Tuesday, May 7, 2013

Waziri wa Ulinzi Libya ajiuzulu...

  
                                              Waziri wa Ulinzi wa Libya Mohammed al-Barghathi 


Waziri wa Ulinzi wa Libya, Mohammed al –Barghathi amejiuzulu wadhifa wake huo akipinga kushikiliwa kwa majengo ya wizara za sheria na mambo ya nje na wanamgambo wenye silaha.
Wanamgambo hao wamekuwa wakidai kupitishwa kwa sheria inayowapiga marufuku maafisa wa serikali ya kiongozi wa zamani wan chi hiyo hayati Kanali Muammar Gaddafi, kupewa nyadhifa za kisiasa.
Jumapili iliyopita, ikiwa ni moja tangu wanamgambo hao wayashikilie majengo, bunge lilipitisha sheria hiyo.
“Sitakubali kwamba, siasa zitaendeshwa kwa nguvu ya mtutu wa bunduki,” shirika la habari la Reuters limemkariri waziri huyo wa ulinzi akisema.
Wanamgambo hao walidai kwamba, hawataondoka katika majengo hayo kabla ya kupitishwa kwa sheria hiyo inayowapiga marufuku maafisa hao wa zamani waliokuwa na nyadhifa wakati wa serikali ya Kanali Gaddafi.
“Hii ni sawa na kuishambulia demokrasia niliyoapa kuilinda,” amesema Bw. Barghathi amabye aliwahi kuwa kamanda wa jeshi la anga huko Benghazi kabla ya kustaafu na kulipwa mafao ya serikali mwaka 1994.

kutengwa kisiasa

Mwandishi wa BBC mjini Tripoli, Rana Jawad, anaripoti kuwa Sheria ya Kuwatenga kisiasa pia itamhusu Bw. Barghathi wakati itakapoanza kutumika.
Inaonekana amejiuzulu kabla ya kufukuzwa. Sheria hiyo huenda ikawaathiri maafisa wengine waandamizi wa serikali akiwemo Mkuu wa Baraza la taifa la Congress, Mohammed al – Megaryef.
Alijitoa kutoka serikali ya Kanali Gaddafi miaka ya themanini baada ya kuhudumu kama balozi wa Libya nchini India.
Mwandishi wetu anasema, tangu sheria hiyo ipitishwe wanamgambo kadhaa wameondoka kutoka majengo hayo, lakini baadhi ya vikundi vya wapiganaji wenye silaha nzito vimebakia.

Wale wanaoshikilia jengo la wizara ya nje, ambalo lilikuwa la kwanza kulengwa Jumapili ya Aprili 28 wamesema wako tayari kuondoka lakini bado hawajaondoka.
Nao wanamgambo nje ya wizara ya sheria iliyoxingirwa Jumanne iliyopita wamesema wanasubiri maafisa wa ulinzi wa serikali kuchukua nafasi yao.
Baraza la Juu la Mapinduzi ambacho ni chombo kinachodai kuwawakilisha wapiganaji kadhaa wa zamani na kinachoaminika kudhibiti baadhi ya makundi yenye silaha, limeiambia BBC kwamba, linataka Waziri Mkuu, Ali Zidan aondolewe madarakani.
Mwandishi wetu anaripoti kuwa, Waziri Mkuu ambaye inasemekana hataguswa na sheria hiyo mpya, hivi karibuni alivielezea vikundi vyenye silaha kama watu walioshindwa katika uchaguzi uliofanyika nchi nzima mwaka jana.
Kanali Gaddafi aliondolewa madarakani na hatimaye kuuawa wakati wa vuguvugu la mageuzi mwaka 2011 baada ya kuitawala Libya kwa zaidi ya miaka 40.
BBC SWAHILI

No comments:

Post a Comment