Wednesday, July 10, 2013

BRELA yarahisisha huduma za usajili wa biashara na kampuni.

 Kaimu meneja wa huduma, utawala na fedha BRELA, Bosco Gadi akionyesha kitabu chenye taratibu za kusajili biashara na kampuni wakati akizungumza na wanahabari katika ukumbi wa idara ya habari MAELEZO leo asubuhi, pembeni yake ni naibu mkurugenzi wa MAELEZO, Zamaradi Kawawa.

Wanahabari wakipitia nakala ya kitabu chenye taratibu za kusajili kampuni na biashara BRELA.
 Bosco akisisitiza jambo kwa wanahabari baada ya kutakiwa kutoa ufafanuzi wa masuala nyeti katika BRELA.

Andrew Mkapa, Naibu msajili mkuu wa idara ya sheria za biashara BRELA akitoa ufafanuzi kwa wanahabari leo asubuhi. Kushoto kwake ni Kaimu meneja huduma, utawala na fedha BRELA, Bosco Gadi akimsikiliza kwa makini.


Wajasiriamali wadogo na wakubwa wameaswa kusajili biashara zao na kupata kampuni zitakazowasaidia kufanya biashara kwa kushirikiana na makampuni makubwa ya ndani na nje.
Hayo yamezungumzwa na kaimu meneja huduma, utawala na fedha wa wakala wa usajili wa biashara na leseni (BRELA), Bosco Gadi wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa idara ya habari MAELEZO jijini Dar es Salaam leo asubuhi.
Bosco ameweka wazi kuwa ili kurahisisha ushawishi wa kusajili biashara kwa wajasiriamali nchini, BRELA wameamua kushirikiana na chama cha wafanyabiashara na wenye viwanda na kilimo Tanzania (TCCIA) ili kuwasaidia kushawishi wajasiriamali kuanzia ngazi ya vijiji, wilaya na mikoa.
“Kuchaguliwa kwa TCCIA kumetokana na wao kuwa na mtandao mpana wa kielektroniki unaounganisha ofisi zao wilayani takriban mikoa yote ya Tanzania.
“Kupitia utaratibu huo, gharama za usajili wa jina la biashara ni Sh 6,000 ambazo wateja hulipia na kupatiwa stakabadhi za BRELA na TCCIA inatoza kiasi kidogo cha fedha Sh 2,000 kwa kila jina la biashara kwa ajili ya huduma za kiutawala ikijimuisha gharama za utumaji wa maombi hayo ofisi kuu ya BRELA,” alisema Bosco.
Aidha kwa upande wa usajili wa makampuni ada ya usajili inayotakiwa kulipwa inategemeana na kiasi cha mtaji mteja anachoandika kwenye katiba ya kampuni anayotarajia kuisajili. Gharama yake inaanzia Sh 50,000 kwa mtaji unaoanzia Sh 20,000- Sh500,000, mteja atalipia Sh 300,000 kwa mtaji unaoanzia Sh 30,000,000.
Katika hatua nyingine kaimu meneja huyo ameweka wazi kuwa kwa sasa kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia BRELA wanapokea maombi ya kusajili biashara na kampuni kwa kutumia njia ya mtandao, mteja anatakiwa kuingia kwenye tovuti ya BRELA ambayo ni www.brela-tz.org na kuangalia orodha ya makampuni yote yaliyosajiliwa Tanzania na kufanya upekuzi wa majina ili kutambua iwapo jina la biashara analotaka kusajili limeshasajiliwa au la, kabla ya kutuma maombi ya kusajili.
Aidha fomu zote za usajili zinapatikana katika tovuti hiyo ya BRELA pia wameweka katiba mfano inayojulikana kwa lugha ya kiingereza ‘Memorandum and article of association’ ambapo mteja anaweza kuichukua na kutengeneza katiba yake ya kusajili kampuni bila gharama yoyote.
BRELA ilianzishwa na kuzinduliwa rasmi Desemba 9, 1999 chini ya wizara ya viwanda na biashara kwa sheria ya wakala za Serikali namba 30 ya mwaka 1997. Ambapo majukumu yake makuu ni kusajili makampuni; kusajili majina ya biashara; alama za bisahra na huduma; kutoa hataza-Uvumbuzi kwa muda maalum (Patents of inventions) na kutoa leseni za viwanda na kusajili viwanda.
HAFIDH KIDO    
10 Julai, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA


No comments:

Post a Comment