Tuesday, July 2, 2013

Kutoka familia ya Barack Obama Kogelo, Kenya



Si rahisi kuingia katika eneo la Kogelo,unahitaji ruhusa ya viongozi wa Serikali Siaya
Kisumu- Ni saa tatu asubuhi, Mkoani Nyanza eneo la Kisumu, ulio kando kando ya Ziwa Victoria, una hali ya joto kiasi.
Wakazi wa hapa wanaendelea na shughuli zao za kila siku zaidi hasa za  kibiashara.
Safari ya kuelekea Wilaya ya Siaya ilianza muda ya saa nne na dakika kumi asubuhi.
Kwa kuwa magari yanayoelekea kijijini Kogello  yapo lukuki, haikuchukua muda kabla ya kufika.
Wenyeji wakanieleza kuwa ili nifike huko ninapokwenda natakiwa nishuke eneo liitwalo Ndori.
Ninaposhuka, sina budi kuchukua usafiri wa pikipiki (bodaboda) ambao utanifikisha Kijiji Kogelo ambako ndiko hasa ninapokwenda… hapo ndipo ulipo ukoo wa  baba mzazi wa rais wa taifa kubwa duniani la Marekani, Barack Hussein Obama.
 Hakuna dereva asiyefahamu mahali hapo, ni maarufu pia panaheshimika  pengine kuliko unavyoweza kufikiri.
Ninaposhuka katika bodaboda, mbele yangu, natazamana na lango kubwa la chuma ambalo pembeni kuna kibanda kidogo.
Haikuchukua zaidi ya dakika moja kabla ya askari waliovalia sare za bluu bahari na bluu iliyokaribia kuwa nyeusi kutoka katika kibanda hicho na kunifungulia lango hilo.
Wananisalimu na kisha wananiuliza shida iliyonifikisha mahali hapo. Ninajitambulisha, huku nikitakiwa kutoa vitambulisho vyangu vyote na baada ya kuwaeleza lengo langu wananihoji iwapo nimepata ruhusa kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Siaya, Mkuu wa Kituo cha Polisi Kogelo na msemaji wa familia ya Rais Barack Obama.
 Ninawajibu kuwa nimepata ruhusa kutoka kwa msemaji wa familia hiyo, ambaye ni  baba mdogo wa Rais Obama, Said Obama.
Hata hivyo, wananitaka niwahakikishie hilo kwa kumpigia simu Said. Ninafanya hivyo na  baada ya Said kuzungumza nao, ninaruhusiwa kuingia.
 Ninakutana na bibi yake Rais Obama, Mama Sara Obama, ambaye ni mke wa tatu wa babu yake Rais Obama.
“Rais   ni Mluo. Baba yake alikuwa  Mluo pia.  Hapa ndipo kwa baba yake, na hii ndiyo asili yake,” anaanza simulizi yake bibi  huyo (Mama Sarah), kama alivyozoeleka na wengi.
Anasema, yeye si mama mzazi wa Obama Mkubwa (Hussein) ambaye alimlea kwa kuwa mama mzazi   wa Obama Mkubwa,  alifariki wakati Obama akiwa na umri wa miaka tisa.
Anasema baba yake Rais Obama (Hussein) alizaliwa Aprili, 1936 akiwa ni mtoto wa kwanza wa Mzee Hussein Onyango Obama na Habiba Akumu Obama.
Kabla ya kuendelea na simulizi zaidi, anasema: “Obama alikuwa ni mwerevu kuliko kawaida.”
 “Mzee Onyango alikuwa mkali mno.  Aliwachapa watoto wake kwa mjeledi pindi walipokosea. Obama alikuwa mkaidi, lakini mwenye akili nyingi,” anasema.
Sarah, anakumbuka wakati mwingine ambapo Obama Mkubwa, alipotoweka nyumbani bila kuhudhuria shule kwa siku kadhaa, na hata aliporejea, bado alishika nambari moja katika mitihani.
Ninazungumza na Said Obama.  Huyu ni baba mdogo kwa Rais Obama na kaka kwa Obama Mkubwa.
 Baba yake Rais
 Said anasema, kaka yake, yaani Obama Mkubwa kama anavyoitwa alisoma shule ya msingi Ng’iya, kabla ya kuchaguliwa kujiunga na shule ya sekondari ya watoto wenye vipaji maalum ya Maseno.
