Saturday, July 21, 2012

Futari yetu ya leo.

Ndugu zangu,

Leo natimiza ile ahadi yangu niliyowapa jana kuwa nitakuwa nawaletea futari ya kupika kila asubuhi. Maana katika umri wangu nimegundua watu wengi hupata tabu ya kuchagua futari ya kupika kwa jioni hiyo.

Na katika futari hizi nitahakikisha nachagua vyakula vyenye lishe, maana Mungu alituambia tufunge ili tupate afya. Lakini kutokana na uroho ama ulafi, waislamu wengi huchanganya vyakula vingi vya wanga, nyama na mafuta katika futari zao. Badala ya kupata afya matokeo yake wanapata maradhi.

Leo nitachagua futari tatu tu, Mihogo ya nazi ama ya kuchemsha, Chapati za kusukuma ama za maji (pan cake), tambi za sukari na samaki wa kukaanga, weka na maharage ama mchuzi wa kutolea (kula na) chapati. ukipata na bhajia za kunde ama dengu ni vema kuongezea. Usisahau chai ya mkandaa (black tea) ama ya maziwa, inasaidia kuchoma matumbo (michango) na kuifanya kuwa imara.

Baada ya hapo unywe juice ya matunda ama maji ya kutosha, lakini kwa wale ambao hawana mashine za kutengenezea juice (blender), wanaweza kula matunda yenyewe, maana matunda yana nyuzi nyuzi (fiber) hivyo husaidia mmengenyo (digestion) wa chakula. Ahsanteni, haya furahia futari yetu ya leo.

HAFIDH KIDO
0713 593894/ 0752 593894
DAR ES SALAAM,TANZANIA
21/07/2012
hafidhkido@yahoo.com

No comments:

Post a Comment