Kila la kheri
Zanzibar, bye bye Muungano!
Toleo la 250
18
Jul 2012
TUMEFIKA mahali na
wakati ambapo yatupasa tuliseme lililo dhahiri; kila la kheri Zanzibar , bye bye Muungano! Hakuna sababu ya kupigania
Muungano usiokuwapo; na Muungano usiokuwapo ambao pia ni dhaifu kupita kiasi
haufai kutetewa hasa kama hauna watetezi. Baada
ya kusema kauli zilizonukuliwa za mjane wa mzee Abeid Karume nahitimisha pasi
na shaka kuwa, mwamko wa kudai kuvunjwa kwa Muungano ambao unaendelea Zanzibar
si wa kikundi cha kidini kama tunavyotaka kuaminishwa bali ni mpango uliobuniwa
madhubuti na wanasiasa wa Zanzibar ambao hawataki kuendelea kuwapo kwa
Muungano.
Nikitambua ukweli wa sauti tunazozisikia
kutoka Zanzibar na hasa kukosekana kwa sauti
thabiti zenye kutetea Mapinduzi ya Zanzibar
ambayo yalizaa Muungano sina shaka yoyote kuwa hakuna namna nyingine yoyote ya
kuuokoa Muungano,. isipokuwa kuuvunja kwanza ili kila mtu aende na zake. Kama
imefika mahali hata mama Karume – ambaye mumewe na mwanae wamewahi kuwa marais
Zanzibar anaona kuwa hakuna faida ya Muungano na anakubaliana na madai ya wanauamsho
wa Zanzibar hakuna namna nyingine isipokuwa kuharakisha kujitoa kwa Zanzibar
kwenye Muungano ili waende na kuwa kile kisiwa cha neema ambacho kiliahidiwa na
wazee wako tangu enzi na enzi!
Mazingira yaliyoibua
Muungano hayapo tena
Mazingira yaliyosababisha Muungano mwaka
1964 hayapo tena. Wakati Muungano unatokea wakati ule Afrika ilikuwa katika
harakati za uhuru na nchi nyingi za kiafrika zilikuwa zinatoka kwenye makucha
ya wakoloni huku nyingine – kama Namibia ,
Zimbabwe
na Msumbiji (nikizitaja chache) – zikiwa kwenye harakati za uhuru.
Mazingira hayo ya kisiasa hayakuwa yameishia
katika harakati za uhuru tu bali pia mgawanyiko wa kambi mbili za dunia katika
Vita Baridi ulikuwa umekamilika. Miaka miwili nyuma dunia ilikuwa katikati ya
hatihati ya kuingia katika vita vya kinyuklia kutokana na mgogoro wa silaha wa Cuba . Hofu
iliyotokea baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ni
hisia kuwa Zanzibar ingeweza kugeuka kuwa “Cuba ya Africa ”.
Hata hivyo, mazingira makubwa zaidi ya
kuondolewa kwa usultani uliodumu kwa karne karibu tatu yalikuwa ni tishio kubwa
kwa watawala wapya wa Zanzibar .
Hakuna mtu aliyetarajia kuwa usultani ungeweza kuondolewa katika saa chache na
watu wenye silaha duni. Tishio la jaribio la kumrudisha sultani kwa wakati ule
lilikuwa dhahiri. Kwa watu wanaokumbuka historia Sultan Jamsheed aliomba msaada
wa askari kutoka Tanganyika
kuzima mapinduzi kitu ambacho Nyerere hakukubali.
Sultani hakupata msaada wowote kutoka bara
na msaada wa kutoka kwa binamu zake wa Oman usingeweza kuelekea visiwani hapo
bila kusababisha watu wa bara kuingilia kati na hata mataifa ya Magharibi
yaliyokuwa na maslahi visiwani humo yasingekaa pembeni.
