Tuesday, July 2, 2013

Habari picha na maneno mkutano mkuu wa Coastal Union June 30, 2013.


 Klabu ilikuwa na shamrashamra sana mpaka wazungu walikuja kununua jezi ishara ya kulikubali chama.

 Hakika ilikuwa siku ya kupendeza kwa maana magari, pikipiki na baskeli zilijaa mtaa mzima wa 11.

 Viongozi kwanza walikutana kujadili kuhusu suala lililoanza kusumbua vichwa vya wanachama, yaani wenye kadi ya uanachama waruhusiwe ama wasiruhusiwe kwenye mkutano.

 Umewaona hawa, walichokuwa wakishikilia ni hilo gazeti la Mwananchi ambalo liliandika kila mwanachama ahudhurie awe na kadi ama asiwe na kadi. Ila baadaye viongozi walitumia hekima na kuamua kila mwenye uwezo wa kulipia siku hiyo basi afanye hivyo.

Kassim Siagi katibu wa Coastal Unio (mwenye sahti la mistari) akiwa na meneja wa timu Akida Machai wa kwanza kushoto pamoja na wanazi wengine wa timu wakiingia ukumbi wa mkutano siku ya jumapili.
 Hilal Hemed mchezaji wa zamani wa Coastal Union wa kwanza kulia, akisubiri kuhakikiwa kadi yake ya uanachama.

 Mwenyekiti wa Coastal Union Hemed Hilal 'Aurora' akiwa nje ya ukumbi wa mkutano na wasaidizi wake.

 Watoto hawa ndiwo watakaokuwa wanahistoria wa timu maana wameanza kufuatilia mwenendo wa timu mapema.

 Pichani kutoka kulia unaonekana uso wa Tafa Boy, Hussein Chusse, Bawazir, Kiraka, Mwenyekiti Aurora na Ubinde.

 Mkutano ukiwa umeanza na hapa wanachama wanaomba dua na kukumbuka waliotangulia mbele ya haki.


 Pichani anaonekana Mzee Shossi (springit) wa kwanza kulia mwenye miwani ambaye alikuwa golikipa tishio wa Coastal Union, kilio chake kikubwa ni kusahauliwa kwa wazee wa timu, lakini mwenyekiti amemuahidi wataandaliwa utaratibu maalum wa kukumbukwa.

Mabingwa wa soka Tanzania mwaka 1988 Coastal Union 'Wagosi wa Kaya' kutoka mjini Tanga wamefanya mkutano wao mkuu kwa mafanikio baada ya wanachama kukubaliana kitu kimoja tu ‘msimu ujao ushindi lazima’.
Muda mwingi ulitumika kusoma ripoti ya mapato na matumizi kwa msimu uliopita hasa vikiangaliwa vipengele vya mafanikio na pale tuliposhindwa kutokana na matatizo ya fedha. Katibu mkuu wa Wagosi wa Kaya Kassim Siagi, alipokuwa akitoa taarifa ya mapato na matumizi kwenye mkutano huo uliofanyika jumapili June 30 ambao umevuta hisia za mashabiki wengi wa klabu hiyo tangu miaka 1990 ilipokuwa ikiwika kwenye medani ya soka, alisema wanachama hawana budi kuichangia klabu yao ili kutimiza malengo ya kutwaa ubingwa msimu ujao.
"Mkumbuke leo Juni 30, ndiyo tunakamilisha kalenda yetu ya mwaka hivyo jiandaeni kulipia ada za uanachama ili kutunisha mfuko wa klabu kwani bila fedha za uhakika hatuwezi kutimiza hata nusu ya ndoto zetu za kutwaa ubingwa msimu ujao.
"Msimu uliopita tulitumia takriban mil 500, lakini vyanzo vya mapato havikufikia kiasi hicho ada za uanachama, fedha za wadhamini wa ligi pamoja na mapato ya mlangoni havikuzidi mil 300, mkumbuke klabu yetu haina mdhamini bali tuna wahisani ikifika siku wakichoka hawa wahisani tutashindwa kuendesha klabu," alisema Siagi.
Kwa upande wake meneja wa timu hiyo Akida Machai alihoji juu ya udhamini wa Simba Cement kwenye timu maana mbali ya kutoa basi dogo hakuna msaada mwingine wowote wanaoutoa kwenye timu mbali ya kuwatangazia bidhaa yao Tanzania na nje ya Tanzania.

