Saturday, May 11, 2013

Sheikh Ponda bado atamba...

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba akitoka kuswali Swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Mtambani, Kinondoni, jana. Picha na Mpigapicha Wetu. 





Dar es Salaam. Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Nchini, Sheikh Issa Ponda ameiomba Serikali kuunda Tume ya kushughulikia matatizo ya Waislamu.
Ponda alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa mawaidha ya Ijumaa katika Msikiti wa Mtambani, wilayani Kinondoni.
Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kumhukumu kifungo cha mwaka mmoja nje, baada ya kupatikana na hatia ya kuingia isivyo halali katika eneo la Markazi Chang’ombe.
Alisema kwa muda mrefu Waislamu nchini wamekuwa na madai ambayo Serikali haijaonyesha dhamira ya kuyashughulikia.
“Waislamu wamekuwa wakinyanyasiki katika nchi yao utadhani wakimbizi, tuna madai ya msingi ambayo hayahitaji watu kufungwa au kuundiwa kesi kwa hiyo sasa ni wakati wa Serikali kuunda tume tutakayokwenda kuwaeleza matatizo yetu na vithibitisho vyake,” alisema Ponda.
Ponda alisema atahakikisha kuwa anawatetea Waislamu ili wapate haki zao zinazopokwa na baadhi ya watu wasiowapenda waumini wa dini hiyo.
“Wamekuwa wakinitungia njama za kuniondoa kwa misingi ya kuwa mimi siyo Mtanzania, hakuna wa kuniondoa hapa nchini na nitapambana hadi hatua ya mwisho na kuhakikisha kuwa Waislamu wanapata uhuru wao,” alinena Sheikh Ponda.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alielezea kusikitishwa kwake juu ya kauli kwamba Sheikh Ponda asingeweza kupata dhamana katika kesi iliyokuwa ikimkabili.
“Vyombo vyetu haviko makini, tuliambiwa Ponda hawezi kupata dhamana lakini leo hii amefungwa kifungo cha nje, hii inatia shaka na uamuzi uliokuwa ukiendelea,” alisema Profesa Lipumba.
Mtaalamu huyo wa uchumi, alitumia nafasi hiyo kuwataka Waislamu kuungana na kuhakikisha kuwa wanatetea haki zao.
“Tuache unafiki, tuungane na kumsikiliza Ponda kwa kauli zake, matendo yake ili kufikia kile ambacho Waislamu wanakitaka,” alinena Profesa Lipumba.
Umati mkubwa wa waumini wa Kiislamu walimiminika kutaka kusikia mawaidha ya katibu huyo kwa mara ya kwanza baada ya kutoka gerezani juzi.
Katika tukio hilo, waumini pia walichanga fedha kwa ajili kumwezesha Sheikh Ponda kugharimia matibabu ya afya yake na sehemu ya fedha hizo walipewa mawakili wake ili wafanye maandalizi ya kukata rufaa.
Pia Mei 18 mwaka huu, waumini hao wamepanga kufanya dua (Itikafu) itakayofanyika katika msikiti huo kwa ajili ya kumwombea Sheikh Ponda na wenzake.
MWANANCHI

No comments:

Post a Comment