Ili kuiokoa Zanzibar
Tanganyika ilijitoa muhanga
kwa kila namna hadi kukubali kufa ili Zanzibar
iwepo. Narudia sentensi hii, ili Wazanzibar wajue kuwa Tanganyika haijawahi kuwa adui wa Zanzibar bali imekuwa ni
zaidi ya rafiki; imekuwa ni ndugu. Tanganyika haikuwa ndugu wa maneno;
ilikuwa ni ndugu aliyekuwa tayari kufa ili mdogo wake aishi. Tanganyika imekufa ili Zanzibar iwepo.
Leo Zanzibar imekomaa na kunusurika na
tishio kubwa ndani yake Tanganyika
inaambiwa ni mkoloni. Tatizo ni kuwa Tanganyika
kwa kweli haikufa kabisa; ilikubali kulazwa nusu kaputi ili kuokoa uhai wa Zanzibar . Sasa Tanganyika
inaamka!
Kinyume na inavyolalamikiwa na wengi
jitihada za kuirejesha Zanzibar
katika uhai wake zilianza miaka karibu 30 nyuma. Zanzibar
ikapata baraza lake la kutunga sheria, Zanzibar
ikapata katiba yake, Zanzibar ikapata wimbo wake
wa taifa, na bendera yake na Rais wake mtendaji na hivi karibuni Zanzibar ikajitaja kuwa
ni nchi kamili.
Wakati huu wote Tanganyika
imeendelea kuilea Zanzibar ili ipate uhai wake;
tulidhania – kwa makosa makubwa – kuwa Zanzibar
itatambua kuwa ina undugu na ukaribu na Tanganyika kiasi cha kutaka
hatimaye kuwa nchi moja kamili. Walipopata vyote Zanzibar wanasema wanataka kutoka. Sasa ni
jukumu la Tanganyika
kuwasaidia kutoka.
Tumechoka kunyonywa!
Imekuwa ni kupe asiyetosheka na sasa
anaamini kuwa kwa kujitoa mgongoni mwa ng’ombe anamkomoa ng’ombe. Ati anadai
uhuru wake, ili awe kupe kamili. Tatizo ni kuwa hakuna namna yoyote kupe
ataweza kukaa bila kunyonya ng’ombe au mnyama mwingine. Zanzibar haiwezi kukaa bila kutegemea nchi
nyingine. Ama itategemea bara au itajaribu kutegemea Uarabuni au nchi nyingine.
Haina uwezo wa kusimama yenyewe hata watu
wake watamanie vipi. Tumaini pekee kuwa ikipata mafuta itageuka pepo ni ndoto
za Alinacha. Hata yakipatikana mafuta kesho inachukua miaka mingi kuweza
kubadilisha maisha ya wananchi. Ila yakipatikana mafuta Zanzibar
kizazi cha watawala kitanufaika sana hilo halina shaka. Ndio
kanuni ya “laana nyeusi”. Nani anatawala Zanzibar ?
Sasa sisi wa bara
nao tumekuwa wavumilivu mno na uvumilivu wa kutukanwa, kukejeliwa na
kudharauliwa na ‘kanchi’ kama Zanzibar
umetuisha. Kwa nini leo sisi tuliotoa “so
much” kwa ajili ya Zanzibar
kuonekana leo ati ndio “wakoloni”?
Leo hii tunatajwa kwa kejeli, muasisi wa
taifa letu akitukanwa hadharani na mtu pekee ambaye aliiokoa Zanzibar na kuipa uhai wake aonekane ni
kituko? Wakati wa kusema “imetosha” umefika. Zanzibar iamue kuondoka, na iondoke mwaka
huu! Hakuna haja ya kura ya maoni – wamuulize nani kama
hadi mke wa Karume anaposimama na kubeza Muungano? Wamuulize nani wakati leo
kitu ambacho kisingiwezekana Zanzibar
(Mpemba kutawala visiwa hivyo) kinawezekana kwa sababu ya Muungano na hakuna
mwenye ujasiri wa kujibu hoja dhidi ya Muungano?
