Monday, December 9, 2013

HINA/HEENA. Ni nini?




MTI WA MHINA.

Muhina ni Mti mdogodogo kiasi ambao hufanana sana na Mchongoma kwa umbo na ambao ukikua una majani mengi sana. Mti huu humea mwituni lakini pia watu wa zamani (hasa wa Pwani ya Tanga na Zanzibar) bado wanaupanda uani katika Majumba yao.

Muhina hutundwa (huchumwa/hukatwa) majani yake, yakakaushwa juani na kisha ukachungwa na kutiwa ndani ya "madebe kasha" kisha kupelekwa kwenye mji kuuzwa. Watu hununua kwa kipimo kulingana na matumizi.

TAMADUNI YA AZZAL NA ENZI.

Unga wa hina hutiwa ndani ya bakuli ukaongezwa chai ya rangi na ndimu kisha kupakwa, Hina hupakwa kwa kutumia vidole vya Mikono au Kijiti japo kwa siku za karibuni kuna vitendea kazi mbalimbali ambavyo hutumika rasmi kupakia. Hina/Heena ina Asili ndefu mno katika taratibu za Watu wa Pwani ya Bahari ya Hindi kuanzia Bara Hindi, Uarabuni, Afrika Kaskazini mpaka Upwa wa Pwani ya Afrika Mashariki.

Hina/heena ipo tangu jadi sana, ikihusisha Michoro na nakshinakshi zenye kuvutia kuangalia na kumpendezesha mpakaji, ikitumika upande wa bara Arabu, India, Misri, Zanzibar, Comoro, Tanga, Mombasa na Dar es salaam kwa kujipamba, ni Miongoni mwa mapambo na tamaduni za asili sana ya watu wa Pwani.

DAWA MUJJARAB.

Lakini hapa kwetu (Tanzania) pia Hina/Heena hutumika kama dawa kwa baadhi ya jamii na imeleta mafanikio makubwa tu katika matumizi yake.

Wataalam wengi wa Tiba Asilia wamekuwa wakiitumia Hina kama dawa ya kupoza presha ikiwa juu, uti wa mgongo, maumivu ya viungo, miguu na pia kwa watu wazima ikitumika kubadilisha rangi za nywele zao (Kwa Taratibu za kiislam Wazee wenye mvi hawaruhusiwi kupaka nywele zao rangi nyeusi bali huruhusiwa kupaka Hina).

SHEREHE NA FURAHA.

Hina mara nyingi huashiria Furaha, pongezi na sherehe,Katika sherehe zetu za waswahili tuko na heena party. Bwana harusi hufinikwa na kitambaa na kupakwa heena kwenye mikono yote na mwili.

Pia Mwanamke anayeolewa hupambwa na kunakshiwa kwa Michoro mbalimbali ya Hina na Piko mwilini mwake ili kumfanya avutie zaidi kwa Mumewe, kwenye matukio ya Harusi ukiacha Bibi Harusi lakini pia hata Wanawake wengine nao hujiremba na kujipamba kwa Hina.

Mama Mjamzito anapojifungua pia hupaka Hina wakati akiwa tayari kukabiliana tena na Mumewe, hilo hufanyika ili kuongeza mvuto mwilini mwake kwa kuwa anakuwa ana muda Mrefu hajakutana naye.

Hina hupakwa pia wakati wa Sikukuu, hasa Eid. Ni jambo la Kawaida kuwakuta Watoto na Wanawake wakirembwa na kupambwa kwa Hina kuelekea Sherehe za Sikukuu za Eid.

HESHIMA YA MATUMIZI.

Hina ni pambo zito sana na lenye maana kubwa kwetu siye watu wa Pwani, Hina ni Kichocheo Kizito cha Mapenzi, kachumbari yenye mshawasha na kipambo chenye kuchochea Nakshinakshi na kuonyesha Furaha na Pongezi.

hivyo kama ilivyo kwa kitu chochote cha Kimila na Kitamaduni ambacho ni kizito na chenye Maana kubwa kama hiki lazima kiwe na Masharti, Heshima na Kanuni zake za Kimatumizi.

Hina inapakwa na Watu wa Rika na Jinsia zote, watoto mpaka watu wazima, Wake pamoja na Waume. Lakini kuna tofauti kubwa katika Aina ya Upakaji, Muda wa Kupakwa na sababu za kupaka.

WATOTO, MABAROBARO NA WANAWARI.

Watoto wanaopakwa Hina hawachorwi maua ya aina yoyote, Bali hupakwa tu Hina tupu kawaida kwenye Nyayo na Mikono zaidi wakichorwa Machenza. Watoto hupakwa hina mara nyingi usiku wa kuamkia siku ya Eid (Eid El Hajj au Eid El Fitr), mikono na miguu inafungwa majani ya mnyonyo, analala nayo. Hawa mara nyingi wanakuwa ni watoto wa kike na wa kiume ambao wanakuwa hawajabalehe.

