Monday, May 27, 2013

Wanafunzi kidato cha nne kupata mteremko....

Dar es Salaam. Idadi ya watahiniwa waliofaulu mtihani wa kidato cha nne mwaka jana imeongezeka kwa kati ya asilimia 20 na 23 baada ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), kufanya marekebisho alama za viwango vya ufaulu, Mwananchi limebaini.

Habari ambazo gazeti hili imezipata zinasema matokeo hayo ambayo yamewezesha kiwango cha ufaulu kupanda na kufikia asilimia kati ya 54 na 57, huenda yakatangazwa wiki hii pamoja na yale ya kidato cha sita ambayo pia yamechelewa kutangazwa.

Chanzo cha habari kutoka Necta kimesema matokeo hayo mapya yanaonyesha kuwa, ufaulu wa kuanzia daraja la kwanza hadi la nne umeongezeka kutoka asilimia 34.5 kwa matokeo yaliyotangazwa awali na huenda yakafikia asilimia 57. Hii inamaanisha kwamba watahiniwa wapatao 82,000 ambao awali walikuwa wamepata sifuri katika matokeo ya awali sasa wamepanda na kupata madaraja ya ufaulu katika matokeo mapya.

Kwa matokeo hayo, watahiniwa wa mwaka 2012 watakuwa wamefanya vizuri kuliko wa mwaka 2011, ambao watahiniwa 225,126 sawa na asilimia 53.37 ya 349,390 waliofanya mtihani huo walifaulu.

Msemaji wa Necta, John Nchimbi alisema upangaji wa matokeo hayo ulikuwa bado unaendelea. “Ninachojua kwa sasa ni kuwa mchakato unaendelea na matokeo yatatangazwa mapema tu ili watoto waweze kujiunga na shule mapema,” alisema Nchimbi.

Pia alisema usahihishaji wa mitihani ya kidato cha sita umekamilika.

Matokeo ya awali

Matokeo ya awali yaliyotangazwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa yalionyesha kuwa kati ya watahiniwa 367,756 waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana, waliokuwa wamefaulu kwa daraja la kwanza mpaka la tatu walikuwa 126,847 sawa na asilimia 6.4. Waliopata daraja la nne walikuwa ni 103,327 sawa na asilimia 28.1.

Katika matokeo hayo, watahiniwa 240,909 sawa na asilimia 65.5 walipata sifuri, hesabu ambayo imebadilika katika matokeo mapya ambayo yanaonyesha kuwa sasa waliopata daraja hilo ni 158,100 ambayo ni asilimia 43.

Hata hivyo, habari kutoka Necta zinasema kuwa licha ya kuwezesha kuongezeka kwa waliofaulu, matumizi ya kanuni mpya ya kukokotoa matokeo hayo yalisababisha zaidi ya wanafunzi 2,500 kushuka ufaulu ikilinganishwa na awali.

Maofisa mbalimbali wa Necta pamoja na wale wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na taasisi zake, walikutana mwishoni mwa wiki iliyopita kukubaliana masuala mbalimbali juu ya matokeo hayo pamoja na suala la matokeo ya wanafunzi hao 2,500 kabla ya kutangazwa wiki hii.

“Baada ya wajumbe kujadili suala lile, busara ilibidi itumike kwa hiyo hakuna mwanafunzi ambaye alama yake itashuka, kwa kawaida isingewezekana mtoto ambaye matokeo yalitoka akiwa amefaulu leo umwambie ameshuka,” kilieleza chanzo chetu.

Matokeo ya awali ndiyo chimbuko la kupitiwa upya baada ya wadau kuyalalamikia na kumlazimisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuunda tume ya kuyachunguza Februari 23, mwaka huu.

Kabla ya tume hiyo kuhitimisha shughuli zake, ilitoa taarifa ya awali ambayo ilipendekeza kufutwa kwa matokeo hayo kwa maelezo kwamba Necta ilitumia kanuni mpya ya kukokotoa matokeo bila kushauriana na wadau.

