Tuesday, May 14, 2013

Hatimaye Mancini atupiwa virago rasmi....





London, England

Hatimaye kocha wa Manchester City, Roberto Mancini ametimuliwa rasmi kuinoa timu hiyo baada ya kukanusha uvumi huo mwishoni mwa wiki hii.

Uongozi wa Man City umetoa taarifa yake Jumatatu na kuweka wazi kuwa “ameshindwa kutimiza malengo ya klabu, kwa matarajio ya kuchukua ubingwa wa klabu bingwa Ulaya msimu ujao.”

Kocha msaidizi Brian Kidd atasimamia mechi mbili zilizobaki za ligi kuu ya Uingereza na ziara yao ya Marekani mwishoni mwa mwezi huu. Taarifa zinaeleza kuwa kocha wa Malaga, Manuel Pellegrini kutoka Chile ndiye anayetajwa kuchukua mikoba ya Mancini kwa msimu ujao.

Katika taarifa ya kumtimua kocha huyo iliyosomwa na mwenyekiti wa klabu hiyo Khaldoon Al Mubarak, inamshukuru kocha huyo mwenye miaka 48 ambaye ameanza kuinoa timu hiyo tangu mwaka 2009 na kufanikiwa kunyakua ubingwa wa ligi hiyo mwaka 2012 ambapo Man city kwa mara ya mwisho kuhukua ubingwa huo ni miaka 44 iliyopita.

Mbali ya ubingwa wa ligi kuu pia Mancini amefanikiwa kunyakua ubingwa wa FA mwaka 2011 na kuifanya kuwa ni timu yenye mafanikio sana tangu kujiunga kwake mwaka 2009.

“Rekodi ya Roberto inazungumza yenyewe, ameweza kulinda mapenzi na heshima ya mashabiki wa Man City, amefanya alichotuahidi na ameleta mafanikio. Ni maamuzi magumu sana kutengana na Mancini lakini ni matokeo ya mipango na mapitio ya msimu huu kuwa mabaya,” alieleza mwenyekiti Khaldoon.

HAFIDH KIDO
May 14, 2013





No comments:

Post a Comment