Watoto wa kiume wakishakuwa wa kubalehe (Mabarobaro) hawapaki hina mpaka siku ya harusi. Ila watoto wa kike waliobalehe (Wanawari) watapaka hiyo hina isiyo na maua mikononi na miguuni siku za sikukuu hata wakishavunga ungo.

Makabila tofauti ya Pwani yametofautiana juu ya hili la kuruhusu Wanawari kupaka Hina kaika baadhi ya sehemu au kuwakataza kabisa, Wanubi na Baadhi ya Makabila ya Tanga wamewaruhusu lakini kwa ile Hina isiyo na Maua na hupaswa kupakwa Miguuni na Mikononi tu.

Makabila Mengi ya Visiwa vya Comoro, maeneo ya Zanzibar na hata Tanga yamezuia kabisa Wanawari kupaka Hina (Japo huruhusu kwa watoto wadogo wa Kike). Mila na Desturi haziwaruhusu wanawari kupaka hina madhumuni hasa ya kuwazuia kupaka hina ikiwa ni kuwaepusha na jicho la wanaume Wakware.

AJUZA NA VIKONGWE.

Uzee huja na mengi, ukiondoa Busara, Hekima na ile dhana ya kuona mengi lakini pia hudhoofisha viungo vya Mwili na kuvifanya vichushe, Miongoni mwa vinavyozoofika zaidi ni Nywele na Ndevu ambazo huota Mvi na kubadilika kabisa rangi yake ya Asili.

Vikongwe hupenda sana kuitumia Hina kupaka kwenye Videvu vyao (Japo Wazee wengi wa Mjini wanaopaka Videvu Hina ni "Manguru" ukiacha wale Wachache ambao ni Wanasunnah).

Nyanya zetu nao hupaka Hina vichwani mwao ili kuhuisha Nywele zao na kuzifanya zipendeze hata wakiwa uzeeni, Wapo wachache ambao huendeleza asili yao ya kujiremba na kuipaka Miguuni, Mikononi, Mapajani nk (Japo wengi wao hawafanyi hayo mambo ya Kisichana ukiaondoa wale wachache wenye "Surua").

HARUSI.

Siku ya harusi sasa kwa mara ya kwanza kabisa binti ndio anapakwa hina yenye maua na urembo, ikinakshiwa kwa piko na kuenezwa kuanzia kwenye nyayo za Miguu mpaka kifuani mwake.

Na siku ya bi harusi kupakwa Hina/Heena huwa special, kunakuwa na mwendelezo wa shamra shamra za harusi, maana nazo zina taratibu zake, iko siku nitawaambia kuhusu hili.

Siku ya hina kinamama wanacheza na kuimba, bi harusi akishamaliza kupakwa hina, anaachwa pale hina inakauka, sasa inabebwa sahani ya hina huku ikiwa imefunikwa vizuri, kwa nyimbo na mgoma inapelekwa kwa bwana harusi mtarajiwa.

Huko na yeye (Bwana Harusi) anakuwa amekaa na nduguze (mara nyingi wanawake) wanasubiri Hina kutoka kwa bi harusi, ikifika ile hina wa kwa mke watataka kumpaka bwana harusi na wa kwa mume watatoa pesa au zawadi yoyote kuwapa ili kijana wao asisilibwe hina mkono mzima, mara nyingi huishia kupaka kwenye kidole/vidole kidogo tu kama ada.

Basi hapo tena nderemo na vifijo na vigelele ndio shamra shamra za harusi hizo (Kiasili hili Jambo la kupaka Hina Bwana Harusi na Masingaji ni Mila ya Kinubi kutoka huko Sudan, Japo baadhi ya Makabila ya Pwani nao hufanya lakini mara nyingi Wanaume wanakataa kwa sababu za kuona haya na pia Dini).

MIIKO.

Lakini kikubwa sana ni kuwa hina ina maana kubwa sana katika mambo ya Chumbani, Nakshi na Maua yake huongeza Mvuto wa Pekee na wa Ajabu kati Umbo la Mwanamke. Binafsi Mwanamke akiwa amepaka Hina nakuwa na Hisia za Ziada sana Juu yake (Hahaha!.. Kuna Mijitu itakomalia Kipengele hichi tu).

Lakini Hina ina Miiko yake kwa wale wanaipaka, Kikawaida utakuta Mwanamke akishakuwa nyumbani kwake kwanza shurti apate ruhusa ya mume kupaka hina, sio kujipakia tu (Ila Mamzo za Suprise pia zimo).

Pili kwa wale walioolewa ni Mwiko Urembo wa Hina zao kuonwa na wanaume wa barabarani, tatu Mwanamke akiwa mjamzito hatakiwi kupaka hina maana shughuli yake hataiweza kama mume anajua maana ya hina na jinsi ya kuitumia, inashauriwa usubiri mpaka umalize kuoga nifasi uwe tayari kumpokea mume ndio sasa unapaka hina, ndio maana unaona kinamama wengi wanapaka hina wakitoka arubaini. Hapa nazungumzia hina kwa maana ya hina nyekundu.
Habari hii nimeitoa kwenye ukurasa wa facebook wa Watanzania Mashuhuri.

No comments:

Post a Comment