Lini umesikia muswada umepitishwa Zanzibar kutoa upendeleo
kwa wananchi wa Mafia? Au wananchi wa Kilwa? Hawawezi kwa sababu mara moja
watadai “udogo wa visiwa”!
Sasa cha Tanzania
ni cha Watanzania wote (wakiwemo Wazanzibari) lakini cha Zanzibar ni cha Wazanzibari wote na si cha
Mtanzania yeyote. Kwa nini tuendelee na mfumo huu wa kinyonyaji? Kwa nini
tuendelee kuipa Zanzibar
upendeleo usiostahili. Zanzibar ina wasomi wengi
na ina watu wengi wako nje na wengi wako Bara; wakati umefika hawa wote warudi Zanzibar na kuanza kujenga nchi yao . Waachilie nafasi zao kwenye Muungano –
kwa kuanzia na Dk. Ghaib Bilal na wengine wote ili nafasi hizo zishikwe na
Watanganyika.
Tuwasaidie
Wazanzibari waache maandamano
Sasa sisi watu wa Tanganyika
(Tanzania
proper) tunaweza kuwasaidia Wazanzibar kuondoka kwenye Muungano ili waweze
kujenga taifa lao jipya lenye maziwa na asali; taifa ambalo wakipiga zumari
hadi maziwa makuu wanacheza; taifa ambalo kila mtu anaishi kwa furaha na kula
halua na tende huku wakicheza gombe sugu! Tuwasaidie Wazanzibar watoke kwenye
Muungano mapema zaidi kuliko ilivyo sasa.
Tusiwaache wafanye makongamano na maandamano
yasiyoisha kudai “uhuru kamili” wakati njia ya kuwapatia uhuru “kamili” ni
rahisi sana .
Niliandika huko nyuma kuwa njia rahisi zaidi ya kuwaondoa Zanzibar
kwenye Muungano ni kuwahamiza wawakilishi wao – kina Jussa na wenzake –
waandike sheria ya kura ya maoni ya kutoka kwenye Muungano na waitishe kura yao kabla ya mwisho wa mwaka huu ili hatimaye ifikapo
Disemba 31, 2012 Zanzibar
iwe taifa huru nje ya Muungano. Miezi imepita na sioni juhudi zozote za
Wazanzibari kutoka kwenye Muungano zaidi ya kuendelea kutuambia kuwa wanataka
kutoka!
Sasa kwa vile kina Jussa hawana ujasiri huo
na kwa vile wana uamsho hawana uwezo wala ujasiri wa kuwashawishi wawakilishi
wao kuitisha kura ya maoni mapema ili watoke kwenye Muungano sisi upande wa Tanganyika
inabidi tuwasaidie. Siyo kwa kuidai Tanganyika
kama wengine wanavyotaka tufanye; la hasha.
Tukiidai Tanganyika maana
yake tunataka Zanzibar iwepo na Tanganyika
iwepo ili kuwe na serikali tatu. Sasa tukiwa na serikali tatu bado Tanganyika
italipa gharama kubwa zaidi ya kuiendesha.
Kwa sababu huwezi kuwa na serikali tatu
ambazo hizo serikali mbili zinachangia 50 kwa 50, kwa sababu mara moja
itaonekana Zanzibar
inanyonywa. Itakuwaje watu milioni 45 wachangie sawa sawa na watu milioni
mbili? Wazanzibari hawa hawa wataanza kulia kuwa Tanganyika inawanyonya bado na
watataka tuchangie kwa “asilimia” huku wao wakitaka kuchangia asilimia kidogo
kwa sababu ni ‘wachache’ na uchumi wake ni ‘mdogo’. Tusikubali mkenge wa kudai Tanganyika .
Njia pekee ya kuwasaidia Wazanzibari kutoka
kwenye Muungano ili wasitusababishie maumivu ya kichwa ya kudumu ni kudai Tanzania moja,
nchi moja. Kwa vile Rais Kikwete na CCM wanasema hawataki tuuvunje Muungano
bali tujadili “muundo wa Muungano” naomba nipendekeze kuwa muundo pekee unaofaa
kwa Muungano ni wa “nchi moja, taifa moja”.
