Jana
tarehe 18 Julai, 2012, majira ya alasiri kumetokea ajali ya kuzama kwa meli ya
MV SKAGIT katika eneo la Chumbe, Zanzibar .
Meli hiyo iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam
kueleka Zanzibar
ilikuwa imebeba watu 290. Kati yao watu wazima 250, watoto 31 na wafanyakazi wa
meli 9.
Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete aliagiza
vyombo vya ulinzi na usalama vya Serikali ya Muungano yaani JWTZ na
Polisi waanze kazi ya uokoaji mara moja.
Kazi hiyo imefanywa kwa kushirikiana na vyombo vya usalama vya Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar na meli za makampuni binafsi. Mpaka giza lilipokuwa
limeingia na hivyo kazi ya uokoaji kusitishwa mpaka kutakapokucha tarehe 19
Julai, 2012, watu 136 walikuwa wameokolewa na maiti 31 zilikuwa zimepatikana.
Aidha, mali
zilizokuwa kwenye meli hiyo hazikuweza kuokolewa.
Kufuatia ajali hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano alizungumza na Dkt. Ali
Mohamed Shein, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi. Alimpa pole kwa ajali iliyotokea hasa kwa vifo na majeraha
waliyopata Watanzania wenzetu na watu wasiokuwa raia wa Tanzania .
Alimuomba afikishe salamu za rambirambi kwa ndugu zetu waliopotelewa na jamaa
zao na kuwapa pole waliopata majeraha na maumivu maungoni mwao. Rais wa Jamhuri
ya Muungano alisema kuwa huu ni msiba wetu sote na kwamba majonzi yao ni majonzi yake na ya
Watanzania wote. Kwa ndugu zetu waliojeruhiwa tunawaombea kwa Mwenyezi
Mungu awape ahueni na wapone haraka ili waweze kuendelea na shughuli zao za kujiletea
maendeleo na kulijenga taifa letu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amempongeza Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein na
viongozi wote wa ngazi mbalimbali kwa uongozi wao thabiti tangu taarifa ya
kutokea kwa ajali mpaka sasa. Aidha, amewapongeza maafisa na askari wa
vyombo vya ulinzi na usalama na wafanyakazi wa meli binafsi, kwa juhudi kubwa
walizozifanya za uokoaji wa ndugu zetu waliopatwa na maafa haya makubwa na ya
aina yake. Amewataka waendeleze juhudi hizo leo na siku zijazo.
Rais amewataka wananchi wawe na moyo wa subira na uvumilivu wakati kazi ya
uokoaji inaendelea. Kama ilivyofanyika katika ajali ya MV Spice Islander
miezi 10 iliyopita, uchunguzi wa kina utafanyika kubaini chanzo cha ajali.
Kutokana na ajali hiyo na msiba huu mkubwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, ametangaza maombolezo ya taifa
ya siku tatu ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti kuanzia leo, tarehe 19
Julai, 2012.
Asanteni sana .
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
No comments:
Post a Comment