Sunday, May 5, 2013

DRFA yazipongeza Red Coast, Abajalo, Friends Rangers




CHAMA cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), kimezipongeza timu zake tatu zilizofuzu kucheza Ligi ya Mabingwa, baada ya kumalizika kwa Ligi Daraja la Pili hatua ya sita bora Aprili 27 mwaka huu.  



Timu hizo ni Red Coast, Abajalo na Friends Rangers, zitakazoungana na timu za mikoa mingine kucheza Ligi ya Mabingwa itakayoanza Mei 12 mwaka huu chini ya Usimamizi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa DRFA, Mohamed Mharizo, alisema ligi hiyo ilikuwa na ushindani wa hali ya juu na kuzitaka timu zilizofuzu hatua hiyo kujipanga vizuri ili kuuwakilisha vyema mkoa na hatimaye kucheza Ligi Daraja la Kwanza.


“Kwa niaba ya DRFA napenda kuchukua nafasi hii kuzipongeza timu hizo kwa kufanya vizuri na kupata nafasi ya kuuwakilisha mkoa wa Dar es Salaam katika kutafuta kucheza Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao wa 2013/2014.

“Tunaamini watajiandaa vyema na kutuwakilisha vizuri katika ligi hiyo, kufanya kwao vizuri ndio itakuwa fahari yetu DRFA na wadau wa mpira wa miguu mkoa wa Dar es Salaam, tunawatakia kila la kheri na tupo pamoja katika kushirikiana nao.

Ligi Daraja la Pili hatua ya sita bora mkoa wa Dar es Salaam ilianza Aprili 15 mwaka huu ambapo ameziomba timu za Sharif Stars, Day Break na Boom FC zilizoshiriki ligi hiyo kujiandaa vizuri kwa ajili ya mashindano yajayo.

No comments:

Post a Comment