Hakuna mantiki ya kuwa na “nchi mbili ndani
Muungano”. Haiingii akilini uwe na “nchi ndani ya nchi”. Sasa kama nchi iko
ndani ya nchi haiwezekani kuwa na nchi mbili; bali moja. Ukiunganisha maji na
maji, huwi na maji mawili bali maji tu!
Sasa njia pekee ya kuwasaidia kuondoka
kwenye Muungano ni kudai “nchi moja taifa moja”. Inapopita timu ya kukusanya
maoni ya Katiba Mpya na linapokuja suala la Muundo wa Muungano watu wa bara
wasidai “serikali tatu”. Wadai “serikali moja”. Yaani kutakuwa na serikali ya
Muungano na tawala za mahali au serikali za mahali na mahali. Tayari tumeshakuwa
na serikali mbili na zimetuletea matatizo haiwezekani tukafikiria kuwa
tukiongeza serikali ya tatu tutakuwa tumepunguza matatizo. Haiwezekani ukiwa na
mtoto mmoja uone ni tatizo halafu ukiwa na watatu utakuwa umepunguza!
Hivyo, watu wa bara tunajua kabisa tukiimeza
Zanzibar rasmi – hakuna cha BlW (Baraza la Wawakilishi), hakuna Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar, hakuna bendera wala wimbo wa “taifa” la Zanzibar na hakuna
Rais wa Zanzibar wala chochote cha ‘Zanzibar”. Tunapoamua kuimeza ndani ya
taifa moja Zanzibar inakuwa sehemu kweli ya Jamhuri ya Muungano. Hili pendekezo
ndilo ambalo watu wa bara tunahitaji kulisimamia na kulidai kwenye mchakato huu
wa Katiba Mpya.
Kwa sababu Wazanzibar wenye uchungu na nchi
yao hawawezi kukubali. Hawawezi kukubali Zanzibar imezwe kabisa. Watakataa na
wataamua bora watoke. Uchaguzi utakuwa ni kumezwa au kutoka na wao watachagua
kutoka – kitu ambacho ndicho tunataka kuwasaidia kufanya. Sasa wakishatoka
Zanzibar isifikirie itakuwa na upendeleo maalumu kwa Tanganyika.
Baadhi ya vitu vya kwanza ambayo serikali ya
Tanzania Mpya itahitaji kufanya ni kuweka masharti makali ya ukaazi na uzawa
ili kwamba Wazanzibar wasije wakajipitisha kama
Watanganyika. Pamoja na hilo kuweka usimamizi
mzuri wa kodi ili kuhakikisha vitu vinavyoingia kutoka Zanzibar vinakidhi kiwango cha bara na kodi
nyingine muhimu. Tusije tukaacha kuwa baada ya kutoka Wazanzibari wakaanza
kupata upendeleo ambao walikuwa bado wanaupata. Tutatumia vigezo vile vile vya
kuhusiana na nchi kama Wakenya, Waganda na
Wanyarwanda.
Ndugu zangu katika
kuendeleza kampeni hii ya Let Zanzibar Goambayo
tumeiasisi tuanze kuitakia kila la kheri Zanzibar
na kusema “bye bye” Muungano.
Tuwasaidie watoke kwenye Muungano kwa kuanza kutaka kuundwa kwa serikali moja –
na si tatu. Hii ndio njia pekee, ya uhakika ya kuweza kuzungumzia suala la
“muundo wa Muungano” bila kutaka kuuvunja moja kwa moja (kitu ambacho sheria ya
katiba inakataza). Tukiidai serikali moja Wazanzibar hawatotaka watatoka nasi
tutaipata Tanganyika yetu na
ili kuzidi kuwaudhi maadui wa Muungano bado itapewa jina la Tanzania ; au tukipenda kurudisha jina la kale
zaidi la AZANIA !

No comments:
Post a Comment