Tuesday, July 2, 2013

Nyuma ya pazia la ziara ya Obama Afrika.


Jana niliulizwa na rafiki yangu Leonard Kituyi kutoka Kenya juu ya ufahamu wangu kwa ujio wa Rais wa Marekani nchini Tanzania aliniuliza hivi: Kama mwandishi wa habari,unamtazamo upi kuhusu ziara ya rais wa Marekani Barack Obama nchini Tanzania, ni yapi matarajio ya watanzania kwenye ziara hii?

Unadhani Obama kususia Kenya kutokana na uzito wa kesi za ICC, kuna athari zozote kwa nchi hii?
Na haya ndiyo yalikuwa majibu yangu: Kituyi nimepata kusema mara nyingi kuwa Marekani hawana adui wa kudumu wala rafiki wa kudumu. Ziara itakuwa na mafanikio kwetu kwa muda mfupi lakini kwa wenzetu kwa maana ya Marekani itakuwa na muda mrefu. Tanzania ina rasilimali ambayo inatumika kuendesha uchumi wa dunia (Oil, gas na madini). Marekani wanataka kushikilia ufalme wa dunia hivyo huzunguka kila kipembe kuangalia rasilimali nilizotaja. Kikubwa kilichosababisha ziara ya Obama ni baada ya mpinzani wao kiuchumi (China) kufanya ziara mwezi uliopita.

Hivyo wanachotaka kujua ni nini china wamekubaliana na Tanzania (sizungumzii makubaliano ya hadharani) watajuaje hayo? Ni kupitia majasusi ambao wametumwa tangu mwezi uliopita kwa mwamvuli wa kuangalia usalama wa Rais Obama. Kitu kingine wanataka kuangalia suala la madini ghali kwa sasa urani 'uranium' ambayo nchi ya Iran mahasimu wakubwa wa Marekani walipata kuingia katika mazungumzo na Tanzania. Nina mengi ila kwa leo turidhike na haya maana ziara ya Obama haikuja kumkomboa mtanzania maskini bali kuja kufuta nyayo za Rais wa China. Kuhusu Kenya na ICC si kweli, Obama hajaisusa Kenya ila hakuna kipya kitakachompeleka kenya. kifupi ziara ya Kenya haina faida kwa Marekani, kwasababu mbili: moja Kenya wanafuata mfumo wa kibepari hivyo si tishio kwao, pili rasilimali zilizo kenya kama madini na mafuta si ya kiasi kikubwa wanachokitaka wao. Na pengine baada ya kufanikiwa kuweka kituo cha kijeshi (military base) Tanzania: Ambayo ni moja ya mikakati ya siri ya ziara hii hapo watakuwa wakiingia Kenya, Uganda na nchi nyingine jirani bila kutumia ziara za Rais wao.



HAFIDH KIDO
JULAI 2,2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA

No comments:

Post a Comment