo ni shauri yake; sio tatizo letu . Mbali na mwaka mmoja uliosalia tumetangaza kumuongezea mwaka mmoja zaidi . Ukiwa na mkataba unapaswa kuuheshimu".

Hadi sasa Jose Mourinho ni Meneja wa Real Madrid inagawa imetangazwa kwamba anarudi Chelsea msimu ujao.

Wakati huohuo kocha mkuu wa Tottenham Andre Villas-Boas amesema ikiwa klabu hiyo inataka kufanya vyema msimu ujao basi lazima wamuhifadhi mchezaji Gareth Bale.

Spurs iliteleza kuingia katika michuano ya Klabu Bingwa bara Ulaya katika michuano ya siku ya mwisho wa Ligi kuu ya Uingereza baada ya Arsenal kuwafunga Newcastle 1-0 hivyo kumaliza ligi wakiwa alama moja juu ya Tottenham.

Kuna hofu kuwa mshambulizi huyo mwenye umri wa miaka 23 huenda akahama kutokana na Spurs kushindwa kufunzi katika mashindano hayo ya bara Ulaya.

Lakini Villas-Boas amesema: "ikiwa tunataka kufaunye vizuri zaidi msimu ujao nilazima tushikilie hazina yetu na hilo ndilo nimekuwa nikifahamishwa tangu awali".

Bale, ambaye anadaiwa kunyemelewa na timu kadhaa maarufu miongoni mwao Real Madrid aliifungua Spurs bao lao la ushindi dhidi ya Sunderland siku ya mwisho wa Ligi kuu ya Uingereza.

Licha ya ushindi huo bado Spurs ilimaliza katika nafasi ya tano, ikiuwa nyuma ya Arsenal.

Villas-Boas amesisitiza kuwa msimu ujao timu yake itafufuka na kuwa katika nafasi bora zaidi ya kufuzu katika michuano ya Klabu bingwa bara ulaya.
BBC SWAHILI