Serikali ilitoa taarifa bungeni kwamba imeamua kufuta matokeo ya 2012 na kuamuru yapangwe upya kwa kufuata madaraja yaliyotumika mwaka 2011.

Ratiba ya Bunge

Wakati hayo yakiendelea, ratiba ya vikao vya Bunge la bajeti imefanyiwa marekebisho na kusogeza mbele zamu ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambayo awali, ilikuwa imepangwa kusoma hotuba yake ya makadirio ya matumizi leo, badala yake nafasi hiyo imepewa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Wizara ya Elimu sasa imepangiwa kuwasilisha hotuba yake Juni 4 mwaka huu, hatua ambayo inatajwa kwamba lengo ni kusubiri kutangazwa kwa matokeo hayo ya kidato cha nne na kidato cha sita.

Wakati Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete alipokutana na wabunge wa chama chake Mei 19, mwaka huu mjini Dodoma, walisema hawako tayari kujadili hotuba ya wizara hiyo hadi matokeo ya kidato cha nne na sita yatakapotangazwa.

Katika mabadiliko hayo, hotuba ya Wizara ya Elimu imeondolewa kama ilivyotarajiwa na sasa italetwa bungeni Juni 3.

Taarifa zinaeleza kuwa, kusogezwa kwa hotuba hiyo kunatokana na mipango ya Serikali ambayo inatafuta namna na kukamilisha mchakato wa matokeo ya kidato cha nne ili kuipa mteremko hotuba ya Waziri wa Elimu, Shukuru Kawambwa bungeni.

Tofauti na mapumziko ya siku mbili za kawaida kwa wabunge, safari hii walipumzika siku moja baada ya Jumamosi kutumiwa kwa ajili ya kuhitimisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini ambayo iliahirishwa Alhamisi iliyopita kutokana na vurugu za Mtwara.

Ratiba ya awali inaonyesha kuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilikuwa isome hotuba yake ikifuatiwa na Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kabla ya kuhitimisha wiki kwa kusoma Makadirio ya Wizara ya Mambo ya Nje.

Wizara ya Elimu ilikuwa katika ‘mtihani’ kwenye Kikao cha 10 cha Bunge mapema Februari,  hasa baada ya Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia kuwasilisha hoja binafsi kuhusu udhaifu uliopo katika sekta ya elimu na zaidi ni kukosekana kwa mitalaa ya elimu.

Hatua hiyo ililazimisha Waziri wa Elimu, Shukuru Kawambwa kupewa muda kuwasilisha mtalaa huo na alifanya hivyo Februari 6, ukihusisha elimu ya chekechea, elimu ya msingi na sekondari kabla ya kupitishwa na Bunge.

Kamati ndogo iliundwa chini ya Magreth Sitta akiwemo Mbatia na wabunge wengine waliobobea katika masuala ya elimu kuangalia uhalali wake.

Hata hivyo, katika kile kinachoelezwa kuwa ni wasiwasi kwa Serikali kuhusu hofu ya vivuli vya wabunge wa upinzani, ratiba ilibadilishwa na kuisogeza mbele hotuba ya Wizara ya Elimu.

Ratiba mpya ya Bunge sasa inaonyesha kuwa, leo Bunge litapokea hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambayo itajadiliwa kwa siku mbili.

Hotuba hiyo pia haitegemei kuwa na mteremko kwani wabunge watakuwa na shauku ya kujadili kuhusu migogoro ya mipaka pamoja na masuala ya upimaji wa ardhi ili kuondoa kero za wakulima na wafugaji yakiwemo mashamba yanayomilikiwa bila kuendelezwa.

Baada ya hotuba hiyo yatafuata Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Wizara ya Kazi na Ajira na kufuatiwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Nchi kabla ya kuhitimishwa kwa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ambazo zote zitakuwa zikisomwa na kujadiliwa kwa siku moja.

MWANANCHI

No comments:

Post a Comment