Wednesday, May 1, 2013

CHIMBUKO LA VYAMA VYA WAFANYAKAZI DUNIANI NA HAJA YA MSHIKAMANO. JK Nyerere.




Hotuba hii ilitolewa mwaka 1995 na hayati baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere katika sikukuu ya wafanyakazi iliyofanyika kitaifa mjini Mbeya. Hotuba hii maarufu ya ‘Tumetoka wapi, tupo wapi na tunakwenda wapi’ ililenga kumwamsha kutoka usingizini mfanyakazi wa Tanzaniana Afrika kwa ujumla.

Nimeamua kuirudia nusu wakuwa historia imejirudia mwaka huu pia maadhimisho ya sikukuu hiyo kitaifa yanafanyika Mbeya, tena katika kipengele muhimu cha historia ya vyama vya wafanyakazi duniani, lengo ni kujikumbusha malengo na nia ya wafanyakazi wa miaka iliyopita kufikiria kuanzisha umoja wao ili kuwasaidia wanyonge kutoa mawazo yao kwa njia za siri na dhahiri.

Mwalimu Nyerere alianza kuelezea chimbuko la vyama vya wafanyakazi kwa kusema; Wazo la kuwa na vyama vya wafanyakazi duniani, kwamba wawe na mshikamano na umoja wa kutetea maslahi yao sio wazo la Tanzania wala la nchi zilizoendelea. Kusema kweli, kwa historia, lilianza huko Marekani na lilikubalika. 

Wafanyakazi wa wakati huo, katika nchi ambazo maendeleo yake yalikuwa mazuri, waliamua wafanye mshikamano wa kuleta maendeleo yao na hasa ya kupambana na waajiri wao.

Mwajiri anaanzisha shughuli yake na anafanya kwa nguvu zake mwenyewe. Anataka kulima na analima kwa nguvu zake mwenyewe. Kama anataka kufungua kiwanda chake cha mbao, maana ninyi ni wafanyakazi inapasa nizungumzie habari ya viwanda badala ya kilimo, anafungua kiwanda chake cha kutengeneza samani. Anaweza kutumia vitu vyake mwenyewe na akawa anafanya kazi na seremala mmoja. Atakuwa amepata randa, meza, patasi na kila kitu chake. 

Anafanya kazi yake mwenyewe, anatengeneza vitu vyake, anauza na anapata hicho anachokipata. Hicho anachokipata kinatokana na nguvu yake mwenyewe. Anataka mbao na anatengeneza. Mtu anamwendea na kumwambia, “mimi nataka meza bwana”, anamtengenezea. 

Inabidi mwenyewe ashughulike na meza hii mpaka inakuwa nzuri. Anapata kile anachopata. Nyingine anafidia zile gharama zake za meza, randa na za vyombo vingine vyote hivyo. Halafu, kinachobaki cho chote, ndiyo maslahi yake. Lakini, kile anachopata kinatokana na jasho lake mwenyewe. Akitoka hapo, anaweza kuwa mshiriki na mwenzake, washirikiane wote wawili na sio kwamba mmoja atamwajiri mwingine. Hapana! Wote wawili watafanya kazi kwa pamoja. Watasaidiana vizuri zaidi wakifanya pamoja. Wao, vile vile, wanaweza wakapata maslahi kutokana na nguvu zao wenyewe. 

Mwanzo wa dhuluma ya unyonyaji:

Wakitoka hapo nao wakajifanya ni waajiri wanaotaka kuwaajiri wengine, shughuli ile si ya hawa walioajiriwa tena. Ni ya hawa wawili tu. Wakisha kuwaingiza wengine, hao si yao. Wanasema. Sasa njoo hapa tusaidie kutengeneza meza, vitanda, madirisha na milango. Lakini, meza inapokuwa imekwisha, tunaiuza. Si mali yenu ninyi wafanyakazi. Ni mali yetu. Ninyi chenu humu ni ule mshahara na wala sio faida itakayopatikana humu.

Faida, ‘baada ya kutoa gharama zote za ununuzi wa mbao, usafirishaji wa mbao zote zile pamoja na gharama za kuwaajiri ninyi mwitoe meza hii - kwa kuwa mishahara yenu ni sehemu ya gharama’ nikitoa gharama zote hizi, kinachobakia ni changu. 

Sasa ile inayobaki, baada ya kutoa gharama hizo, inaweza kuwa kubwa na inaweza kuwa ndogo. Inategemea sana gharama zilikuwaje. Kama gharama za kununulia mbao zilikuwa kubwa, zinanipunguzia faida yangu. Kama gharama za wafanyakazi ni kubwa mishahara ya wafanyakazi kama ilikuwa mikubwa, inanipunguzia faida yangu. Kwa hiyo, sipendi vyote viwili. Sipendi muuza mbao aniuzie aghali na sipendi mfanyakazi adai mshahara mkubwa. Napenda wote waniuzie rahisi. Nataka mbao kiurahisi, nataka mishahara iwe chini. Hapo ndipo ninapopata faida kiuchumi. 

