Saturday, May 11, 2013

Waarabu watoa tamko kuhusu bomu la Arusha..


Dar es Salaam/Arusha. Serikali za Saudi Arabia na Falme za Kiarabu (UAE) zimezungumzia kukamatwa kwa raia wake, ambao wanahusishwa na tuhuma za kurushwa kwa bomu kwenye Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Arusha, Jumapili iliyopita.
Watu watatu walifariki dunia na wengine 60, akiwamo Balozi wa Vatican nchini na Mwakilishi wa Papa, Francisco Montecillo Padilla wakijeruhiwa baada ya bomu kurushwa wakati wa ufunguzi wa kanisa hilo lililoko Parokia ya Olasiti.
Watu tisa wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo la kigaidi, kati yao Watanzania ni watano na raia wageni wanne.
Viongozi wa Serikali walikaririwa wakisema wageni waliokamatwa raia watatu ni wa Saudi Arabia na mmoja wa UAE ambao walikamatwa wakati wakiondoka nchini kupitia Namanga.
Balozi wa Saudi Arabia
Balozi wa Saudi Arabia nchini, Hani Momina alikaririwa na mashirika ya habari ya kimataifa akikiri kukamatwa kwa raia wa nchi yake na kusisitiza kwamba hakukuwa na ushahidi wa kumhusisha na shambulizi hilo kwani alikuja Tanzania kutalii.
Momina alisema alikutana na Mwenyekiti wa Kikosi Kazi kinachochunguza suala hilo kwenye kituo cha polisi anaposhikiwa raia wake akitaka kujua kama mtu wao amewekwa vizuri.
“Tuna matumaini makubwa kuwa wataachiwa na tutaendelea kufuatilia suala lao hadi tuone mwisho wake,” alisema Balozi huyo na kusisitiza kwamba hawaondoki Arusha.
Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya UAE, kupitia mtandao wa Twitter ilieleza kuwa inafuatilia kwa karibu suala la raia wake watatu waliokamatwa. Ilisema walikuwa wanafanya kazi kwa karibu na ubalozi wa nchi yao huko Tanzania ili kufahamu hatima ya watu wao.
UAE imesema inapinga kwa nguvu zote vitendo vya ugaidi na iko tayari kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Tanzania juu ya raia wake kuhusishwa na tukio hilo.
Majeruhi saba waletwa Dar
Majeruhi saba wa mlipuko huo walisafirishwa kwa ndege kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili baada ya hali zao kuwa mbaya.
Majeruhi waliosafirishwa jana ni Jenipha Joachim aliyeumia kwenye mapafu na miguuni. Alimpoteza mtoto wake, Patricia Joachim juzi.
Wengine ni Fatuma Tarimo, ambaye chembechembe za vyuma zimeingia tumboni, Apolinary Malasha aliyejeruhiwa miguu na jicho kutokana na masalia ya vyuma vya mabomu, Albert Njau ambaye amedhurika mbavu na mgongo na Faustin Shirima ambaye amekutwa na vyuma tumboni.
Wengine ni Gabriel Godfrey (9) ambaye ana chembechembe za bomu tumboni na miguuni na Athanas Mrema(14) ambaye amevunjika mbavu na pia ana chembechembe za vyuma tumboni.
Kutokana na tukio hilo, wabunge walichangia posho yao kwa kikao cha jana ambayo ni Sh200,000 kwa kila mmoja.
Utata aliyefariki KCMC
Jina la mtoto Patricia Assey (9) ambaye ni miongoni mwa waliouawa katika mlipuko wa bomu hilo lilizua utata jana kiasi cha kufanya uongozi wa Hospitali ya KCMC na polisi kuzuia mwili wake kwa muda.

Wakati huo huo taarifa za jana zinaeleza kuwa majeruhi wameanza kutoa ya moyoni kuhusu kilichotokea na kueleza kuwa Bomu lililorushwa na kuua watu watatu na kujeruhi wengine zaidi ya 60 kwenye Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi huko Arusha, inadaiwa lilitengenezwa kienyeji.

Wakati kukiwa na madai hayo, mazishi ya marehemu hao Regina Kurusei, (45), James Gabriel (16) na Patricia Joachim (9) yanatazamiwa kufanyika leo Olasiti, Arusha na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda anatarajiwa kuhudhuria.
Ofisa mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alimdokeza mwandishi wetu jana kuwa kwa ujuzi na uzoefu wake wa masuala hayo, bomu hilo si la kiwandani akisema msingi wa imani yake ni jinsi vyuma vilivyotawanyika na kuumiza watu zaidi ya 20.
Watu saba wamefikishwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya kuondolewa vyuma na kupata matibabu zaidi.
Mstaafu huyo alieleza kuwa mabomu mengi zaidi ya kienyeji hutengenezwa kwa kutumia bakuli za chuma, zikiwekewa baruti ndani na kufungwa kwa waya.
“Hawa jamaa huweka vipande kama 36 vya baruti na hufungiwa ndani ya bakuli kwa kubanwa sana ili kuvipa joto na bomu likitua, husababisha madhara makubwa,” alisema ofisa huyo ambaye alishiriki Vita ya Uganda mwaka 1978 hadi 1979.
Mstaafu huyo alisema mabomu ya aina hiyo yametumika kwenye mashambulizi ya kigaidi katika nchi mbalimbali duniani kama Lebanon, Vietnam, Libya, Ireland Kaskazini, Syria, Afghanistan, Iraq, Chechnya na India.
Mmoja wa majeruhi, Mwalimu Fatuma Tarimo amesimulia alivyoshuhudia bomu likitua mbele yake na kulipuka.
Tarimo, ambaye amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, alisema jana kuwa aliliona bomu hilo likiwa na rangi ya shaba. Pia alisema lilikuwa na waya kwa juu.
“Baada ya kutua, nilisikia kishindo kikubwa nikashtuka ikabidi niangalie. Baada ya kuona ni kitu kama chuma nilipata hofu nikafikiria kuondoka,” alisema mwalimu huyo wa Shule ya Msingi ya Burka Estate, nje kidogo ya Jiji la Arusha. Hata hivyo, alisema kabla ya kuondoka, alishtukia amenyanyuliwa juu na hakujua kilichoendelea kwani aliposhtuka alijikuta akiwa katika Hospitali ya Mount Meru.
Tarimo ametolewa kipande cha chuma katika mguu wake wa kulia.
“Nina maumivu bado lakini nina matumaini nimechukuliwa kipimo cha ‘T-Scan’ kwa matibabu zaidi,” alisema Mwalimu Tarimo ambaye anaaminika kuwa na kipande kingine kwenye mapafu.
Majeruhi mwingine, Jenipher Joackim ambaye amefiwa na mwanaye Patricia Joackim (9) hana taarifa za kifo hicho kilichotokea katika Hospitali ya KCMC.
“Nimeambiwa kwamba yupo ICU sijui anaendeleaje,” alisema.
 MWANANCHI

No comments:

Post a Comment