Tuesday, July 2, 2013

Wakati Mzee Mandela akipigania roho yake Misuguano yazuka kuhusu wapi atazikwa.

 Mjukuu wa Nelson Mandela ndugu Mandla Mandela ambaye ndiye chifu wa ukoo wa Mzee Madiba.

Haya ndiyo makaburi ya famila ya Mzee Mandela yaliyozua vurugu kubwa za kifamilia.


Huku rais mstaafu wa Afrika Kusini Nelson Mandela akiendelea kuugua mjini Pretoria, jamaa zake wamejikuta kwenye malumbano kuhusu mgogoro ambao umejitokeza wazi kwenye vyombo vya habari.
Badhi ya jamaa za familia wamemshtaki mjukuu mkubwa wa Mandela, Mandla, katika juhudi za kutaka kufukua maiti za wanawe watatu wa Mandela ili wawazike katika makaburi ya Qunu, ambako Mandela anataka azikwe.
Na Mgogoro kuhusu kutaka kuwafukua wafu hao ni ishara ya mgawanyiko mkubwa katika familia kubwa ya Mandela, wake zake watatu , watoto sita na wajukuu 17 na vitukuu
12 . Kulingana na baadhi ya viongozi wa kijamii, wakati familia yake inapoendelea kuzozana , roho ya Mandela haiwezi kuwa na amani.
Jamaa kumi na sita wa familia ya Mandela pamoja na viongozi wa kijamii wiki jana walipewa idhini ya muda na mahakama kufukua maiti hao na kuwapeleka katika mji wa
Qunu, ambako makaazi ya Mandela yapo.
Lakini Mandla Mandela, ambaye kulingana na vyombo vya habari, alihamisha maiti hao umbali wa kilomita 22 kutoka mji wa wa Qunu hadi nyumbani kwake eneo la Mvezo mnamo mwaka 2011, anapinga uamuzi huo.
Maiti hao ni pamoja na Makgatho Mandela, babake Mandla aliyefariki kutokana na ugonjwa wa ukiwmi, mwaka 2005 pamoja na ndugu zake, Thembekile, aliyefariki katika ajali ya barabarni na mwanawe wa kwanza aliyefariki akiwa na miezi tisa, walizikwa kwenye makaburi yaliyokaribiana.
Watatu hao walifukuliwa bila ya idhini ya familia yote ya Mandela na viongozi wa kijamii wa ukoo wa AbaThembu ambao pia ni ukoo wa Mandela.
Wanaamini kuwa roho ya Mandela, ina sumbuka hivi sasa kutokana na mzozo kwenye familia yake na ndio maana roho yake haikatiki.
Watu kumi na sita ni mashahidi katika kesi ya kuomba mahakama idhini ya kufukua maiti hao, akiwemo mkewe Mandela, Graca Machel, mwanawe Mandela Makaziwe na viongozi wakuu wa ukoo wa AbaThembu.
Kinachohojiwa zaidi kwenye mzozo huu ni nani atachukua nafasi ya Mandela kama kiongozi wa familia?
Viongozi wa kijamii walimteua Mandla kama kijana mwenye umri mkubwa zaidi kuweza kuchukua nafasi ya Mandela, na kumkabidhi jukumu la chifu Zwelivelile wa ukoo wa Thembu.
Pia ni mbunge katika chama tawala ANC.
Lakini wengi katika familia wanaonekana kutopendezwa na miendeno yake, akiwemo Makaziwe, mwanawe Mandela wa kike.
Mpango wake wa kutaka kufungua makavazi katika shamba ambalo makaburi hayo yapo, imewaacha wengi vinywa wazi katika familia hiyo.
Katika mgogoro mwingine, wanawe wa kike na wakubwa wa Mandela, Makaziwe na Zenani wameenda mahakamani wakitaka kuwanondoa wasaidizi watatu wa Mandela kutoka katika kampuni za baba yao.
Wawili hao wanataka umiliki wa kampuni hizo ambazo ni za thamani ya mamilioni ya dola.
Wiki jana Makaziwe aliandaa mkutano wa dharura wa kijamii ambapo inasemekana Mandla alilaaniwa vikali kwa kuhamisha maiti za jamaa zake bila idhini.
Baadhi wanaamini kuwa Mandela lazima asuluhishe mzozo huu kabla ya ya kifo chake.
Moja ya imani za kitamaduni nchini Afrika Kusini ni kuwa mtu huwa hafi wakati ana mambo yanayomsubiri kuyasuluhisha.
Baadhi wanaamini kuwa badhi ya mambo ambayo bado hajakamilika kwa Mandela ni kuweza kusuluhisha migogoro hii ndani ya familia pamoja na kuipatanisha familia take.
Mandela alistahili kuafikiana na familia yake kabla ya kufukua miili za jamaa zake.
Wajumbe wa ukoo wa AbaThembu, wameandaa mkutano wa dharura mjini Qunu baadaye mwezi huu kusuluhisha mizozo hiyo.
BBC SWAHILI

No comments:

Post a Comment