Monday, May 20, 2013

Waraka kuhusu muswada wa Baraza la Vijana la Taifa wa Mwaka 2013

Sunday, May 19, 2013

Vijana wenzangu na wote wenye dhamira ya kuwezesha maendeleo ya vijana nchini, salaam!

Mtakumbuka kwamba mwezi Januari 2013 nilitoa taarifa kwa umma ya kueleza kuwa niliwasilisha kwa Katibu wa Bunge Muswada Binafsi wa Sheria ya Baraza la Vijana la Taifa na kuomba hatua za ziada toka ofisi ya Bunge kwa kuzingatia Kanuni ya 21 na Kanuni ya 81 ya Kanuni za Kudumu za Bunge.

Toka wakati huo muswada huo mpaka sasa Mei 2013 haujachapwa katika gazeti la Serikali na nimepokea barua toka kwa ofisi ya Bunge kwamba wamepokea ushauri toka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa muswada huo hauwezi kuchapishwa katika gazeti la Serikali kwa kuwa umekiuka masharti ya ibara ya 99 ya Katiba ya Nchi.

Sababu ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutoa ushauri huo ni kuwa muswada unalenga pamoja na mambo mengine kupitia kifungu cha 31 kipengele cha kwanza kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kwa madhumuni ya kugharamia shughuli za baraza la vijana la taifa, mipango ya baraza na kutekeleza miradi ya vijana kwa ajili ya maendeleo ya vijana.

Kwa maoni yangu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametoa ushauri huo bila kuzingatia kwamba kifungu cha 31 kipengele cha pili kinataja vyanzo mbalimbali vya fedha za mfuko ikiwemo kutaja kuwa fedha za mfuko zitatokana na fedha zilizotengwa na Serikali na Bunge kwa ajili ya Baraza kwa mujibu wa Ibara ya 135 kifungu cha pili cha katiba ya Nchi.

Ibara ya 135 (2) ya Katiba ya Nchi inatamka kuwa “fedha ambazo hazitawekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali ni zile zote ambazo zimetajwa na sheria ya kwamba zitumike kwa shughuli maalum au ziwekwe kwenye mfuko mwingine kwa ajili ya matumizi maalum”.

Hivyo, ni maoni yangu kuwa ibara hiyo ya Katiba ya Nchi inaweza kutumika kuwezesha kuanzishwa kwa Baraza la Vijana na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana bila kufungwa na Ibara ya 99 ya Katiba kifungu cha kwanza ambacho kimeweka masharti kuwa “Bunge halitashughulikia jambo lolote kati ya mambo yanayohusika na ibara hii isipokuwa kama Rais amependekeza kwamba jambo hilo lishughulikiwe na Bunge na pendekezo hilo la Rais liwe limewasilishwa kwenye Bunge na Rais.”

Kifungu cha pili kinataja mambo yanayohusika na ibara hiyo ya 99 ni pamoja na muswada wa sheria kwa ajili ya “kuagiza kwamba malipo au matumizi ya fedha yafanywe kutokana na Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali au mfuko mwingine wowote au kubadilisha kiwango hicho kwa namna nyingine yoyote isipokuwa kupunguza”.

Toka Sera ya zamani ya maendeleo ya vijana ya mwaka 1996 itamke kwamba Serikali itawezesha kuanzishwa kwa Baraza la Vijana na suala hilo kurudiwa katika Sera mpya ya mwaka 2007; miaka takribani 17 imepita marais wote wa awamu husika na mawaziri wenye dhamana hawajawasilisha bungeni muswada huo hali ambayo imenifanya niandae muswada binafsi kuwezesha baraza kuundwa.

Muswada wa Sheria ya Baraza la Vijana la Taifa 2013 niliouwasilisha kwa maoni yangu hauna lengo la kuagiza malipo au matumizi ya fedha yafanywe kutokana na Mfuko mkuu wa Hazina ya Serikali au Mfuko mwingine wowote kwa mujibu wa ibara ya 99 bali unalenga kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kwa kuzingatia masharti ya Ibara ya 135.

Hata hivyo, kwa kuwa muswada huu unahusu mustakabali wa vijana na ni suala la kitaifa kupitia waraka huu naomba kupata maoni yenu kuhusu suala hili, mapendekezo ya marekebisho yanayohitajika kufanyika na hatua zinazopaswa kuchukuliwa.

Maoni, mapendekezo na hatua hizo zitumwe kupitia mbungeubungo@gmail.com au kwa Afisa wa Ofisi ya Mbunge Ubungo Gaston Garubimbi (0715825025) kabla ya tarehe 24 Mei 2013.

Nakala ya rasimu ya muswada wa Baraza la Vijana la Taifa wa mwaka 2013 inapatikana katika mtandao wa http://mnyika.blogspot.com kwa ajili ya rejea.


Aidha, nawaalika kushiriki mikutano ya kupokea maoni kupitia mtandao huo tarehe 20 mpaka 23 Mei 2013 saa 9 alasiri mpaka 10 Jioni ambayo nitashiriki na kutoa maelezo ya zaidi kwa kadiri itakavyohitajika.

Natarajia kupokea maoni ya vijana na wananchi wengine bila kujali tofauti mbalimbali kwa kuwa madai ya kutaka kuundwe Baraza la Vijana la Taifa yamekuwa yakitolewa na vijana, asasi na taasisi kwa muda mrefu.

Vyama vya siasa kwa kuzingatia matakwa hayo viliahidi kutekeleza azma hiyo kwa mfano Ilani ya CHADEMA ya mwaka 2010-2015 kipengele 6.4.1 (viii) ilitamka “Kwa kuwa vijana ndio kundi kubwa hapa nchini, na kwa kuwa uhai wa muda mrefu wa taifa letu upo mikononi mwa vijana, Serikali ya CHADEMA itawezesha vijana kuunda Baraza la Vijana (BAVITA) ambalo limekwamishwa na Serikali ya CCM kwa muda mrefu”.

Kwa upande mwingine, Ilani ya CCM ya mwaka 2010-2015 iliahidi katika kipengele 80 (k) “Kuhamasisha ushiriki wa vijana katika ngazi mbalimbali za maamuzi ikiwa ni pamoja na kukamilisha uanzishaji wa Baraza la Vijana”.

Mwaka 2011 niliihoji Serikali bungeni ni lini itakamilisha uanzishwaji wa baraza hilo na ikaahidi kwamba kazi hiyo itakamilishwa katika mwaka wa fedha 2011/2012 hata hivyo sasa ni Mei 2013 Serikali haijakamilisha.

Hivyo vijana, wabunge na wananchi kwa ujumla ni muhimu kuboresha muswada huo na uwasilishwe bungeni kuwezesha baraza la vijana na mfuko wa maendeleo vijana kuanzishwa; maslahi ya umma kwanza.

Wenu katika uwakilishi wa wananchi,

John Mnyika (Mb)
19 Mei 2013
Dodoma


Muswada wa Baraza la Vijana 2013-Rasimu ya Kwanza; pakua hapa (download here):
https://docs.google.com/file/d/0B8xvLNf5FlohSHJPX2trR3p6YzQ/edit?usp=sharing

No comments:

Post a Comment