MBUNGE wa jimbo la
Ubungo, John Mnyika atakuwa ni mmoja wa mashahidi wa Serikali
watakaoithibitishia mahakama namna walivyohusika washtakiwa wanaotuhumiwa
kumuua Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Kata ya Ndago, Yohana
Mpinga (30).
Jeshi la Polisi mkoani
Singida, limemefikia azimio hilo baada ya
kumhoji Mnyika kwa saa tatu juzi usiku, kuhusiana na tukio hilo la mauaji lililotokea baada ya mkutano
wake wa hadhara uliofanyika Julai 14 mwaka huu, majira ya jioni.
Mahojiano hayo
yaliyoanza saa 11.53 jioni na kumalizika saa 3:15 usiku, yaliendeshwa chini ya
kikosi maalum cha askari wa upelelezi kutoka jijini Dar es Salaam kwenye ofisi
ya Kamanda wa Polisi mkoani hapa.
Habari zilizolifikia gazeti
hili jana zilithibitisha kwamba Jeshi la Polisi lilimtaka Mnyika awe tayari
kuitwa wakati wowote ili kusaidia kwenye kesi hiyo ya mauaji.
Tayari watu 18 wametiwa
mbaroni, miongoni wakiwemo wanachama wa Chadema, kwa tuhuma za kuhusika kwenye
mauaji ya kijana huyo wa CCM.
Mnyika alihojiwa huku
akiwa na wakili wa Chadema na mbunge wa jimbo la Singida Mashariki, Tundu
Lissu.
Mauaji hayo ya
mwenyekiti wa UVCCM yalifanyika Julai 14 mwaka huu saa 10 jioni huko katika
kijiji cha Nguvumali kata ya Ndago jimbo la Iramba magharibi.
Mauaji hayo yanadaiwa
kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na vurugu zilizotokea kwenye mkutano wa hadhara
ambao Mnyika alikuwa mgeni rasmi.
Katika hatua nyingine,
mshauri na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam (UDSM), Dk Kitila Mkumbo, ambaye alikuwa
ameambatana na Mnyika, alitarajiwa pia kuhojiwa kuhusiana na mauaji hayo jana.
Chanzo: www.mwananchi.co.tz

No comments:
Post a Comment