Hili sijambo la ajabu la wazungu wenzetu wanaojua bali ni la kila mtu mwenye akili kama zenu kutokana na mtiririko wa mantiki wa hoja yenyewe. Kwamba, mimi nataka mshahara wenu uwe mdogo kwa kuwa faida yangu inatokana na mshahara wenu kuwa mdogo. Sasa ninyi mtasema: ALAA Bwana Mkubwa, kazi tufanye sisi halafu wewe utupe mshahara mdogo. Tukufanyie kazi wewe? Basi uone iwapo tutakufanyia. 

Umoja na mshikamano ndio silaha ya kupambana na dhuluma ya unyonyaji, Kama watakuwa wananiambia mmoja mmoja, nitawafukuza. Unakuja peke yako na unaniambia ‘Lakini Mzee sasa mimi nataka uniongeze mshahara.’ Nitakuambia. Unaniambia nini wewe? Unasema nikupe mshahara wa shilingi ngapi? Utajibu. ‘Ah, kama utakavyoona, lakini uniongeze. Mungu anaona na Mtume.’ Nikaona kidomodomo chake huyu Nikamuambia: Unataka mshahara huo ninaokupa sasa hivi? Nyamaza na nenda kafanye kazi huku utachagua. Kama hutaki, toka. Kazi sikukuomba. Ulikuja mwenyewe. 

Nitakutisha hivyo. Ukifikiri mchezo, nitakufukuza. Na wenzako watajua kafukuzwa kwa nini yule. Amedai mshahara mwingi. Mimi kimya! Wengine hawatathubutu tena maana watafikiri. Nikisemasema hapa na mimi nitatimuliwa na watoto wana njaa. Nikitimuliwa nitapata taabu. Wewe unaonaje?

Anaendelea huyu kukunyanyasa. Kama anaweza kuwanyonya wauza mbao na kukunyonya wewe mfanyakazi, atawanyonyeni wote mpaka wauza mbao washirikiane kwa pamoja wapate bei nzuri. Mpaka wafanyakazi washirikiane kwa pamoja wapate mishahara mizuri. Bila kushirikiana, hawapati mishahara mizuri. 

Hii ndiyo asili ya kuanzisha Vyama vya Wafanyakazi. Nasema hamkuvianzisha ninyi vilianzishwa zamani, tena Marekani. Lakini, Marekani havikuwa na nguvu sana. Vilikuwa na nguvu zaidi Ulaya. Hata hivyo, havina nguvu sana tena Ulaya. Sitaki kuingilia na kuliendeleza hili kwa kuwa viongozi wenu kama wanaelewa, watawaelezeni.

 Zamani, Vyama vya Wafanyakazi vilianzisha mshikamano wa Wafanyakazi Duniani. Kauli mbiu yake ilikuwa ‘Wafanyakazi Duniani Unganeni. Hamna cha Kupoteza isipokuwa minyororo yenu.’ Mantiki ya kauli mbiu hiyo ilikuwa kwamba, kwa kuwa mmefungwa minyororo na mmenyonywa unganeni. Huo ulikuwa ndio ujumbe wa kauli mbiu hiyo kwa Wafanyakazi Dunia nzima. Hata hivyo, sisi hatukuwapo. 

TUMETOKA WAPI?
Azimio la Arusha na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.

Tukaweka kitu kimoja hapa kinaitwa Azimio la Arusha. Leo narudia kusoma Azimio la Arusha hata kama hamlitaki. Kama kuna watu Tanzania hawajali, wachukue waanze kulisoma ili waone na waniambie wanachokiona mle kibaya ni nini hasa. Asome tu kwa dhati tu na kisha aseme hiki ni kibaya.

Siasa ya Ujamaa.

Linasema Azimio la Arusha, kwa msingi kabisa, kwamba “Nchi yetu ni ya Wakulima na WafaƱyakazi”. Sasa mnasemaje? Imeacha kuwa ni nchi ya Wakulima na Wafanyakazi? Kwa hiyo, kama tunaijenga nchi hii, tunaijenga kwa faida ya Wakulima na Wafanyakazi. Ndivyo Azimio Ia Arusha linavyosema. Ukweli huo umekwisha? Umefutika? Umefutwa na nani? Nini kimefuta ukweli huo kwamba nchi hii ni ya Wakulima na Wafanyakazi? Ninyi hapa ni Wakulima na Wafanyakazi.

