WAHESHIMIWA MADIWANI,
CCM NA TLP
HALMASHAURI YA MANISPAA
YA ARUSHA
YAH: MGOGORO WA MEYA
ARUSHA MJINI
Tafadhali husika na
kichwa cha habari hapo juu.
Sisi Madiwani wa CHADEMA
tumefikiri na kutafakari kwa kina kuhusu mustakabali wa maendeleo ya wananchi
wa Manispaa ya Arusha Mjini. Kwa nafasi yetu ya wawakilishi na utetezi wa
wananchi Arusha kwa umoja wetu ni vema tufikiri na tutafakari kwa kina kwa pamoja
hasa kipaumebele ikiwa ni kutanguliza HAKI na MAENDELEO katika kumlenga kila
mkazi wa aliyepo katika Halmashauri yetu. NI vema tukawa WAKWELI na WAZELENDO
kwa wananchi wetu wa Arusha, huku wote tukijua kwa kina kile kilichotokea
Arusha.
Kwa muda mrefu kumekuwa
na mgogoro wa Uchaguzi wa MEYA wa manispaa ya Arusha, ambayo ilitokana na
ukiukwaji wa kanuni na taratibu za uchaguzi wa Meya ambayo akidi yake ilikuwa
haijatimia. Ikumbukwe kuwa Mhe. Kivuyo ambaye katika sakata hilo alijikuta
akichaguliwa kwa hila kuwa NAIBU MEYA, alifikia hatua ya kujizulu nafasi hiyi
na kukiri mbele ya waandishi wa habari na wananchi wa Arusha kuwa uchaguzi
uliofanyika haukuwa wa haki na yeye alipewa nafasi hiyo kwa hila, kitu ambacho
baada ya tafakari ya kina aliamua kujiuzulu ili asiwe sehemu ya dhambi hiyo na
kujikuta anakalia KITI CHA DAMU. Jambo hili pia limekuwa likisemwa na baadhi ya
madiwani wa CHAMA CHA MAPINDUZI pindi tunapokutana nao kuwa mfumo wa chama cha
CCM unazuia kuyatamka haya lakini ukweli ni kuwa huo uchaguzi wa meya
uliofanyika na Mhe Gaudence Lyimo kupata nafasi hiyo ulikuwa batili kwa mujibu
wa kanuni, lakini mbaya zaidi, umepelekea damu kumwagika, jambo ambalo ndio
baya.
Wote tunashuhudia jinsi
ambavyo mgogoro huu ulivyo na madhara makubwa sana kwa wananchi wetu na sisi pia ambao ni
sehemu ya jamii hiyo hiyo. Mbali na kusababisha watu watatu kupoteza maisha,
pameendelea kutokea sintofahamu kubwa kutoka kwa wananchi jambo ambalo
limeendelea kuzidisha hasira kwa wananchi kwa serikali. Jambo hili ni vema likafanyiwa
kipimo maana mchezo huu na hila hii inaweza kuzaa balaa ambalo sio rahisi
kulimudu tena.
Dharau na makusudi
yanayofanywa na chama cha mapinduzi, mathalani Mhe Gaudence Lyimo na MKURUGENZI
wa halmashauri katika kupuuzia wito wa CHADEMA kuwa HAKI haikutendeka, KANUNI
zilivunjwa na hivyo uchaguzi wa MEYA ufanyike upya kwa kufuata kanuni sasa
inafika mahali haivumiliki na hapo ndipo itakuwa mikononi mwa wananchi na sio
CHADEMA tena.
Sambamba na hali hii,
pia mgogoro huu unatumiwa na watendaji wa Halmashauri kufanya mambo yao yasiyo ya kiuadilifu
kwani hakuna udhibiti wa kabisa katika uendeshaji wa halmashauri yetu.
Waheshimiwa madiwani, katika ukweli huu, MKURUGENZI na huyo anayeitwa MEYA
watatoa wapi ujasiri na kujiamini “moral authority” ili hali wao wameshiriki
dhambi mbaya ya kuchakachua kanuni za kufanya uchaguzi wa meya isivyo halali na
mbaya zaidi Mhe Gaudence kuendelea kung’ang’ania nafasi hiyo kwa kiwango cha
damu ya watu kumwagika bila hata kujali??
