Thursday, May 23, 2013

Hali bado tete vurugu za gesi Mtwara.


Waziri wa Nishati na Madini Prof Sospeter Muhojngo akijadiliana na baadhi ya Mawaziri na Wabunge mara baada ya kikao cha Bunge kuahirishwa jana ili kufuatilia vurugu za Mtwara.




Mtwara. Wakati mtu mwingine akiripotiwa kufa, hali bado ni tete katika Mji wa Mtwara kutokana na mabomu ya machozi na risasi za moto kuendelea kurindima kwenye mitaa kadhaa wakati polisi wakipambana na makundi ya vijana wanaopinga mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kwenda Dar es Salaam.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula, Mohamedi Kodi alithibitisha kupokea mwili wa mjamzito ukiwa na tundu tumboni, linaloaminika kuwa linatokana na risasi.

“Ni kweli kwa leo tumepokea maiti moja ya mwanamke ambaye ni mjamzito wa miezi saba akiwa amepigwa risasi tumboni,” alisema Dk Kodi. Inadaiwa kwamba mjamzito huyo ambaye jina lake halikufahamika, ameuawa akiwa nyumbani kwake. Kifo hicho ni cha pili baada ya Karim Shaibu (22), mkazi wa Chikongola kuuawa juzi.

Aidha, kuna taarifa ambazo hazijathibitishwa kuwa mtu mwingine ambaye jinsia yake haikujulikana aliuawa kwa bomu la machozi na mwili wake kutawanyika barabarani.

Kuhusu majeruhi, Dk Kodi alisema wamefikia watu 18... “Majeruhi wa mwisho tuliyempokea ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Chuno. Alikuwa amevunjwa miguu yote kwa risasi.”

Waomba hifadhi hospitalini

Umati wa watu wengi wao wakiwa kinamama na watoto umemiminika kwenye Hospitali ya Ligula kukimbia msako wa nyumba kwa nyumba unaofanywa na polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti, wakazi hao wamelalamikia kitendo cha polisi kuingia katika makazi yao, kuwapiga na kuwapora mali zao.

“Magomeni A hatuna amani, askari wanaingia nyumbani kwetu, wanatupiga na kutunyang’anya simu, yaani huku Magomeni hatuna amani kabisa, tumepotezana na watoto na hatujui hata waume zetu wako wapi,” alisema Paulina Idd.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa alisema hali ni shwari na kuwataka wananchi kuendelea na shughuli zao kama kawaida.

Hadi sasa huduma za kijamii zimesimama, hakuna maduka yaliyofunguliwa, hakuna usafiri wa daladala wala pikipiki, mji upo kimya huku sauti za milio ya mabomu na bunduki ikitawala, wanajeshi waliovalia sare wametapakaa sehemu mbalimbali za mji wakiwa katika magari na pikipiki.

Nchimbi atua Mtwara, jeshi lamwaga vifaa

Dk Nchimbi aliwasili jana jioni kwa helikopta na kukutana na viongozi wa Mkoa wa Mtwara walioongozwa na Mkuu wa Mkoa, Kanali Joseph Simbakalia kujadili suala hilo.

Pia ndege kubwa ya jeshi nayo ilitua huko na wanajeshi walikuwa wakipakua vitu mbalimbali vilivyoaminika kuwa vifaa.

Jeshi hilo limeombwa kuongeza kukabiliana na vurugu hizo ambazo zimesambaa sehemu mbalimbali za Mtwara.

Imeandikwa na Haika Kimaro, Mary Sanyiwa na Elias Msuya.
MWANANCHI

No comments:

Post a Comment