Mtaona wafanyabiashara wadogo wadogo, siku hizi wengine wanaitwa Wamachinga. Lakini, hasa hasa, nchi hii bado ni nchi ya Wakulima na Wafanyakazi. Kama tutafanya jitihada za kuijenga nchi hii, tutajenga uchumi wake na huduma zake za umma ambazo lazima ziwafae Wakulima na Wafanyakazi. Hali hiyo imebadilika lini? 

Siasa va Kujitegemea.

Tukasema kwamba “Hatuna budi kujenga nchi hii kwa kujitegemea”. Hatuwezi kuwa tunataka maslahi yetu ya Watanzania ya afya bora, maisha bora na elimu nzuri lakini eti tudhani tunaye mjomba huko nje atakuja kutuletea maslahi hayo.

HATUNA! Tutajenga nchi hii kwa faida yetu wenyewe sisi wenyewe. Akipatikana mtu kutusaidia, tutamshukuru. Lakini kazi ya kujenga nchi hii kwa manufaa ya Watanzania wote ni kazi ya Watanzania, si kazi ya mtu mwingine. Msimamo huo tukauita Siasa ya Kujitegemea. 

Msingi huo umekufa. Hivi mmeshapata mjomba? Hivi kweli mtawadanganya Wafanyakazi hawa msiwambie “chapeni kazi kama mnataka maslahi yenu yaboreshwe, tuchape kazi kwa faida yetu!” Tuache kuwambia wakulima kwamba “kama tunataka maendeleo, tuchape kazi hivyo hivyo”. Hivi mtawaambia hawa kwamba “tumeshapata mjomba msiwe na wasiwasi!” Mjomba huyo ni nani? Mimi nitafurahi kumwona. Nitakwenda kumwona, lakini sitamwuliza lo lote. Nitafurahi kumwona. Halafu mkinionyesha, “ndiye huyu mjomba”, nitacheeka!! Hali ya nchi hii haijabadilika hata kidogo. Tanaweza kujenga nchi kwa maslahi ya Watanzania kwa siasa ya kujitegemea tu, lakini kwa manufaa ya wote. Manufaa ya wote ndicho tulichokiita ujamaa. 

Nchi ya Kijamaa.

“Nchi ya Ujamaa”, tukasema, “ni nchi ambako kila mtu anafanya kazi. Kama ni mkulima, anafanya kazi; kama ni mfanyakazi, anafanya kazi”. Lililokuwa la msingi na linalotawala ni mfanyakazi: maslahi yanatokana na kazi yake na jasho lake. Watu ambao hawana ulazima, kimsingi ya kupata maslahi yao kutokana na jasho lao wenyewe wapo.

Watoto wadogo hawana jukumu hilo. Eti chakula chao kitokane na nguvu zao wenyewe? Hao ni wanyonyaji wa haki sawa kwani wanawanyonya mama zao. Ni haki yao. Lakini zee na madevu yake hatulitazamii limnyonye mama yake. Watoto wadogo tu wanayo haki hiyo. Vile vile, kuna watu ambao hawana uwezo wowote ule wa kujifanyia kazi- sio uwezo wa kutokuwa na kazi!

Wako watu hawawezi. Wana vilema fulani ambao hawawezi kufanya kazi wajipatie riziki kwa kazi na kwa nguvu zao wenyewe. Hawa wana haki ya kulishwa na kutunzwa na umma pamoja na jumuiya zote. Hali kadhalika, wako watu wazima ambao wamefanya kazi zao. Walipofika umri wao wa kushindwa, hawawezi kufanya kazi tena. Ah, basi tena. Hawajiwezi hawa, tuwatunze. Hawa ni haki kuwatunza. Wamo watu wa aina hiyo wanajulikana kila mahala. 

Nchi ya Kibepari
Hata hivyo, mbali ya makundi hayo, wapo watu wengine ambao wanapata riziki yao kwa kufanya kazi na wengine wanapata riziki yao kwa kafanyiwa kazi.

Nasema nchi ya namna hiyo inaitwa ya kibepari. Nchi inakubali wengine wafanye kazi na kupata riziki yao kwa jasho kama inavyosema misahafu, wengine wanafanya kazi kwa kunyonya kama watoto wadogo kama vile vilema na vizee. Ni majitu yanakaa na uwezo wao yanatumia wengine kama vyombo. Kwa hiyo, mfanyakazi na randa ni sawa sawa. Nasema nchi ya namna hiyo inaitwa ni nchi ya kibepari. Sasa katika dunia ya siku hizi maneno hayo si mazuri sana kuyasema.

Na mimi nawakumbusheni tu na wala sijayasema! Mimi sina taabu, nawakumbusheni tu. Hili Azimio la Arusha, ambalo sasa mnalitemea mate, lilikuwa linasema hivyo na, kutokana nalo, kuna mambo fulani tukaanza kuyapata.