“Alikwenda  kusoma Marekani kwa mpango wa taifa ( Kenya) kuwapa elimu vijana wa Kiafrika (Africanization) baada ya uhuru. Alichaguliwa kwa kuwa alikuwa mwerevu mno,” anaeleza Said.
Huko Marekani, mzazi huyo wa Rais Obama, alipata Shahada ya Kwanza katika Uchumi Chuo Kikuu cha Hawaii nchini Marekani. Kisha alipata elimu zaidi katika Chuo Kikuu cha Harvard kabla ya kurudi kuitumikia nchi yake, Kenya.
“Aliporudi nchini mwake mwaka 1965, alifanya kazi serikalini katika Wizara ya Usafiri, na baadaye  kama mshauri mkuu wa uchumi,  Wizara ya Fedha na pia alifanya kazi  katika kampuni mojawapo ya mafuta,” anaeleza Said.
 Yaliyomfika wakati huo
Baada tu ya mwanasiasa maarufu wa Kenya, Tom Mboya kuuawa, Obama Mkubwa aliachishwa kazi.
“Kuanzia hapo alianza kuwa mlevi kupindukia. Alipata ajali ya gari akajeruhiwa mguu. Alikaa hospitali kwa zaidi ya mwaka mmoja,” anaeleza Said na kuongeza:
“Hata alipokwenda Hawaii mwaka 1971 kumwona mwanaye (Rais Obama), tayari mguu wake ulikuwa na matatizo.”
Said anaeleza zaidi na kusema, mikosi haikuishia hapo, alipata ajali nyingine ya gari ambayo ilimpotezea miguu yote miwili mwaka 1972.
 Ajali ya tatu, ilitokea mwaka 1982 akiwa na umri wa miaka 46. Hapo ndipo alipoteza maisha.
Maombolezo ya Obama kwenye kaburi la baba yake
Mama Sarah, anasema kwanza haikutegemewa kama Rais Obama angerudi kuitafuta asili yake.
Lakini, jambo la pili, wao hawakutegemea kama angerudi baadaye akiwa Gavana  wa Jimbo la Illnois (Marekani), na ajabu zaidi, hawakutarajia kuwa, angekuwa rais wa taifa kubwa kama Marekani.
“Mwaka 1987 alifika hapa akiwa na umri wa miaka 26. Hatukutegemea, ilikuwa imepita miaka mitano tu tangu baba yake afariki,” anasimulia Sarah.
Obama alifika, na hakusita kulala katika nyumba ya matope,(wakati huo)  aliyoishi baba yake.
Sarah anasema, Rais Obama alipoliona kaburi la baba yake, alilia mno. Hakutaka kuondoka kaburini mpaka dada yake alipokwenda kumtoa kwa nguvu.
“Alipofika ilikuwa ni muunganiko mpya wa familia. Aliuliza mengi kuhusu baba yake, kuhusu asili yake na mila na taratibu zetu,” anaeleza Sarah.
Mama Sarah anasema, Obama alipofika hapo alifanya shughuli za kijijini kama kawaida, alibeba magunia ya mahindi, akalisha ng’ombe na alishika jembe kwa mkono wake mwenyewe.
“Unaona picha ile , amebeba gunia la mahindi akisaidia kazi za shambani alipokuja mwaka 1987,” anaeleza.
Ujio wa Obama mwaka 2006
Mmoja wa wajukuu wa  Mama Sarah, Nelson Ochieng anasema Rais Obama alifika tena Kenya mwaka 2006 akiwa tayari ni mtu mwenye cheo kikubwa Marekani. Hakuacha kutembelea kijijini Kogelo.
“Alifika na kama kawaida alikuja hapa akasikiliza matatizo yetu na kuahidi kuyatatua ingawa safari ile, hakulala katika chumba chake cha kawaida (ananionyesha kwa kidole chumba alicholala Obama alipokuja 1987)
Katika kitabu cha Rais Obama, (Dreams From my Father), rais huyo amefafanua na kusema,mama yake Ann Dunham alikutana na baba yake katika Chuo Kikuu cha Hawaii mwaka 1960.
Wawili hao walifunga ndoa Februari 1961 na Rais wa Marekani aliyetabiriwa na Martin Luther King Jr, alizaliwa Agosti 4, mwaka huo huo.
Mwananchi.

No comments:

Post a Comment