Tuesday, August 12, 2014

Madaktari waunda masikio toka ubavuni



MADAKTARI nchini Uingereza wametengeneza masikio kutoka ubavuni mwa kijana aliyezaliwa bila ya viungo hivyo muhimu.

Kijana huyo mwenye umri wa miaka tisa, Kieran Sorkin alizaliwa bila masikio na madaktari wamekuwa wakifanya majaribio ya mbinu mpya ya matibabu katika hospitali ya Great Ormond Street iliyoko jijini London.
Takwimu nchini Uingereza zinaonesha kuwa takriban watoto 100 huzaliwa bila kiungo hicho muhimu nchini humo, ambapo madaktari wanaita ugonjwa huo microtia.
Kieran, aliyezaliwa kama kiziwi hakuwa na masikio, alipozaliwa alikuwa na shimo mbili na ndewe tu badala ya masikio.
Tayari Kieran, anasikia baada ya upasuaji wa awali ambao ulimsaidia kupandikiza kifaa kinachomsaidia kupaza sauti ndani ya masikio yake.
"Ningependa watu wakome kuniuliza kwanini unakaa tofauti hivi, " alisema Kieran akiwa katika mtaa wa Hertfordshire.
Aliongeza kuwa, “nimefurahishwa sana kufanana na marafiki zangu, maana hata mimi ninafurahi kuwa sasa nitaweza kuvaa miwani na vifaa vya kusikizia muziki."
Mamake Kieran, Louise Sorkin alisema kuwa kijana huyo ni mchangamfu sana na alikuwa anasubiri kwa hamu kufanyiwa upasuaji wa kupandikiza masikio hayo.
"Sikuwa nafurahia watoto wenzake wakimkejeli kutokana na maumbile yake."
Asubuhi ya siku ya upasuaji huo Neil Bulstrode, alitengeneza masikio hayo na akapandikiza akitumia teknolojia ya kisasa ya kushona chini ya ngozi ya kichwa chake.
Wanasayansi hao wanasema kuwa walitumia mbinu mpya ya kukuza viungo hivyo.
Kieran alifurahishwa sana alipooeshwa masikio yake mapya siku tatu baada ya operesheni hiyo.
Chanzo: BBC Swahili

No comments:

Post a Comment