Kujenga uƧhumi wa viwanda
Tukaanza shughuli ya kujenga uchumi wetu. Natumaini nitazungumzia hili la viwanda. Nchi zinazoendelea duniani ‘kama Marekani ya Kaskazini, Marekani yenyewe na Kanada, Ulaya, hasa Ulaya Magharibi na Japani’ na maana moja ya kuendelea ni kwamba uchumi wake unategemea viwanda. Viwanda ndivyo vinatengeneza vipaza sauti, kamera zetu tunazotumia sasa nakadhalika. 

Maana ya maendeleo ya leo ya uchumi wenye nguvu ni maendeleo ya viwanda. Nchi yenye viwanda tunasema ni nchi iliyoendelea. Hata hivyo, tuna maana nyingine ya nchi zilizoendelea ya kuziita ni nchi zenye viwanda. Nchi haiwezi kuendelea bila kuwa na viwanda vya kisasa. 

Wakati tunajitawala, hatukuwa na viwanda. Tulikuwa tunalima kahawa, mkonge na pamba, lakini tunauza vyote nje. Mimi najua kidogo historia ya Uingereza, ilikuwa ndiyo nchi ya kwanza duniani kuanza maendeleo ya kisasa ya viwanda.

Sekta moja ya viwanda waliyoanza nayo, ambayo ilikuwa rahisi wakati huo na leo ni rahisi zaidi, ilikuwa ya kutengeneza nguo. Waingereza wakaitumia na wakajenga viwanda. Nguo zao zikawa zinatokana na viwanda vyao. 

Vile vile, walikuwa wana dola kubwa. Walikuwa wanatutawala sisi Afrika, wanawatawala Asia na wanatawala sehemu nyingine za Amerika, lakini hasa Afrika na Asia. Walipoingia India, walikuta Wahindi tayari wanatengeneza nguo zao kwa mashini. Wakawaza “hata Wahindi nao wanatengeneza nguo! Haina maana”. Wakawazuia Wahindi kutengeneza nguo kusudi soko duniani liwe la Waingereza: liwe huru lisizuiwe zuiwe.

Namna moja kulifanya soko hilo kuwa huru ilikuwa ni kwa kuvitawala vijitu hivi, halafu unauza vitu vyako. Wenyewe ndivyo walivyoanza na viwanda vya nguo na, baadaye, wakaongeza vingine na hatima yake, Waingereza wakawa wakubwa. Wenzao duniani wakaona  “Alaa hivi Vingereza tunaviachia vinaendelea namna hii kwa nini?”. Wakaanza mambo, wakagombana gombana, wakapigana pigana na wakanyang’ anyana. 

Tulipojitawala mwaka sitini na moja tulikuwa tunajua mambo haya, ijapokuwa tulikuwa wachache, kwamba nchi haiwezi kuendelea na kuwa ya kisasa bila viwanda. Mtawachumia pamba wakubwa hawa na kukata miwa. Hiyo ilikuwa sababu moja ya kuleta utumwa ili kuwachukua Waafrika waende Marekani wakachume pamba na wakakate miwa.

Baada ya kupata uhuru tukajiuliza. Leo tunajitawala, tuendelee kuchuma pamba na kukata miwa? Tukaamua: Tuanze kujenga viwanda kwa kuwa sisi tunalima pamba. Kwa hiyo, shughuli ya kwanza kabisa tutakayoanza nayo ni ya kujenga viwanda vya nguo. 

Nikawaomba wanaojua mambo haya ya viwanda duniani. Wakati huo sisi wenyewe hatukuwa na watalaam. Nikawaeleza watu hawa maneno haya: Hivi tunajitawala, tuendelee kuuza pamba ghafi nje? Nataka nianze kutengeneza nguo hapa Tanzania.
 Wakanishauri na wakaniambia Mwalimu, mnaweza kuanza kutengeneza nguo kutoka pamba yenu hapa. Jenga uwezo ili Tanzania iweze kutumia asilimia themanini na tano (85%) ya pamba inayolimwa Tanzania kutengeneza nguo hapa hapa. 

Walinishauri nijenge uwezo ndani ya Tanzania wa kutumia asilimia themanini na tano (85%) ya pamba yetu hapa hapa. Asilimia kumi na tano (15%) ya pamba iliyobaki, ama tunaweza tuitumie wenyewe hapa hapa au tunaweza kuiuza nje. Hiyo ilikuwa safi sana, kwamba tujenge viwanda kwa makusudi kabisa.
 Wakati ule, hata mimi ningekuwa na sera za kibepari, ningejenga viwanda. Mabepari ndio walioanza viwanda na viwanda vyenyewe hivyo havikuwa na sera ya ubepari au ujamaa. Vilikuwa ni viwanda tu! Sasa tukaanza kujenga viwanda vya nguo na sasa sitaki kusema sana juu ya jambo hili.

HAFIDH KIDO
DAR ES SALAAM, TANZANIA
1st May, 2013

No comments:

Post a Comment