Monday, July 8, 2013

Watoto wa Mandela wadaiwa kuuza haki ya mazishi kwa vyombo vya habari vya magharibi.



Gazeti la uchunguzi la The Sunday Independent la Afrika Kusini limesema mtoto mkubwa wa Mandela, Makaziwe Mandela na binamu yake, Ndileka wapo kwenye mipango ya kupata fedha kutoka kwa Televisheni ya CNN wakati wa mazishi ya baba yao.
Mmoja wa maofisa wa Shirika la Utangazaji la Afrika Kusini (SABC) ambaye pia alishiriki mkutano huo alikaririwa akisema kwamba Makaziwe na Ndileka walikaa katika mkutano wa siri mwishoni mwa Juni mwaka huu pamoja na maofisa wa shirika hilo na Ofisi ya Rais ili kupanga jinsi ya kuyarusha matangazo ya mazishi ya kiongozi huyo kwa vyombo vya kimataifa.
Hata hivyo, Mwakilishi wa CNN Johannesburg, Kim Noorgard alisema hafahamu chochote kuhusu suala hilo.
The Sunday Independent liliwatafuta viongozi wa CNN wa makao makuu jijini Atlanta, Marekani lakini hawakupatikana kuzungumzia suala hilo.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Makaziwe alikataa kuzungumza lolote na kumtaka mwandishi kuwataja maofisa wanaoelezwa kwamba walizungumza nao.
“Hadi uniambie nani amekwambia habari hii ndipo nitakujibu unachotaka kufahamu,” alisisitiza Makaziwe.
“Niambie nani kakwambia,” alizidi kuomba. “Huo ulikuwa mkutano wa siri na sidhani kama kuna kitu cha kuongelea hapo.”
Ndileka naye alikataa kuzungumza lolote kuhusu mkutano ule.
Ripoti ya mkutano huo ilieleza kuwa majadiliano makuu yalikuwa ni kwa namna gani mazishi ya Mandela yatarushwa hewani lakini watoto wa Mandela walilazimisha CNN wapewe haki ya kurusha matangazo ya mazishi hayo.
Mmoja wa maofisa hao aliyehudhuria mkutano aliyaponda mazungumzo hayo na kusema kuwa hayafai kutoka katika vinywa vya wanafamilia ambao wanazungumzia kifo cha baba yao wakati akiwa bado yupo hai.
“Wanataka kupata fedha kutoka mashirika ya kimataifa na ndiyo maana wanapanga mipango hiyo. Kama Serikali hatuna cha kufanya kwa sababu inaonekana wanafamilia tayari wana mipango yao,” alisema afisa huyo.
Ilibainika kuwa tayari CNN walikuwa wameshafanya mazungumzo na wanafamilia hao na kukubaliana.
Mandla avuliwa uchifu
Mfalme wa Kabila la Thembu, Zwelibanzi Dalindyebo amemwondoa Mandla Mandela katika wadhifa wake wa uchifu.
Mandla anatuhumiwa kuivuruga familia yake baada ya kuhamisha makaburi matatu ya watoto wa babu yake, Nelson Mandela.
Alihamisha makaburi hayo kutoka Qunu na kuyapeleka katika Kijiji cha Mvezo mwaka 2011 yaliko makazi yake.
Miili ya watoto hao ilirudishwa Qunu baada ya familia ya Mandela kwenda mahakamani kuomba na kukubali kumlazimisha Mandla airudishe miili hiyo.
Mfalme Dalindyebo alisema kuanzia sasa Mandla hataruhusiwa kujihusisha na masuala ya kabila hadi aombe radhi.
“Kitendo alichofanya kimeudhi watu wengi wa kabila letu na hatutaki kumuona akijihusisha na masuala ya familia ya Mandela.”
Mandela amelazwa hospitalini mwezi mmoja sasa na mvutano wa familia yake umeishtua dunia.
Mandla alitaka Mandela azikwe Mvezo kwa maelezo kwamba ndiko alikozaliwa lakini habari nyingine zinadai kwamba alitaka kunufaika kifedha kutokana na watu ambao wangekwenda kutembelea kaburi la Mandela.
Mandela aliacha wasia kuwa atakapofariki azikwe karibu na makaburi ya wanae.
MWANANCHI

No comments:

Post a Comment