Hata hivyo, hata kama Mhe Gaudence Lyimo hatajali wito huu ambao kwetu ni
wito wa mwisho kwake na chama chake, jambo hili tunaliacha kwa MUNGU mwenye
HAKI atashughulika nae kwa wakati wake na muda si mrefu tutapata majibu ya
maombi yetu. Pili tunaliacha jambo hili kwa wananchi ili waamue kwa sababu
wameshajua wazi kuwa Mhe Gaudence Lyimo na chama chake waliamua na wameendelea
kuwafanyia uhuni katika mji wao. Sisi tumeliacha kwao waamue watakavyoamua.
Tunafahamu kabisa katika
nafsi na mioyo yenu mnafahamu uchaguzi haukuwa halali lakini mnashindwa
kusimamia ukweli kwa sababu ya ubinafsi na kukosa uzalendo kwa wananchi wa
Arusha kwa kutanguliza maslahi yenu mbele, kitu ambacho tusingependa kipewe
tafsiri hiyo
Tunawasihi kwa dhati
kabisa tuamue kwa pamoja kwa manufaa ya Arusha tukubaliane kama viongozi
wazalendo, wapenda maendeleo na wenye hofu ya MUNGU tufanye uchaguzi wa MEYA wa
Halmashauri ya Arusha ambao utakuwa ni halali kwa vyama vyote.
Nchi nyingi za Afrika
kumekuwa na vita vya wao kwa kwao kwa sababu ya uchu wa madaraka. Hili
limetokea pia hapa Arusha watu wamekufa kwa sababu ya MEYA, hii ni aibu na ni
dhambi kwa kung’ang’ania madaraka ambayo si haki.
Waheshimiwa madiwani
wenzetu hata juhudi za serikali kufanya maendeleo wananchi wengi wa Arusha bado
hawana imani na serikali yao
kwa sababu ya MEYA tu. Hivi sasa kuna mradi wa ujenzi w barabara unaondelea
ukweli ni kwamba jambo hili ni zuri lakini wananchi wanalibeza sana
kama vile linafanywa kwa hila. Kwa nini iwe
hivi??
Kimsingi tunataka MEYA
ambaye yupo huru kutembelea kata zote kwa ajili ya maendeleo bila kujali
itikadi ya chama chake. Hatutaki MEYA anayevizia misiba na harambee.
Mwisho tunamwomba Mh.
Gaudence Lymo atafakari kwa kina kwa kumuomba MUNGU wake ampe hekima na ujasiri
wa kuchukua maamuzi magumu ya kujiuzulu nafasi ya UMEYA na uchaguzi wa
kidemokrasia ufanyike kwani utampa heshima na amani katika maisha yake yote.
Tunaomba Waheshimiwa
Madiwani wenzetu kwa pamoja tuseme dhambi hii imetosha na tutubu kwa kufanya
uchaguzi wa haki na Amani. Na kwa dhati kabisa yeyote atakayechaguliwa hata kama ni Mh. Gaudence tutampa ushirikiano wa dhati kabisa.
Tunaomba ushirikiano
wenu katika jambo hili ambalo ni la msingi kwa maendeleo ya watu Arusha. Kila
mmoja kwa imani yake aombee jambo hili kwani halitaki ushabiki linahitaji
utulivu wa akili.
WAHESHIMIWA MADIWANI,
FANYENI TAFAKARI YA KINA, ZINGATIENI JINSI WANANCHI KATIKA KATA ZENU
WANAVYOWATAZAMA, ni matumaini yetu kuwa tutafanya uchaguzi wa MEYA ndipo
tufanye uchaguzi wa Naibu MEYA. Na jambo hili litakuwa ni ushindi na sifa
iliyotukuka kwa MADIWANI WOTE na sio kundi fulani la watu.
Asanteni sana
Doita Isaya Harri
Mwenyekiti madiwani wa
CHADEMA
Nakala:
Katibu wa CHADEMA (M)
Katibu wa CCM (M)
Katibu wa TLP (M)
No comments:
Post a Comment