Sunday, May 12, 2013

Waziri wa kwanza mweusi Italia atamba kuwa mweusi....


Roma, Italia
Kauli ya waziri wa kwanza mweusi nchini Italia kuhusu kujivunia kuzaliwa mweusi imezua mjadala mkubwa nchini humo baada ya kudhamiria kujibu maneno ya ubaguzi wa rangi na jinsia dhidi yake.

Cecilia Kyege mzaliwa wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo (DRC), baada ya uteuzi wake kuwa waziri anayeshughulikia masuala ya ubaguzi wiki iliyopita alitangaza anajisikia fahari kuwa mweusi na kwamba Italia si kweli kuwa ni nchi ya ubaguzi.


Waziri huyo ambaye alifika Italia mwaka 1983 akiwa na umri wa miaka 18 tu anasema alikwenda Italia kwa lengo la kusoma lakini akaona ni mahala pazuri kuendesha maisha yake.

Waziri Mkuu mpya wa Italia Enrico Letta aliamua kuweka kitu tofauti katika baraza la mawaziri baada ya Jumamosi iliyopita kumfanya Kyege kuwa mmoja wa wanawake saba katika serikali mpya.

Tangu kuteuliwa kwake kushika wadhifa wa waziri anayesimamia masuala ya ubaguzi, Kyege amekuwa akiandamwa na maneno ya udhalilishaji kwenye tovuti mbali kuhusiana na asili yake. Baadhi ya majina mabaya anayobandikwa katika tovuti ni kama "tumbili wa Kongo", "Zulu" na "Mweusi mpinga Italia".

Aidha waziri huyo anapata wakati mgumu kutokana na maneno ya kibaguzi na udhalilishaji kutoka kwa mbunge wa jumuiya ya Ulaya Mario Borghezio, ambaye ni mwanachama wa (pro-devolution League) ya Kaskazini, ambayo imekuwa na ushirika katika siku za nyuma na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Italia Silvio Berlusconi.

Borghezio amekwenda mbali zaidi na kusema Waziri Kyege hafai kushika wadhifa huo kwani hana sifa za uwaziri ila anapendeza kuwa mama wa nyumbani.


Mbali ya shutuma hizo anazokumbana nazo waziri huyo ameendelea kuweka msisitizo wake kuwa Italia si nchi ya kibaguzi na ana mpango wa kuandaa taarifa maalum katika bunge la nchi hiyo ili kuundwa kwa sheria ambayo itaweza kuruhusu watoto waliozaliwa Italia na wazazi wahamiaji kupata uraia wa moja kwa moja badala ya kusubiri mpaka kufikisha umri wa miaka 18 ili kuomba.

"Mimi niliwasili nchini Italia peke yangu nikiwa na umri wa miaka 18, na siamini katika kukata tamaa mbele ya vikwazo," alisema Kyenge ambaye hataki neno mrangirangi ‘coloured’ linalotumiwa juu yake katika ripoti nyingi kwenye vyombo vya habari vya Kiitaliano, "Mimi si mrangirangi, mimi ni mweusi na nasema kwa kiburi kuwa ni mweusi."

Waziri Kyenge, ambaye ameolewa na Mtaliano mweupe amesema yeye hakuwa na mtazamo hasa kama Italia ni nchi ya ubaguzi wa rangi, na kuamini kwamba mitazamo ya uhasama inatokana na ujinga.

"Italia ina desturi ya kukaribisha wageni na sadaka ya ukarimu kwa watu wengine. Tunahitaji kutambua mila hizi na kuzitumia siku hadi siku, "alisema.

Wakati akizungumza na gazeti moja la Italia waziri huyo alisema tangu kuteuliwa kushika nafasi hiyo ameshapokea ujumbe mwingi wa vitisho vya kifo dhidi yake, nyingine zikiwa ni ujumbe wa udhalilishaji wa kingono katika mitandao kwa lengo la kumfanya akose umakini katika kazi yake mpya.

Cecilia Kyenge Kashetu amezaliwa Agosti 28, 1964 katika mji wa Katanga kijiji cha Kambove, nchini Kongo (DRC) kitaaluma ni daktari wa macho na mwanasiasa, ambaye ameolewa mwaka 1994 na mhandisi Domenico, pia wamejaaliwa kupata mabinti wawili Julia na Maisha.

Anaishi katika mji wa Castelfranco Emilia, ana shahada ya Madawa na upasuaji kutoka Chuo Kikuu cha Cattolica del Sacro Cuore mjini Roma. Pia ni mtaalamu katika ‘ophthalmology’ katika Chuo Kikuu cha Modena na Reggio Emilia.

HAFIDH KIDO
12 May, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA



No comments:

Post a Comment