Katibu alitoa majibu kuwa upo utaratibu unaofanywa kuangalia namna ya kuondoa nembo za kampuni hiyo ya Cement nchini Tanga, lakini ikiwa watakubali kuingia mkataba wa kuisaidia timu hiyo wataendelea kuziacha nembo za kampuni ya Cement. Lakini akaweka wazi kuwa mpaka sasa timu haina mdhamini zaidi ya wahisani u wanaoongozwa na kampuni ya betri za magari na matairi yaani Binslum Tyre.
Kwa mujibu wa mkurugenzi wa ufundi Nassor Binslum, huenda kikosi kikaanza msimu wa ligi Tanzania bara wakiwa na udhamini mnono kutoka kampuni kubwa ya vifaa vya michezo, Umbro Ltd.
Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika klabuni barabara 11 mjini humo, mkurugenzi wa ufundi Binslum, alisema tayari mazungumzo baina yao na kampuni ya Umbro yanafikia ukingoni na huenda msimu unaotarajiwa kuanza mwisho wa mwezi huu wakavaa jezi zilizotengenezwa na kampuni hiyo. 
"Mazungumzo yanafikia ukingoni na Umbro, ni kampuni kubwa ya vifaa vya michezo ndiwo wanaowavalisha Manchester City na timu ya taifa ya Uingereza hivyo tunatarajia msimu ujao kuvalishwa na Umbro kuanzia jezi, viatu, soxy, mipira, mabegi ya kubebea vifaa vya mazoezi na nguo mpaka beji ya nahodha kwa kifupi kila kitu cha mchezaji.
"Tumebakisha kipengele kimoja tu cha maakubaliano kuhusu kununua jezi za mashabiki elfu thalathini kwa bei ambayo wamepanga wao ingawa tunaiona kubwa lakini hatutashindwa kufungua mazungumzoa tena ili mambo yaende sawa maana wameshatutumia mfano wa jezi watakazotuvalisha, wanachosubiri ni jibu kutoka kwetu kuwa wazitengeneze," alisema Binslum.
Baadhi ya wanachama walisuguana sana juu ya uhalali wa katibu mkuu wa timu kuteua wanachama kwa nafasi mbalimbali za kiutendaji, lakini hali ya hewa ilirejea baada ya kunukuliwa vipengele katika katiba ya timu ambavyo vinaonyesha kumpa nafasi katibu kuteua na hata kuajiri.
Katika hatua nyingine wajumbe wawili wa kamati ya utendaji walipigiwa kura ya kutokuwa na imani nao baada ya kushindwa kutekeleza wajibu wao wa kiutendaji.
Naye mwenyekiti wa klabu hiyo kongwe iliyoanzishwa mwaka 1948, Hemed Hilal 'Aurora' alisema kauli mbiu ya mwaka huu ni 'Coastal Union bingwa' kwani awali walipokuwa wakitoa kauli mbiu za kushika nafasi tatu za juu walikuwa wakijipima ikiwa wataweza mikiki ya ligi kuu baada ya kukaa nje ya ligi kwa takriban muongo mmoja.
"Mtakumbuka huu ni msimu wetu wa pili tangu turudi ligi kuu hivyo tayari tumejifunza mbinu nyingi hasa ikizingatiwa miaka ya nyuma ligi haikuwa na ushindani mkubwa kama ilivyo sasa, zamani ligi iliendeshwa bila kutumia gharama kubwa lakini sasa bila pesa klabu si tu inashuka daraja lakini ianweza kufa kabisa na ndiyo maana tunaweka wazi kuwa msimu huu kauli mbiu yetu ni 'Ubingwa' nadhani mmeona usajili tulioufanya," aliweka wazi Aurora.
Coastal Union 'Wagosi wa Kaya' ni miongoni mwa klabu zilizoanzisha ligi ya taifa na baadaye ligi kuu mwaka 1965 ambapo klabu nyingine ni Sunderland sasa inaitwa Simba SC, Cosmo Politan, Dar es Salaam Young Africans na African Sports ya Tanga. Mwaka 1988 ilikuwa na kikosi imara kilichoiletea heshima kubwa ya kuwa wafalme wa soka Tanzania na kupeleka ushindani mkubwa katika michuano ya Afrika Mashariki.
Itakumbukwa kwa miaka ya 1970-80 Coastal Union ilikuwa ni timu iliyoleta ushindani mkubwa katika soka mpaka kuifanya Tanga kuwa mkoa wa pili wenye ushindani wa soka Tanzania baada ya Dar es Salaam.
COASTAL UNION
1 Julai, 2013
TANGA, TANZANIA

No comments:

Post a Comment