AJALI ya kuzama kwa Boti
mali ya kampuni ya Seagull
July 18, 2012 ilizua hali ya kwanini ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , baada
ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kukataa hoja ya kutaka kujadili suala la ajali
hadi pale taarifa kamili zitakapotolewa hivyo mjadala wa Bajeti ya Wizara ya
mambo ya Ndani uendelee.
Kutokana na ajali hiyo,
muda mfupi baada ya kipindi cha jioni kuanza, Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad
Rashid Mohamed alisimama na kuomba mwongozo kwa kutumia Kanuni ya 47(3)
kulitaka Bunge lipitishe Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya
Nchi kwa mafungu bila ya kutolewa ufafanuzi ili wabunge waweze kupata muda wa
kujadili tukio hilo .
Hata hivyo, Spika Anne
Makinda alipinga hoja ya Hamad na kutaka Bunge liendelee akieleza kwamba kanuni
hiyo imekuwa ikitumiwa vibaya na kwamba tayari ameshawasiliana na waziri husika
na kwamba taarifa kamili zitakapopatikana angelitaarifu Bunge.
Baada ya kauli hiyo
Spika Makinda aliruhusu shughuli za Bunge ziendelee na kumwita Silima kutoa
ufafanuzi wa hoja za wabunge.
Lakini wakati Naibu
Waziri huyo akielekea kutoa hotuba yake, wabunge wote wa CUF, Chadema na baadhi
wa CCM walitoka nje na kwenda katika Ukumbi wa Msekwa ili kupeana taarifa za
ajali hiyo na kupanga mikakati ya jinsi ya kutuma ujumbe wa haraka kwenda
Zanzibar kushirikiana na waokoaji.
Ukumbi huo uligeuka kuwa
wa maombolezo kwa muda baada ya wabunge wengi kuangua vilio pale walipopewa
taarifa rasmi za ajali hiyo.
Mbunge wa Wawi, Hamad
Rashid alieleza kwa ufupi tukio lilivyo na kwamba wangemwomba Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda awasaidie ndege ya Serikali ili waweze kwenda Zanzibar
kujumuika na wenzao katika tukio hilo .
Baada ya Hamad kumaliza
alisimama Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia ambaye alijaribu kuwatuliza wabunge
akisema kuwa, meli inaweza kuzama lakini watu wasipoteze maisha kutokana na
kuchukua muda, kauli ambayo ilipingwa na wabunge wengi.
Mbunge wa Mji Mkongwe
(CUF), Ibrahim Sanya alimshutumu Spika Makinda akisema, amekosa hisia na hajui
kwamba kuzama kwa meli ni janga la kitaifa.
“Kwa hili hata
nikikutana na Spika nitamwambia kweli ameniudhi. Sihitaji ubunge kama hali yenyewe ndiyo hii na tutapiga kura ya kutokuwa
na imani na Spika,” alisema Sanya.
Wakati hayo yakitokea,
katika Viwanja vya Bunge baadhi ya wabunge na mawaziri walionekana wakiwa
katika vikundi wakijadili suala hilo ,
huku wengine wakipinga uamuzi huo wa Spika.
Wakati hayo yakiendelea
katika Ukumbi wa Msekwa, Bunge lilikuwa likiendelea kumsikiliza Silima akijibu
hoja za wabunge na baada ya kumaliza, Spika Makinda alimwita mtoa hoja, Waziri
Nchimbi naye kujibu.
Lakini badala yake,
alitumia fursa yake kuondoa hoja ya Makadirio ya Matumizi ya wizara yake ili
kutoa fursa kwa Bunge kujadili ushiriki wake katika tukio la kuzama kwa boti
hiyo.
Dk Nchimbi alitumia
Kanuni ya 58 (5) ambayo inamtaka mtoa hoja kusimama na kutoa hoja ya kuondoa
mezani hoja yake kama kuna jambo la dharura.
“Mheshimiwa Spika,
natumia Kanuni ya 58 (5) ambayo inamtaka Waziri kusimama na kutoa hoja ya
kuondoa mezani hoja yake kama kuna jambo la
dharura,” alisema Dk Nchimbi.
Dk Nchimbi aliendelea:
“Ikumbukwe Mheshimiwa Spika, muda mfupi kabla ya kuingia hapa ndani uliniita
mimi na Naibu Waziri ukataka tukueleze hali ya ajali hiyo na kwa wakati huo
Kamishna wa Matukio Zanzibar alikuwa eneo la tukio. Sasa basi, kutokana na
agizo lako, ni imani yangu kwa muda aliotumia Naibu Waziri unatosha kuendelea
kufuatilia jambo hilo .”
Baada ya kutoa maelezo
hayo, Wabunge wote 49 waliokuwa wamebaki katika ukumbi walisimama kuunga mkono
hoja.
Baada ya hapo, Spika
Makinda aliwahoji na kwa kauli moja waliridhia kuahirishwa kwa kikao hicho
wakati huo ikiwa saa 11:31 hadi leo saa 3.00 asubuhi, huku akiitisha kikao cha
dharura cha Kamati ya Uongozi ya Bunge jana hiyohiyo kujadili suala hilo .
Akizungumza baada ya
kikao hicho cha Kamati ya Uongozi, Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel alisema,
limeamua kufuta kipindi cha Maswali kwa Waziri Mkuu na kwamba kikao cha Bunge
kitaendelea leo asubuhi kuanzia saa 2:00 kupokea taarifa ya Serikali kisha
watajadili mustakabali wa vikao vya Bunge.Kamati hiyo pia iliamua kutuma ujumbe
wa wabunge kwenda Zanzibar kuwafarijiwa wale wote walioathiriwa na ajali hiyo.
Imeandikwa na Salma
Said, Zanzibar, Neville Meena, Habel Chidawali na Boniface Meena, Dodoma;
Raymond Kaminyoge, Aidan Mhando, Dar es Salaam.
SOURCE: mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment